Saturday, January 14, 2017

UHIWAI WASHUTUMIWA KWA KUTOWATETEA WAFUGAJI SIKONGE

Image result for sikonge
Na Mussa mbeho,Tabora

JUMUIYA ya Hifadhi za Wanyamapori Ipole (JUHIWAI) iliyopo wilayani Sikonge Mkoani Tabora imeshutumiwa na wananchi wa vijiji vya Utimule, Ngoywa, Msuva na Ipole kwa kushindwa kutetea au kukemea unyanyasaji kwa wafugaji.

Malalamiko hayo yalitolewa juzi mbele ya Mkuu wa wilaya hiyo Peresi Magiri ambapo walidai Jumuiya hiyo iliyopewa dhamana ya kutunza na kusimamia hifadhi hiyo ilipaswa kuwasaidia kukomesha vitendo hivyo na sio kuchochea.

Walidai viongozi wa Jumuiya hiyo kuendelea kukaa kimya wakati wanajumuiya waliowaweka madarakani wakionewa kila kukicha na mifugo yao ikikamatwa na kutozwa faini za mamilioni ya shilingi, hawawatendei haki wananchi hao.

Mzee Michael Shingwa mkazi wa Utimule alisema viongozi wa Jumuiya hiyo wamekuwa kama Mungu mtu kwa kufanya kile wanachotaka wao badala ya kutekeleza majukumu yao kama yalivyoelezwa katika katiba.

‘Hii Jumuiya ni yetu, lakini viongozi tukiwaita hawaji, wala mikutano hawaitishi, mapato na matumizi hawasomi, mifugo inakamatwa lakini hawatusaidii kwa lolote, wakati wanafahamu kilio chetu cha kila siku ni malisho na maji’, aliongeza.

Mzee Shiga Lubinza na Samson Jilala walisema JUHIWAI kama msimamizi mkuu wa hifadhi hiyo alipaswa kuwa mtetezi wao hata katika suala la kupata eneo la malisho lakini kitendo cha kuwaacha waendelee kutaabika kinawauma sana.

Wafugaji hao walimweleza DC kuwa Jumuiya hiyo haina msaada wowote kwa wananchi kwa kuwa vitendo wanavyofanyiwa na Maafisa wa Maliasili wakiwemo askari wa hifadhi hiyo hata viongozi wao wanahusika.

‘Hatuoni faida ya kuwepo kwa JUHIWAI ni afadhali ifutwe kwa sababu haitusaidii lolote, imeshindwa kutusaidia kupata eneo la kulishia mifugo, badala yake tunalima na kulisha mifugo yetu kwa kujibana katika kaeneo hakohako’, aliongeza.

Diwani wa kata ya Ngoywa Lucas Kiberenge alisema malalamiko ya wananchi hao ni ya msingi sana ila akabainisha kuwa JUHIWAI sio mbaya ila baadhi ya viongozi wake ndio wabaya.

Alisema tatizo la uongozi wa Jumuiya hiyo ni kutokaa meza moja na wananchi hao ili kusikiliza kero zao na kutoa ufafanuzi wa malalamiko yanayoelekezwa kwao, hivyo akashauri uongozi kupanga ratiba ya kukutana na wananchi ili kutoa majibu ikiwemo kufafanua wapi wachungie
mifugo yao na wapi wasiingie.

No comments:

Post a Comment

bila kutumia lugha ya matusi na kumharibia mtu siku
yake