ANGALIA LIVE NEWS

Friday, March 31, 2017

‘Tunao uwezo kuchambua mchanga wa dhahabu’

Mtendaji Mkuu wa GST, Profesa Abdulkarim Mruma
MTENDAJI Mkuu wa Wakala wa Jiolojia Tanzania (GST), Profesa Abdulkarim Mruma amesema kazi ya kuchunguza na kubaini kiwango cha madini kilichomo kwenye ‘mchanga wa dhahabu’ itakuwa ni rahisi kutokana na maabara yake kuwa na vifaa vya kisasa.

Akizungumza na gazeti hili Profesa Mruma alisema kwamba maabara ya GST ni miongoni mwa maabara bora kabisa barani Afrika.

“Ukiacha Afrika Kusini na nchi za Kiarabu, sisi tunaongoza katika nchi za kusini mwa Afrika kuwa na maabara ya jiolojia ya kisasa zaidi,” alisema Profesa Mruma ambaye taasisi yake ambayo iko chini ya Wizara ya Nishati na Madini, makao makuu yake ni Dodoma.

Alifafanua kuwa nchi zingine kama Malawi, Kenya na zinginezo huwa zinaleta sampuli zake kwenye maabara hiyo, jambo ambalo linaifanya iwe miongoni mwa maabara bora.

Aidha, alisema kazi hiyo aliyopewa na Rais ya kuwa mmoja wa wajumbe wanaounda kamati ya kuchunguza kilichomo kwenye mchanga huo, itafanyika kwa uadilifu mkubwa.

“Hii kazi ambayo tumepewa na Rais itakuwa ni rahisi, hii ni kutokana na aina ya maabara tuliyo nayo pamoja na wataalamu waliopo,” alisema Profesa Mruma ambaye juzi aliteuliwa na Rais John Magufuli kuwa miongoni mwa wajumbe wa kuchanguza kilichomo kwenye mchanga huo wa madini.

Profesa Mruma anaunda kamati hiyo pamoja na wajumbe wengine saba ambao ni Profesa Justianian Ikangula, Profesa Joseph Bushweshaiga, Dk Yusuf Ngenya, Dk Joseph Philip, Dk Ambrose Itika, Mohamed Makongoro na Hery Gombela.

Profesa Mruma alisema hawatatumia maabara inayotumiwa na Wakala wa Madini (TMAA) kwenye uchunguzi wao.

Alisema anajiamini kwa kuwa vifaa vilivyoko kwenye maabara hivyo vimenunuliwa miaka miwili iliyopita chini ya fedha walizopatiwa na Benki ya Dunia.

Aliwahakikishia Watanzania kuwa licha ya kuwepo vifaa vya kisasa, maabara ya GST pia ina wataalamu waliobobea kwenye uchunguzi wa masuala ya madini ya miamba jambo ambalo litafanya kazi yao iwe rahisi zaidi.

Alisema kwa kuwa ni suala la uchunguzi, hawawezi kukomea kwenye maabara ya GST peke yake, lazima waangalie pia na maabara zingine zikiwemo za nje ya nchi kwa lengo la kujiridhisha zaidi.

Alisema kwenye uchunguzi wowote ili kupata matokeo sahihi ni lazima ulinganisho ufanyike kati ya maabara moja na nyingine.

“Naamini kuna sampuli ambazo lazima tutalazimika kuzipeleka nje ya nchi ili kuona kama matokeo ya vipimo yanaoana,” alieleza Profesa Mruma.

Rais Magufuli ameunda kamati hiyo inayohusisha wataalamu mbalimbali na leo wataenda Ikulu kwa ajili ya kukabidhiwa majukumu yao rasmi.

Kabla ya kamati hiyo kuundwa, Jumatatu wiki hii, Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa alitembelea mgodi wa Buzwagi na kuchukua sampuli kwenye makontena ambako alisema serikali itaenda kuzipima tena sampuli hiyo ili kujiridhisha kilichomo ndani ya mchanga huo.

TMAA pamoja na Wizara ya Nishati na Madini ilishatoa ufafanuzi kuwa kilichomo kwenye mchanga huo ni madini ya shaba kwa asilimia 90, fedha asilimia 0.08. na dhahabu ambayo kiwango chake ni asilimia 0.02.

Kutokana na utata huo, Mamlaka ya Usimamzi wa Bandari (TPA) imezuia usafirishaji wa makontena zaidi ya 260 ambayo yalikuwa yanapelekwa nje ya nchi.

TPA imechukua uamuzi huo kwa kutii agizo la Rais Magufuli linaloitaka wizara ya nishati kuzuia usafirishaji wa mchanga.

TPA inaamini kilichomo kwenye mchanga huo, asilimia 90 ni dhahabu na ndio maana wawekezaji wanasafirisha kontena hizo kwenda nje kwa ajili ya kuchenjua dhahabu hiyo.

Kwa mujibu wa TMAA, kwa mwaka makontena takribani 50,000 yenye mchanga wa dhahabu yanasafirishwa nje ya nchi.

Biashara hiyo ilianza mwaka 1998 na mchanga huo unasafirishwa kutokana na Tanzania kutokuwa na kinu cha kuchenjua mchanga huo na kutenganisha madini yaliyomo kwenye mchanga huo.

Spika wa Bunge, Job Ndugai ameshatangaza kuwa ataunda kamati maalumu ambayo itachunguza kwa kina biashara hiyo ya mchanga, nani anafaidika na Tanzania inafaidikaje na mchanga huo.

Ndugai alisema wanaunda kamati hiyo na matokeo yake watayatangaza ili wananchi wafahamu kiini cha biashara hiyo.

Mchanga huo ni mali ya migodi ya Buzwagi na Bulyanhulu pamoja na wachimbaji wadogo wa madini ya mentaliki.

Wachimbaji hao wadogo wamejitokeza hadharani hivi karibuni na kudai kuwa makontena 60 ambayo ni miongoni mwa makontena yaliyozuiwa ni mali yao.

HABARI LEO

No comments: