Na Mussa Mbeho, Katavi
HALMASHAURI ya wilaya ya Nsimbo Mkoani Katavi imeanza kuweka mikakati thabiti itayosaidia kukomesha na kutokomeza mimba za utotoni kwa wanafunzi wa shule za msingi na sekondari ili kuweza kuwasaidia kusoma na kufikia malengo yao.
Akizungumza na mwandishi wa gazeti hili ofisini kwake Mkurugenzi Mtendaji wa halmashauri hiyo Mairwa Pangani alisema Kuwa kwa sasa wamedhamiria kukomesha vitendo vya mimba mashuleni kwa kuweka mikakati mikali kwa walimu,wazazi na wanafunzi wenyewe.
Alisema kuanzia sasa wale wote watakaobainika kuwapa ujauzito wanafunzi watakamatwa mara moja na kukabidhiwa kwa vyombo vya dola kwa ajili ya kufikishwa mahakamani ili sheria ichukue mkondo wake.
Alibainisha mikakati iliyowekwa na halmashauri hiyo kuwa ni kuhakikisha zoezi la upimaji ujauzito linafanyika mara kwa mara kwa mabinti wa shule za msingi na sekondari huku akiwataka walimu wa shule zote kutoa ushirikiano wakati wa zoezi hilo.
Pangani alisema wataendelea kushirikianas na wadau wa elimu wilayani humo wakiwemo wazazi na walezi wa watoto hao ili kuweka mikakati ya pamoja itakayosaidia kudhibiti vitendo hivyo hata wakiwa nyumbani ili kuwasaidia waweze kusoma na kufikia malengo yao.
Aidha Pangani alibainisha kuwa walimu wote watatakiwa kufanya ukaguzi wa mara kwa mara kwa wammafumzi wanaoishi katika shule zenye mabweni ili kuhakikisha hakuna mwanafunzi anaeweza kulala nje kwa lengo la kudhibiti tatizo la mimba katika halmashuri hiyo
Pangani Alifafanua mkakati mwingine kuwa ni kuhakikisha walimu wanawajengea hali ya ujasiri na kujiamini wanafunzi wao ili kuondokana na woga wa kukubali udanganyifu wa wanaume huku akikisitiza vipindi vya dini kutiliwa mkazo katika shule zote ili kuwajengea imani sambamba na kuwa na hofu ya Mungu.
Aidha aliwataka walimu wakuu na wakuu wa shule za msingi na sekondari kuhakikisha wanawabana walimu wa madarasa katika kufuatilia mienendo ya wanafunzi wao na kubainisha taarifa za kila mwanafunzi kwa kila muhula huku mkuu wa shule akitakiwa kuwa na njia mbadala ya kupata taarifa za wanafunzi kutoka kwa wazazi moja kwa moja.
Naye Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo Rafael Kalinga aliwataka Madiwani, Watendaji na Watumishi wote wa halmashauri hiyo kutoa ushirikiano wa hali ya juu utakaosaidia kutiwa mbaroni wanaume wote wanaorubuni wanafunzi ikiwemo wazazi watakaoozesha watoto wao wa kike walio chini ya miaka 18.
Kwa upande wake Mkuu wa wilaya ya Mpanda Bi Lilian Matinga ambae anasimia halmshauri hiyo ametoa onyo kali kwa walimu wote watakaobainika kujihusisha na vitendo vya kurubuni wanafunzi wao wa kike ili wafanye nao mapenzi huku akisema kuwa hatua kali za kisheria zitachukuliwa dhidi yao.
No comments:
Post a Comment