ANGALIA LIVE NEWS

Thursday, February 2, 2017

MKUU WA MKOA AMGOMEA WAZIRI MAGHEMBE

Uamuzi uliofanywa wiki iliyopita na Waziri wa Maliasili na Utalii, Professa Jumanne Maghembe wa kuagiza kuendelea mchakato wa kulitenga eneo la pori tengefu la Loliondo umepingwa na Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Mrisho Gambo.

Badala yake, RC Gambo ameagiza Kamati ya wataalamu iliyoundwa kwa maelekezo ya Waziri Mkuu, Khasimu Majaliwa inayochunguza chanzo cha mgogoro wa Loliondo iendelee na kazi iliyopewa na hatimaye itoe mapendekezo yake ya namna ya kumaliza mgogoro huo uliodumu kwa miongo miwili.

Gumbo alikuwa akizungumza jana katika mkutano wa wadau wa vyombo vya habari   katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Arusha (AICC).

Alisema hakuna kiongozi yeyote mwenye mamlaka ya kukosoa au kusimamisha maagizo ya Waziri Mkuu isipokuwa Makamu wa Rais na Rais. 


RC Gumbo alionekana dhahiri kuwa amekerwa na kukasirishwa na uamuzi wa Waziri Maghembe wa kufanya ziara ya kushtukiza katika eneo la Loliondo na   kutoa maagizo ya kugawa eneo la kilometa za mraba 1500  kuokoa Hifadhi ya Serengeti.

Alisema uamuzi uliotolewa na waziri  huyo ni ushauri kwa kamati yake na jambo linalozusha sintofahamu juu ya mwenye mamlaka zaidi kati ya Waziri na Mkuu wa Mkoa . 

“Hakuna kiongozi mwingine yeyote mwenye kukosoa maagizo au maelekezo ya Waziri Mkuu isipokuwa Makamu wa Rais na Rais.

“Sisi kauli ya waziri tunaichukulia kama ushauri ambao unaweza kutolewa na mwananchi yeyote, ” alisema.

Alisema ni lazima kamati ya wataalamu aliyoundwa ikamilishe kazi yake ikiwa ni pamoja na kujiridhisha kuhusu mipaka, vyanzo vya maji, maeneo ya ufugaji, uhifadhi, mipaka ya vijiji na hatimaye  kuwasilisha mapendekezo yake serikalini   yafanyiwe kazi na si vinginevyo.

Mkuu huyo wa Mkoa alishangazwa na uelewa na umakini wa Wizara ya Maliasili na Utalii katika kulitambua na kufuatilia eneo la pori tengefu.

RC Gumbo alisema inaelekea  wataalamu wa wizara hawana uelewa wowote kuhusu kinachoendelea Loliondo.

“Wizara inazungumzia pori tengefu lakini tayari kuna mji pale, hata eneo la kilometa za mraba 1500 wanazosema tumewauliza inaanzia wapi na kuishia wapi hawajui.

"Hata aliyechora ramani naye hajui mipaka ndiyo maana nasema tuache kamati imalize kazi yake," alisema.

No comments: