ANGALIA LIVE NEWS

Friday, February 3, 2017

MAGARI MANNE YAGONGANA BARABARA YA NYERERE ENEO LA MTAVA JIJINI DAR ES SALAAM NA KUMJERUHI DEREVA TEKSI

 Wananchi wakimuangalia dereva wa teksi aliyejeruhiwa baada ya gari lake lenye namba za usajili T 625 AWS kugongana na gari dogo lenye namba usajili T 214 CFX wakati likiingia barabara ya Nyerere likitokea Jengo la Kibiashara la Quality Centre Dar es Salaam leo asubuhi.
 Mwonekano wa Teksi hiyo namba T 625 baada ya kugongana.
 Wananchi wakiangalia ajali hiyo.
 Wananchi wakiangalia gari dogo aina ya Toyota Corolla lenye namba T 214 CFX baada ya kuyagonga magari namba T 741 DEK na T 596 BCG katika eneo hilo la Mtava.
 Askari wa Usalama Barabarani akipima ajali hiyo.
 Gari dogo aina ya Toyota Corolla lenye namba T 214 CFX likiwa eneo la ajali kabla ya kuondolewa.

Na Dotto Mwaibale
DEREVA wa gari dogo teksi yenye namba za usajili T 625 AWS amenusurika kufa baada ya gari lake alilokuwa akiliendesha kutoka mjini akielekea Uwanja wa Ndege kugongana na gari dogo lenye namba T 214 CFX aina ya Corolla lililokuwa likiingia Barabara ya Nyerere likitokea Jengo la Biashara la Quality Centre eneo la Mtava jijini Dar es Salaam leo asubuhi.

Mashuhuda wa ajali hiyo wakizungumza na waandishi wa habari eneo la ajali walisema ajali hiyo ilisababishwa na gari hilo dogo aina ya Corolla lililokuwa likiingia barabara ya Nyerere bila kuchukua tahadhari.

"Chanzo cha ajali hii ni gari hilo dogo aina ya corolla ambalo liliingia barabara ya Nyerere bila ya dereva wake kuchukua tahadhari na kama dereva wa gari namba T 625 AWS angekuwa katika mwendo wa kawaida madhara yake yasingekuwa makubwa kiasi hicho" alisema shuhuda aliyejitambulisha kwa jina la Mlugulu.

Mlugulu alisema baada ya magari hayo kugongana gari hilo aina ya Corolla liligeuka na kwenda kuyagonga magari mengine namba T 596 BCG na T 741 DEK yaliyokuwa yamesimama yakisubiri kuingia upande ambao lipo Jengo la Kibiashara la Quality Centre.

Katika ajali hiyo gari namba T 625 AWS liliacha njia na kuhamia upande wa pili wa barabara ya kutoka Tazara kwenda mjini.

Baada ya ajali askari wa usalama barabarani walifika na kupima ajali hiyo na kuchukua maelezo ya madereva wote wanne ambapo magari mawili T 214 CFX na T 625 AWS yakiondolewa na  magari ya kukokota magari mabovu (Breck Down) na kupelekwa kituo cha Polisi cha Chang'ombe Temeke jijini Dar es Salaam kwa hatua zingine za kisheria.

No comments: