ANGALIA LIVE NEWS

Monday, March 27, 2017

MAFUNZO JUU YA MWONGOZO WA USIMAMIZI WA UWEKEZAJI WA UMMA

Dkt. Lorah Madete, Kaimu Naibu Katibu Mtendaji, Klasta ya Uchumi Jumla, Tume ya Mipango (aliyesimama), akitoa neno kwa washiriki wa mafunzo kabla ya kumkaribisha mgeni rasmi ili afungue mafunzo hayo ya siku tano. Waliokaa ni Bw. Maduka Paul Kessy, Kaimu Katibu Mtendaji, Tume ya Mipango (katikati) na Bw. John Mduma, Mhadhiri Mwanamizi, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.
Mgeni Rasmi Bw. Maduka Paul Kessy, Kaimu Katibu Mtendaji, Tume ya Mipango (aliyesimama) akitoa hotuba ya ufunguzi wa mafunzo kuhusu Mwongozo wa Usimamizi wa Uwekezaji wa Umma kwa washiriki kutoka Idara za Sera na Mipango za Wizara, Idara zinazojitegemea na Wakala za Serikali. Wengine ni Bi. Lorah Madete, Kaimu Naibu Katibu Mtendaji, Klasta ya Uchumi Jumla, Tume ya Mipango (kulia) na Bw. John Mduma, Mhadhiri Mwandamizi, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (kushoto). 

Na Thomas Nyindo.

Maofisa wa Idara za Sera na Mipango kutoka Wizara, Idara na Wakala za Serikali wametakiwa kuongeza ufanisi na ubunifu katika kuandaa na kusimamia miradi ya maendeleo ili kuharakisha malengo ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2025.

Kauli hiyo imetolewa leo na Kaimu Katibu Mtendaji wa Tume ya Mipango, Bw. Maduka Kessy wakati akifungua mafunzo ya Mwongozo wa Usimamizi wa Uwekezaji wa Umma yanayoendelea katika ukumbi wa Chuo cha Mipango Dodoma.

Kessy alieleza kuwa mafunzo hayo yanalenga kuwajengea uwezo maofisa wanaosimamia masuala ya Sera na Mipango katika kuibua na kutekeleza miradi ya maendeleo, hususan, ile inayogharamiwa kwa fedha za Serikali ili kufanya Tanzania kuingia kwenye nchi za kipato cha kati kama ilivyoaninishwa kwenye Dira ya Taifa ya Maendeleo.

“Mipango ya maendeleo tunayojiwekea, kama taifa, inapaswa kutafsiriwa katika miradi na programu za utekelezaji, hivyo mafunzo haya yatatusaidia kuongeza ufanisi, ubunifu na uwajibikaji katika kuandaa miradi na kusimamia miradi yenye tija kwa wananchi,” alisema Kessy.

Aliwasisitiza washiriki wa mafunzo hayo kuwa wao ni miongoni mwa wadau muhimu katika kuifanya Tanzania ipige hatua za maendeleo kwa kuwa ndio wanaohusika katika kupanga na kusimamia utekelezaji wa miradi ya maendeleo.

Aidha, Kessy alieleza kuwa mafunzo hayo yatawasaidia washiriki kuongeza ufanisi na ubunifu katika kuchagua miradi, kutafuta fedha za ugharamiaji na kuboresha uratibu wa kufungamanisha uwekezaji wa umma kwa kubainisha hatua za kufuata katika kujumuisha miradi ya maendeleo katika bajeti za maendeleo.

“Mwongozo huu utawasaidia kufanya maamuzi katika kuchagua miradi sahihi ya uwekezaji katika sekta ya umma na kuhakikisha ufanisi katika utekelezaji wake. Sote tunafahamu kuwa azma yetu ya maendeleo kitaifa ni kufikia uchumi wa kipato cha kati ifikapo 2025,” alisema. Kaimu Katibu Mtendaji huyo alieleza kuwa zipo changamoto zinazokabili usimamizi wa miradi ya maendeleo, kuanzia hatua ya kubuni, kutekeleza hadi kukamilisha miradi hiyo. Kwa hiyo Mwongozo wa Usimamizi wa Uwekezaji waRasilimali za Umma ni mojawapo ya maandiko muhimu ambayo yamebuniwa kukabiliana na changamoto hizo.
Washiriki wa Mafunzo wakimsikiliza kwa makini Mgeni Rasmi (hayupo pichani) wakati wa ufunguzi wa mafunzo hayo.
Washiriki wa Mafunzo wakimsikiliza kwa makini Mgeni Rasmi (hayupo pichani) wakati wa ufunguzi wa mafunzo hayo.
Dkt. John Mduma, Mhadhiri Mwandamizi, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (aliyesimama), akitoa neno kwa washiriki wa mafunzo mara baada ya mafunzo hayo kufunguliwa rasmi.
Washiriki wa mafunzo kuhusu Mwongozo wa Usimamizi wa Uwekezaji wa Umma kutoka Idara za Sera na Mipango za Wizara, Idara zinazojitegemea na Wakala za Serikali pamoja na wawezeshaji wa mafunzo wakiwa katika picha ya pamoja na Mgeni Rasmi mara baada ya ufunguzi wa mafunzo hayo.

No comments: