ANGALIA LIVE NEWS

Friday, February 10, 2017

DKT. MPANGO AZIHIMIZA KAMPUNI KUCHANGAMIKIA FURSA ZA SOKO LA HISA LA DAR ES SALAAM (DSE)

Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt. Philip Mpango

Benny Mwaipaja-WFM, Dodoma
WAZIRI wa Fedha na Mipango, Dkt. Philip Mpango, amezitaka Kampuni kubwa na za kati kuchangamkia fursa ya uwepo wa Sekta ya Soko la Mipaji, kwa kujiorodhesha katika soko la hisa la Dar es salaam ili kushiriki moja kwa moja katika umiliki wa uchumi wa nchi.

Dkt. Mpango ametoa rai hiyo Bungeni Mjini Dodoma, wakati akijibu swali lililoulizwa na Mbunge wa Jimbo la Magomeni, Mhe. Jamal Kassim Ali, aliyetaka kujua mchango wa Mamlaka ya Masoko ya Mitaji na Dhamana (CMSA) na Soko la Hisa la Dar es saam (DSE), kwa wafanyabiashara wazawa.

Alifafanua kuwa kampuni kadhaa, ikiwemo Kampuni ya Bia Tanzania (TBL), TOL Gases, Kiwanda cha Sigara (TCC), Kiwanda cha Saruji Tanga, Wakala wa Huduma za Mizigo kwenye viwanja vya ndege-Swissport na Benki ya NMB, ni baadhi ya kampuni zinazouza hisa zake katika Soko la Hisa la Dar es salaam.


Dkt. Mpango alisema kuwa kampuni hizo zimechangia kukuza uchumi wa nchi ikiwemo ajira, kutoa gawiwo kwa Serikali na wanahisa, lakini pia ni miongoni mwa walipa kodi wakubwa.


“Kwa mfano kwa mwaka 2015 NMB, ilitoa gawiwo Serikalini kiasi cha shilingi bilioni 16.5 na TCC shilingi billion 1.4 kwa hisa zinazomilikiwa na Serikali huku mapato yatokanayo na kodi pamoja na gawiwo, hutumiwa katika kutoa huduma mbalimbali ambazo jamii ikijumuisha wafanyabiashara wadogo hunufaika nazo”alisema Dkt. Mpango

“Vilevile, Serikali imekuwa ikitumia masoko ya mitaji kama chanzo cha upatikanaji wa fedha za bajeti (Treasury Bonds), Miradi inayotekelezwa na fedha hizi, pamoja na mambo mengine, imekuwa ikitoa ajira na fursa za kibiashara kwa wafanyabiashara wazawa; wadogo na wa kati” aliongeza Dkt. Mpango

Dkt. Mpango, alibainisha kuwa Serikali inatambua mchango mkubwa wa kampuni ndogo ndogo katika kukuza uchumi wa nchi ndio maana mwaka 2013 Soko la Hisa la Dar es Salaam lilianzisha dirisha linaloziwezesha kampuni ndogo na za kati za wazawa zisizokidhi vigezo vya kujiunga na soko hilo kupitia dirisha kuu, kutumia Soko la Hisa katika kupata mitaji kutoka kwa umma wa watanzania.

Dkt. Mpango alibainisha kuwa watanzania wengi wananufaika na uwepo wa soko la hisa, na kushiriki moja kwa moja katika umiliki wa uchumi wa nchi huku akizitaja baadhi ya kampuni zilizonufaika na utaratibu huo wa dirisha dogo la hisa  kuwa ni Benki ya Mwalimu Commercial Bank, Swala Oil and Gas Tanzania, Maendeleo Bank PLC, Yetu Microfinance na Mkombozi Commercial Bank, ambazo zina jumla ya mitaji isiyopungua shilingi bilioni 120.

No comments: