Muonekano wa baadhi ya Nyumba zinazojengwa na Wakala wa Majengo Nchini (TBA) Bunju, nje kidogo ya jiji la Dar es Salaam zikiwa katika hatua za mwisho za ujenzi wake.
Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Majengo Nchini (TBA), Arch. Elius Mwakalinga, akifafanua hatua iliyofikiwa kwenye ujenzi wa nyumba kwa Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Eng. Edwin Ngonyani, alipokagua maendeleo ya ujenzi wa nyumba hizo jijini Dar es Salaam.
Muonekano wa moja ya mtungi wa kutengenezea gesi ukaa (Biogas), inayoendelea kujengwa katika Nyumba zinazojengwa na Wakala wa Majengo Nchini (TBA), eneo la bunju jijini Dar es Salaam. Gesi hiyo itatumika kutoa huduma kwa wakazi wa eneo hilo.
Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Majengo Nchini (TBA), Arch. Elius Mwakalinga (wa tatu kulia), akimuonyesha Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Eng. Edwin Ngonyani, hatua iliyofikiwa kwenye ujenzi wa hosteli za Chuo Kikuu cha Dar es Salaam zinazojengwa na Wakala huo.
Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Eng. Edwin Ngonyani wa pili kulia), akitoa maelekezo kwa Uongozi wa Wakala wa Majengo Nchini (TBA), alipokagua maendeleo ya ujenzi wa hosteli za wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam. Kulia ni Meneja Kikosi cha Ujenzi cha TBA, Arch. Hamphrey Killo.
Muonekano wa moja ya
jengo la hosteli ya wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam ambalo
limekamilika na majengo hayo yataanza kutumika wiki ijayo kufuatia ujenzi wake
kukamilika.
Naibu Waziri wa
Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Eng. Edwin Ngonyani ameupongeza Wakala wa
Majengo Nchini (TBA), kwa jitihada wanazozifanya
katika kuongeza mapato na kununua vifaa vipya na kisasa vitakavyowezesha wakala
huo kumudu ujenzi wa miradi mingi mikubwa kwa wakati.
Akizungumza mara baada
ya kukagua mradi wa nyumba 851 ulioko Bunju nje kidogo ya jiji la Dar es Salaam
na mabweni ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Eng. Ngonyani ameeleza kuridhishwa
kwake na mabadiliko makubwa ya utendaji yanayoendelea katika wakala huo.
“Nawapongeza kwa kazi
nzuri ya ujenzi wa nyumba za kisasa za makazi ya watu, ongezeni ubunifu
ili nyumba zote zinunuliwe na
kuwawezesha Watanzania kupata makazi bora kwa bei nafuu’ amesema Eng. Ngonyani.
Ameitaka TBA
kuhakikisha inapata faida ili kuchangia katika mfuko mkuu wa Serikali kama
ilivyo kwa taasisi nyingine za Umma na hivyo kuiwezesha Serikali kuongeza kasi
katika utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo.
‘Ongezeni kasi katika
ukusanyaji wa madeni kwa watu binafsi wanaokaa kwenye nyumba zenu na sisi Wizarani
tutawasaidia katika kuhakikisha mnalipwa kwa wakati kwa wadaiwa wa Serikalini’
amesisitiza Eng. Ngonyani.
Katika hatua nyingine
Naibu Waziri huyo ameelezea kuridhishwa kwake na kasi ya TBA katika ujenzi wa
mabweni kwa ajili ya wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam ambapo
yanatarajiwa kukabidhiwa kwa chuo hicho wiki ijayo.
Mbweni hayo yenye
uwezo wa kuchukua wanafunzi zaidi ya 3,840 yamejengwa na TBA katika kipindi
kisichozidi miezi sita na yamegharimu
takribani shilingi bilioni 10.
Naye Mtendaji Mkuu wa
TBA, Arch. Elius Mwakalinga amemhakikishia Naibu Waziri Eng. Ngonyani kuwa Wakala
huo umejiimarisha kwa kuwa na vifaa vya kisasa na watendaji wenye sifa hivyo
Serikali iendelee kuuamini na kuupa miradi mingi ya ujenzi wa nyumba na ofisi.
“Tunao wahandisi 74,
wachoraji ramani 66, wakadiriaji majenzi 52 na bado tunao wataalam mbalimbali
kutoka kwenye vyuo vikuu nchini wanaowezesha wakala wetu kuwa imara wakati
wote’ amesema Arch. Mwakalinga.
Naibu Waziri Eng.
Ngonyani yuko katika ziara ya siku mbili ya kukagua miradi mbalimbali ya ujenzi
inayosimamiwa na Wakala wa Majengo Nchini (TBA) jijini Dar es Salaam.
Imetolewa na Kitengo
cha Mawasiliano Serikali, Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano
No comments:
Post a Comment