Monday, January 16, 2017

Wachina 20 waishi nchini kinyume

Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana na Ajira, Antony Mavunde
RAIA 20 wa China wamekutwa wakiishi nchini kinyume cha sheria katika kiwanda cha kuchenjulia dhahabu cha Mgodi wa Sunshine kilichopo Matundasi wilayani Chunya mkoani Mbeya.

Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana na Ajira, Antony Mavunde alibaini uwepo wa raia hao alipofanya ziara ya kushtukiza katika kiwanda hicho jana.

Katika ziara hiyo, Naibu Waziri huyo alipata nafasi ya kuzungumza na watumishi ambao walilalamikia kunyanyaswa na raia wa Kichina ambao ndiyo wasimamizi wa shughuli za mgodini hapo kwa kufanya kazi ambazo pia zinaweza kufanywa na Watanzania.

Mbali na kugundua Wachina hao kuishi nchini bila kibali pia hawakuwa na vibali vya kufanya kazi nchini na badala yake walikuwa na vibali vya kuishi Tanzania ambavyo vilikuwa vimeisha muda wake tangu mwaka 2015.

Naibu Waziri pia alibaini mapungufu 12 ya ukiukwaji wa sheria ya usalama mahali pa kazi ambapo mwajiri alikuwa hana sera ya usalama mahala pa kazi, upungufu wa vitendea kazi, ukosefu wa huduma ya kwanza, wafanyakazi kutopima afya zao, kutokuwa na chama cha wafanyakazi na kutofanyika kwa ukaguzi wa umeme.

Aliongeza kuwa upungufu mwingine uliogunduliwa ni pamoja na kuongeza eneo la kambi bila ruhusa kutoka mamlaka inayohusika, kutozingatia muda wa kazi wa watumishi, kima cha chini cha mshahara kwa watumishi na kutoa mikataba ya kazi kwa miezi mitatu kinyume cha sheria na utaratibu wa ajira.

Kutokana na upungufu huo Naibu Waziri Mavunde alikitoza faini ya Sh milioni 14 kwa kushindwa kufuata utaratibu na sheria ya usalama wa mahali pa kazi, pia aliagiza raia wote wa Kichina wakamatwe na kufikishwa ofisi za Uhamiaji kwa ajili ya taratibu za kurudishwa makwao kutokana na kutokuwa na vibali vya kuishi nchini na kufanya kazi.

Awali Mkuu wa Wilaya ya Chunya, Rehema Madusa alimwambia Naibu Waziri kuwa tangu aanze kazi Chunya amekuwa akipokea malalamiko kutoka kwa wafanyakazi wa Sunshine wakilalamikia kunyanyaswa na Wachina na kufanyishwa kazi kwa muda mwingi bila mapumziko, likizo na malipo ya ziada.

HABARI LEO

No comments:

Post a Comment

bila kutumia lugha ya matusi na kumharibia mtu siku
yake