ANGALIA LIVE NEWS

Tuesday, March 28, 2017

Manji aondoa maombi Mahakama Kuu, sasa aachiwa kwa dhamana



Mfanyabiashara, Yusuf Manji
By James Magai, Mwananchi jmagai@mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Idara ya Uhamiaji imemwachia kwa dhamana mfanyabiashara, Yusuf Manji ikiwa ni siku chache baada ya kufungua maombi Mahakama Kuu akiomba amri ya kutaka idara hiyo iitwe mahakamani kueleza uhalali wa kumshikilia.

Jana, mawakili wake, Alex Mgongolwa, Hudson Ndusyepo na Jeremiah Mtobyesa walidai mahakamani kuwa Manji alikuwa akishikiliwa.

Hata hivyo, baada ya kupatiwa dhamana, Manji aliomba kuondoa maombi hayo aliyofungua dhidi ya Kamishna Mkuu wa Uhamiaji, Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), Ofisa Uhamiaji Mkoa wa Dar es Salaam na Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu.

Jaji Ama-Isario Munisi aliyekuwa akisikiliza maombi hayo aliamuru kuondolewa mahakamani maombi hayo baada ya Wakili wa Serikali Mkuu, ambaye pia ni Naibu Mkurugenzi wa Mashtaka, Oswald Tibabyekoma kueleza kuwa hakuwa na pingamizi dhidi ya maombi hayo.

Nje ya Mahakama, Mgongolwa alilieleza gazeti hili kuwa, Machi 21 mteja wake alimpigia simu akimweleza alipigiwa simu na ofisa uhamiaji akimtaka kufika ofisini kwake kwa ajili ya utaratibu wa dhamana.

Alisema alikwenda naye ofisi za uhamiaji Machi 22 na alipewa dhamana na kutakiwa kuripoti ofisini hapo Jumatatu.

Kabla ya kufungua maombi hayo, Manji ambaye pia ni Diwani wa Mbagala (CCM), alikuwa amelazwa katika Hospitali ya Aga Khan akiwa chini ya ulinzi wa maofisa wa uhamiaji.

Machi 20 wakati maombi hayo yalipotajwa na Mwanasheria Mkuu wa Serikali kuwasilisha hati ya kiapo kinzani, alikana kumshikilia mfanyabiashara huyo.

Hata hivyo, mawakili wake walisisitiza kuwa mteja wao alikuwa chini ya ulinzi wa maofisa wa uhamiaji na polisi waliokuwa wakimlinda akiwa hospitalini usiku na mchana.

Mawakili hao waliomba kuwasilisha mahakamani ushahidi wa viapo vya maofisa wa Hospitali ya Aga Khan kuhusu madai ya mteja wao.

Manji alipelekwa ofisi za uhamiaji mkoa Februari 20 na kuhojiwa kwa tuhuma za kuingia nchini kinyume na sheria, akidaiwa siyo raia wa Tanzania.

Manji alikwenda kuhojiwa akitokea hospitalini, baada ya kutoa maelezo alirejea hospitali.

No comments: