Advertisements

Sunday, February 26, 2017

MSIGWA: RAIS AMESIKILIZA BUNGE

Mbunge wa Iringa Mjini (Chadema), Mchungaji
By Fredrick Nwaka, Mwananchi fnwaka@mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Mbunge wa Iringa Mjini (Chadema), Mchungaji Peter Msigwa amesema mshikamano wa wabunge ulioweka pembeni tofauti za kiitikadi unaonyesha Bunge linaweza kurejesha nguvu zake iwapo halitaingiliwa katika utendaji.

Mchungaji huyo wa Kanisa la Vineyard amesema hata uamuzi wa Rais John Magufuli kumteua Rogers Sianga kuwa Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Kupambana na Kuzuia Dawa za Kulevya umedhihirisha nguvu hiyo ya Bunge.

Msigwa alikuwa akizungumza na Mwananchi katika mahojiano maalumu jijini Dar es Salaam wiki iliyopita.

Mbunge huyo wa Iringa Mjini alisema Rais Magufuli alifanyia kazi hoja za wabunge baada ya kitendo cha Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda kutangaza majina ya watu akiwahusisha na dawa za kulevya, kulalamikiwa na wabunge.

Makonda alitangaza majina ya wasanii, wanasiasa, wafanyabiashara na viongozi wa dini akiwataka kuripoti Kituo Kikuu cha Polisi cha Dar es Salaam kwa ajili ya mahojiano kuhusu matumizi na biashara ya dawa za kulevya, jambo lililopingwa na watu wengi, na hasa wabunge.

Wakizungumza katika mkutano uliopita, wabunge walisema wanaunga mkono vita hiyo, lakini hawakubaliani na kitendo cha kutangaza watuhumiwa na wengine wakasema chombo kinachostahili kuendesha vita hiyo ni mamlaka ambayo tangu iundwe kisheria haikuwa imepata watendaji wake.

Siku chache baadaye, Rais Magufuli alimteua Sianga na watendaji wengine, ambao mara moja wakaanza utekelezaji wa majukumu yao.

Uteuzi huo umemfanya Msigwa kuamini kuwa Bunge linaweza kuwa na sauti moja lisipoingiliwa kiutendaji.

“Hakuna asiyeunga mkono vita hii lakini approach (mbinu) ya Makonda haikuwa na mamlaka kisheria na ndiyo maana Rais ametusikiliza (wabunge) na kumteua mtu atakayesimamia jambo hilo kisheria,” alisema Mchungaji Msigwa.

“Vita hii inatuhitaji wote; kuanzia kamishna, vyombo vingine vya usalama, viongozi na wananchi wote na si kwa kuitana kwa kutumia redio na televisheni, huko hatutafika zaidi ya kuishia kudhalilishana na kuchafuana,” alisema mbunge huyo machachari.

Aidha, Msigwa ambaye aliingia bungeni kwa mara ya kwanza 2010, alifananisha hatua ya Makonda na baadhi ya wakuu wa wilaya na mikoa nchini kujitwisha mamlaka ya kuwaweka mbaroni wananchi na waandishi wa habari, akisema wengi wanaendeleza chuki baada ya kuangushwa kwenye kura za maoni ndani ya CCM.

“Wengi wao ni wale walioshindwa kwenye kura za maoni ndiyo wanawaharibia sifa wabunge waliochaguliwa majimboni,” alisema

Chaguzi ndani ya Chadema

Mchungaji Msigwa pia alizungumzia chaguzi za ndani ya Chadema kwa ajili ya kusimika viongozi wa kanda, ukiwamo wa Desemba mwaka jana uliompa mbunge huyo uenyekiti wa Kanda ya Nyasa inayojumuisha mikoa ya Mbeya, Iringa, Rukwa na Songwe.

Uchaguzi huo nusura uingie dosari baada ya kamati kuu kuondoa jina la Makamu Mwenyekiti wa Baraza la Vijana wa Chadema (Bavicha), Patrick Ole Sosospi.

“Uchaguzi ulikuwa na kashikashi kwa kuwa kuna watu wako nje ya Chadema na hawakutaka nichaguliwe,” alisema Msigwa akidai kuwa hoja ya waliokuwa wakitaka asigombee ni kutokana na kuwa mbunge.

“Mbona (John) Heche ni mbunge na Mwenyekiti wa Kanda ya Serengeti? (Cecil) Mwambe ni mbunge na Mwenyekiti wa Kanda ya Kusini na (Kasuku) Bilago ni mbunge na Mwenyekiti wa Kanda ya Magharibi?.

“Katiba yetu iko wazi, Kamati Kuu ndiyo yenye mamlaka ya mwisho ya kuteua wagombea. Hata kwenye uchaguzi mkuu kuna wagombea walishinda katika kura za maoni, lakini Kamati Kuu iliwaengua.”

Msigwa alidai kuwa kuna watu hawakutaka awe mwenyekiti ili wakimalize chama Kanda ya Nyasa, lakini akasema “wana bahati mbaya”.

Msigwa alisema kuchaguliwa kwake kuongoza Kanda ya Nyasa kunalenga kuhakikisha Chadema inavuna ushindi mnono katika Uchaguzi Mkuu wa 2020.

“Tumedhamiria kuhakikisha Kanda ya Nyasa inashinda kata na majimbo mengi kuliko kanda yoyote ili kurahisha ushindi wa kiti cha urais. Hizi ni salamu kwa wote wenye nia mbaya na chama hiki,” alisema.

Utawala wa Awamu ya Tano

Kuhusu utawala wa Serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Rais Magufuli, mbunge huyo alisema umewafanya watu kuwa na hofu, huku akidai kuwa mkuu huyo wa nchi haiamini CCM.

Msigwa alisema Serikali ya Awamu ya Tano haikubali kukosolewa.

“Mwalimu Nyerere hakujenga majengo, lakini fikra zake zinadumu mioyoni mwa watu. Utawala huu ni wa watu waoga,” alisema Msigwa. “Haujiamini na hauko tayari kukosolewa. Wamevuruga Bunge kwelikweli.”

Alikuwa akizungumzia uamuzi wa Serikali wa kutoruhusu baadhi ya shughuli za Bunge kurushwa moja kwa moja na vituo vya televisheni, kupiga marufuku mikutano ya hadhara ya kisiasa na kukamatwa mara kwa mara kwa viongozi wa upinzani.

Pia alisema Rais Magufuli haiamini CCM na ndiyo maana amefanya mabadiliko ya katiba ya chama hicho yaliyopunguza idadi ya wajumbe wa vikao vikuu na kuondoa baadhi ya nafasi za utendaji.

“Rais Magufuli haamini CCM inapigania nini na inataka nini,” alisema.

“Anafanya vitu vinavyotofautiana na Chama cha Mapinduzi. Watendaji wa chama hawaheshimiwi. Haya mabadiliko yaliyofanywa yanalalamikiwa na watendaji wa chini ambao wanatumia muda mwingi kufanya kazi za chama.

“Chama ni chambo tu, Magufuli anaamini kuna vyombo vilivyojificha chini ya CCM kuwa ndivyo vinaendesha nchi.”

Hata hivyo, Mabadiliko anayozungumzia Msigwa, yalipendekezwa na Kamati Kuu ya CCM na baadaye kupitishwa na kikao cha Halmashauri Kuu kilichofanyika Desemba 13, 2016 na sasa yanasubiri baraka za Mkutano Mkuu.

Miongoni mwa mabadiliko hayo ni kupunguza wajumbe wa Halmashauri Kuu kutoka 388 hadi 158, na wajumbe wa Kamati Kuu kutoka 34 hadi 24.

Utumishi kwa wananchi wa Iringa Mjini

Akizungumzia kipindi chake cha kuwatumikia wananchi wa Iringa Mjini, Mchungaji Msigwa alisema kazi yake ni kuhakikisha anakuwa daraja bora kati yao na Serikali.

“Ninajivunia wananchi wangu wa Iringa. Kazi kubwa tunayofanya ni kuhamasisha wananchi kutambua wajibu na haki zao. Nimelia nao na nimecheka nao katika vipindi vyote. Nimekamatwa na kuwekwa ndani lakini sijaacha kuwatumikia,” alisema Msigwa.

Alisema hivi sasa huduma ya majisafi na salama inapatikana kwa zaidi ya asilimia 90 ya wananchi wa jimbo lake.

“Tumegusa maeneo yote, huduma za afya na elimu pia zimeimarika kwa ushirikiano wa viongozi na wananchi. Bado kuna muda mrefu kutekeleza mambo mengine,” alisema Msigwa.

No comments: