Siku chache baada ya Ruth Segeleti (52) kufukua kaburi la mtoto wake, Baraka Mwafongo (22) kwa imani kwamba angefufuka baada ya siku tatu, imeelezwa kwamba mama huyo alifanya hivyo akidaiwa kwamba aliota kuwa mtoto wake atakuwa nabii.
Akisimulia maisha ya mwanamke huyo, balozi wa nyumba 10, katika Mtaa wa Shigamba, Shaban Anangisye alisema mzazi huyo wa watoto wanne wakiwamo wa kike watatu na marehemu ambaye alikuwa mwanamume pekee, aliwaambia wanawake wenzake siku moja baada ya kumzika marehemu kwamba aliota ya kuwa mwanaye ni nabii na hajafa.
Alisema aliwaarifu majirani, lakini walisita kufika kwenye msiba huo kwa vile mwanamke huyo hakufahamika sana kutokana na ugeni wake na kushinda ndani akimuuguza mtoto wake ambaye alikuwa akiumwa tangu 2013.
Anangisye alisema majirani waliamua kuhudhuria mazishi baada ya yeye kuwaelezea ukweli kwamba tangu amehamia hapo amekuwa na mgonjwa hivyo kushindwa kuhudhuria misiba ya majirani.
“Watu walijitokeza kuzika na majirani walibaki kumliwaza. Lakini usiku aliwaambia wenzake kwamba mtoto wake atafufuka.”
Anangisye alisema baada ya kusimulia hayo, alidamka alfajiri kwenda kufukua kaburi na alionekana akirudi na jembe pamoja na furushi la nguo akitokea makaburini. “Wanawake wenzake walipomwona walikwenda mbio makaburini na kuona kaburi likiwa limefukuliwa ndipo walipokuja kwangu kunieleza ili tuwaarifu polisi,’’ alisema.
Alisema alipiga simu polisi ambao walifika na kuomba kibali cha Mahakama kufukua kaburi hilo ambalo walikuta sanduku tupu na ilibainika baadaye kuwa mwili wa marehemu umelazwa kwenye banda la mwanamke huyo.
Anangisye alidai kwamba mwanamke huyo alikiri kufukua kaburi hilo akisaidiwa na vijana wawili aliowapa Sh5,000 kila mmoja na kwamba alimbeba mtoto wake mgongoni hadi kwenye banda alilomweka akisubiri mchungaji afike kumwombea ili afufuke.
Alisema baada ya maneno hayo alichukuliwa na pamoja na hadi kituo cha polisi huku mwili wa marehemu ukipelekwa Hospitali Teule Ifisi.
Baada ya kuenea kwa taarifa za tukio hilo, wananchi walivamia nyumba ya mama huyo na kuichoma moto. Polisi walilazimika kutumia mabomu ya machozi kuwatawanya na jana, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya Dhahiri Kidavashari alisema watu saba wamekamatwa kwa tuhuma hizo na wapo nje kwa dhamana.
No comments:
Post a Comment