ANGALIA LIVE NEWS

Friday, March 31, 2017

SERIKALI YAIPONGEZA BoT KWA KUELIMISHA WAANDISHI WA HABARI


 Mkurugenzi wa Idara ya Habari MAELEZO, ambaye pia ni Msemaji Mkuu wa Serikali, Dkt. Hassan  Abbasi, (wapili kulia), akipeana mikono na Kaimu Meneja wa Uendeshaji wa BoT, tawi la Zanzibar, Bi.Graceana Bemeye, muda mfuoi baada ya kufungwa kwa semina ya mafunzo wka waandishi wa habari za Uchumi na Fedha, kwenye ukumbi wa BoT, tawi la Zanzibar mjini Unguja, leo Machi 31, 2017. Wakwanza kushoto ni Kaimu Meneja Uhusiano wa Umma na Itifaki wa BoT, Bi. Vicky Msina.
Dak. Hassan Abbasi akizungumza wakati akiwasilisha mada juu ya Sheria mpya ya Huduma za vyombo vya Habari wakati wa kufunga semina ya mafunzo kwa waandishi wa habari za Uchumi na Fedha mjini Zanzibar
Kaimu Meneja wa Uendeshaji wa Bot, tawi la Zanzibar, Bi.Graceana Bemeye, (aliyesimama), akitoa hotuba ya kufunga semina hiyo. Kulia ni Bi. Vicky Msina
NA K-VIS BLOG/Khalfan Said
MKURUGENZI wa Idara ya Habari MAELEZO, ambaye pia ndiye Msemaji Mkuu wa Serikali, Dkt. Hassan Abbasi, (pichani juu), ameipongeza Benki Kuu ya Tanzania, (BoT), kwa kuandaa semina ya mafunzo kwa waandishi wa habari za Uchumi na Fedha, iliyomalizika mjini Unguja, Zanzibar leo Machi 31, 2017.
Dkt. Abaasi alisema, BoT, kama taasisi ya serikali inao wajibu wa kuwapatia habari wananchi kupitia waandishi wa habari na uamuzi wa kutoa mafunzo hayo ni ishara tosha ya ushirikishaji wa waandishi katika kuhakikisha wananchi wanapatiwa habari sahihi kutoka BoT.
"Tumekutana hapa wakati serikali imepitisha sheria mbili, moja ni ile inayohusu huduma za vyombo vya habari, na ya pili ni ile ya haki ya waandishi kupata taarifa kutoka taasisi za serikali na mimi nikiwa kama msimamizi mkuu katika eneo hili la utoaji habari kwenye taasisi za umma, ninawaalika mtusumbue sana katika kupata taarifa maana utoaji wa habari kwa sasa si suala la utashi tena bali ni  la kisheria." Alisema Dkt. Abbassi.
Dkt. Abbasi pia aligusia wajibu wa waandishi wa habari katika kutekeleza majukumu yao chini ya sheria ya sasa,

“Lengo la sheria hii ni kuwajengea heshima Waandishi wa habari ili waweze kufanya shughuli zao katika mazingira ya heshima na bora, tofauti na hivi sasa ambapo taaluma ya uandishi wa habari imekuwa ikilalamikiwa kwa kuchafuliwa na baadhi ya waandishi ambao kimsingi hawana sifa za kuwa waandishi wa habari.” alisema na kuongeza,
“kila taaluma, iwe taaluma ya Sheria, iwe taaluma ya udaktari, lazima wote walio kwenye taaluma hizo wanasimamiwa na kanuni na sheria, kwa hivyo sheria hii itatenganisha kati ya waandishi wana taaluma na wale ambao si wana taaluma.” Alisema.
Dkt. Abbasi pia amekanusha habari kuwa Serikali kupitia sheria hii inataka kuwazuia baadhi ya watu wasifanye kazi za uandishi kwa kigezo cha kitaaluma.
“Hii si kweli, hata Yule anayeitwa Kanjanja, anaweza kufanya kazi ya uandishi lakini kwa kuzingatia kanuni mpya zinazoangazia sheria hii mpya, hivyo hata wale ambao si wanataaluma na wanafanya kazi za kiuandishi wanayo fursa ya kufikia vigezo vya kuitwa waandishi wa habari kwa mujibu wa kanuni hizo ambazo tayari zimeanza kufanya kazi.” Alifafanua.
Aidha Dkt. Abbasi amesema, Sheria hii ya sasa inatoa fursa kwa chombo cha habari kuomba radhi na kuchapisha habari ambazo zina makosa kwa nia ya kuzisahihisha, na swala hilo likakubaliwa kisheria na halitapelekwa mahakamani chini ya kifungu cha 40 cha sheria ya Huduma za vyombo vya habari.
Akifunga maunzo hayo, Kaimu Meneja Uendeshaji wa BoT tawi la Zanzibar, Bi. Graceana Bemeye aliwashukuru waandishi hao kwa ushiriki wao uliotukuka. "Niwahakikishie kuwa BoT, inatambua umuhimu wa waandishi wa habari katika shughuli zake za kila siku, hivyo tutaendelea kutoa mafunzo haya ili kujenga uwezo wa waandishi kuandika kwa usahihi habari zinazohusu BoT kwa manufaa ya taifa.Aidha Kaimu Meneja Uhsuiano wa Umma na Itifaki wa BoT, Bi. Vicky Msina, alisema mafunzo yaliyotolewa na BoT kwa waandishi hao wa habari ni moja ya majukumu ya BoT katika kuelimisha umma na kwamba mafunzo hayo yalijumuisha waandishi wa habari kutoka vyombo vya habari vya Bara na Zanzibar, vikiwemo vile vya kielektroniki, magazeti na Mitandao ya Kijamii. "Lengo ni kuhakikisha tunawajengea uwezo waandishi wa habari za Uchumi na Fedha ili waweze kuripoti kwa usahihi habari za BoT. "Lakini pia BoT, kupitia website yake imeanza kutafsiri baadhi ya taarifa zake kwa lugha ya Kiswahili ili kutoa wigo mpana kwa wananchi kuzielewa taarifa za BoT." Alisema. Akizungumza kwa niaba ya washiriki wa semina hiyo, Bw. Ezekiel Kamwaga, aliishukuru BoT kwa kuandaa semina hiyo na kuhimiza ushirikiano zaidi katika utoaji wa habari zinazohusu taasisi hiyo nyeti hapa nchini.
 Kaimu Meneja Uhsuiano wa Umma na Itifaki wa BoT, Bi. Vicky Msina
 Mwenyekiti wa Semina, Bw. Ezekiel Kamwaga, akizungumza
 Afisa Uhusiano Mkuu kutoka Idara ya Uhusiano wa Umma na Itifaki wa BoT, Bw. Lwaga Mwambande
 Baadhi ya wanasemina wakisikiliza hotuba
 Maafisa wa BoT, Bw.Lusajo Mwankemwa, (kushoto), na Bi.Flora Mkemwa
Mkurugenzi wa Idara ya Habari Maelezo na Msemaji Mkuu wa Serikali, Dkt. Hassan Abbasi, (Kushoto), akipeana mikono na Mmiliki wa K-VIS Blog, Bw. Khalfan Said mwishoni mwa semina hiyo
Dkt. Abbasi akitoa semina


Dkt. Abbasi (kushoto), akimsikiliza Mchumi Mwandamizi kutoka Kurugenzi ya Utafiti na Sera za Uchumi, BoT, Bw.Lusajo Mwankemwa, wakati wa ufungaji wa semina hiyo


Mwandishi wa habari wa Sauti ya Ujerumani, (DW),  mwenye makazi yake Zanzibar, Bi. Salma Said, akizungumza

Bi. Vicky Msina, (kushoto) na Bw. Lusajo Mwankemwa
Picha ya pamoja





No comments: