Advertisements

Wednesday, March 29, 2017

TEMESA YAKABIDHIWA BOTI NNE ZA KISASA BAADA YA UJENZI WAKE KUKAMILIKA

 Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Ufundi na Umeme (TEMESA) Dkt. Mussa Iddi Mgwatu (kushoto) akiteta jambo na Mkurugenzi wa Ukodishaji na Huduma za Vivuko TEMESA Mhandisi Japhet Maselle, nyuma yao ni Meneja wa TEMESA mkoani Mwanza Mhandisi Ferdnand Mishamo wakati wa majaribio ya boti Mpya ya MV Mkongo  iliyojengwa kwa ajili ya kutumika katika eneo la Utete Rufiji Mkoani Pwani. Boti hiyo ina uwezo wa kubeba abiria 40.
 Boti tatu kati ya nne mpya zilizokabidhiwa leo kwa Wakala wa Ufundi na Umeme (TEMESA) na Kampuni ya Songoro Marine Boatyard baada ya kukamilika kwa ujenzi wake. Makabidhiano yamefanyikia jijini Mwanza na boti hizo zitasafirishwa kuelekea Pangani Tanga, Kilambo Mtwara na Msangamkuu Mtwara ili zianze kutoa huduma kwa wananchi.
 Boti Mpya ya MV Kuchele iliyokabidhiwa leo kwa Wakala wa Ufundi na Umeme (TEMESA) na Kampuni ya Songoro Marine Boatyard baada ya kukamilika kwa ujenzi wake. Boti hii iliyojengwa kwa “fibre glass” ina uwezo wa kubeba abiria nane na itakuwa ikitumika nyakati za dharura katika eneo la Msangamkuu Mtwara. Makabidhiano hayo yamefanyika leo jijini Mwanza.
 Boti Mpya ya MV Tangazo  iliyokabidhiwa leo kwa Wakala wa Ufundi na Umeme (TEMESA) na Kampuni ya Songoro Marine Boatyard baada ya kukamilika kwa ujenzi wake. Boti hii iliyojengwa kwa “fibre glass”ina uwezo wa kubeba abiria 25 na itakuwa ikitumika nyakati za dharura katika eneo la Kilambo Mtwara. Makabidhiano hayo yamefanyika leo jijini Mwanza.
Boti Mpya ya MV Bweni iliyokabidhiwa kwa Wakala wa Ufundi na Umeme (TEMESA) na Kampuni ya Songoro Marine Boatyard baada ya kukamilika kwa ujenzi wake. Boti hii iliyojengwa kwa “fibre glass”ina uwezo wa kubeba abiria nane na itakuwa ikitumika nyakati za dharura katika eneo la Kilambo Mtwara. Makabidhiano hayo yamefanyika leo jijini Mwanza. Picha na Theresia Mwami – TEMESA Mwanza

Na Theresia Mwami – TEMESA Mwanza
Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Ufundi na Umeme (TEMESA), Dkt. Mussa Iddi Mgwatu, leo amepokea boti nne zilizokuwa zikijengwa na kampuni ya Songoro Marine Boatyard ya jijini Mwanza. Dkt. Mgwatu amesema kukamilika kwa boti hizi ni utekelezaji wa ahadi za Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Mhe. Prof. Makame Mbarawa alizozitoa kwa wananchi wa Pangani Tanga pamoja na Kilambo na Msangamkuu Mtwara kwa nyakati tofauti.
Dkt. Mgwatu ameongeza kuwa boti hizo nne zitatoa huduma za dharura hasa wakati wa usiku kwa ajili ya kuhudumia wagonjwa na pia kutoa usafiri mbadala wakati vivuko vikubwa vinapokuwa haviwezi kutoa huduma kutokana na changamoto mbalimbali ikiwemo kupungua kwa kina cha maji katika maeneo ya Kilambo mkoani Mtwara pamoja na Utete Mkoani Pwani.
Nae Mkurugenzi kutoka kampuni ya Songoro Marine Boatyard Mhandisi Major Songoro amesema kuwa boti tatu kati ya nne zilizokabidhidhiwa zimejengwa kwa kutumia “fibre Glass” na boti moja imejengwa kwa kutumia chuma. Boti ya MV Kuchele ambayo itapelekwa katika eneo la Msangamkuu Mtwara ina uwezo wa kubeba abiria nane, sawa na boti ya MV Bweni itakayopelekwa katika eneo la Pangani mkoani Tanga. MV Mkongo itakayopelekwa Utete mkoani Pwani ina uwezo wa kubeba abiria 40 na MV. Tangazo itakayopelekwa Kilambo/Namoto Mtwara ina uwezo wa kubeba abiria 25.
Aidha Dkt. Mgwatu ameishukuru Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kupitia Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano kwa kuwezesha ujenzi wa boti hizo na tayari amemuagiza mkandarasi huyo kuhakikisha anazisafirisha boti hizo kwenye maeneo husika haraka iwezekanavyo ili wanachi waanze kunufaika na huduma mbadala itakayotolewa na boti hizo. Ujenzi wa boti hizo umefanywa kwa kutumia fedha za ndani na umegharimu jumla ya shilingi milioni 415.

No comments: