Aidha, tayari majaribio ya mpango huo wa kuwahamishia walimu hao uameanza katika Mkoa wa Arusha na yakifanikiwa, itahusisha mikoa yote nchini hasa kwenye mahitaji.
Naibu Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi) Elimu, Bernard Makali alisema hayo mbele ya Kamati ya Kudumu Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC) wakati kamati hiyo ilipokuwa ikichambua taarifa za Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG).
Kamati ilikuwa inakagua taarifa hiyo kuhusu ufanisi katika Wizara ya Elimu, Sayansi, Teknolojia na Mafunzo ya Ufundi.
Makali alisema katika sekondari walimu wa sanaa (Arts) ni wengi kwa idadi hiyo ya zaidi ya 7,000 na kwamba hao wanaohamishwa wanachochea ubora wa elimu katika shule za msingi na marupurupu yao na mishahara itabaki kama ilivyo.
Kwa mujibu wa Makali, shule za msingi nchini zina upungufu wa jumla wa walimu 47,151 na ziada ya walimu wa sanaa katika shule za sekondari ni hiyo 7,463 na ndio watakaopelekwa shule za msingi.
Naibu Katibu Mkuu alikuwa akijibu hoja ya Mbunge wa Kilindi, Omari Kigua (CCM) alihoji kwa nini walimu wengi wa shule za msingi wanajiendeleza lakini wakirejea kazini, wanabaki kufundisha shule hizo za msingi badala ya kupandishwa wafundishe sekondari.
Akijibu hoja hiyo, Naibu Katibu Mkuu alisema asilimia 90 ya walimu wa shule za msingi wanaokwenda kujiendeleza, wanachagua masomo ya sanaa na walimu wa masomo hayo ni wengi katika shule za sekondari kiasi kwamba wengine wanagawana mada (topic) badala ya vipindi katika ufundishaji.
Makali alitoa mfano wa Shule ya Sekondari ya Makole ya Dodoma ambayo ina mwalimu mmoja wa fizikia ambaye pia ndiye mwalimu mkuu huku ikiwa na walimu wa sanaa wakiwa na ziada.
“Tumeanza na ‘pilot’ (majaribio) mkoani Arusha na tutafanya kwa nchi nzima ili kujiridhisha na kuhakikisha lengo linatimia,” alifafanua Naibu Katibu Mkuu Tamisemi.
Kuhusu upungufu wa walimu wa hisabati na sayansi, alisema wamepata kibali cha kuajiri walimu 4,129 wa masomo ya sayansi na wataalamu wa maabara.
Aidha, baadhi ya wajumbe wa kamati waliuliza kuhusu kuwepo kwa walimu wasio na sifa kazini na kutaka kujua hatua zinachukuliwa na serikali hasa baada ya kuweka utaratibu kwao kwenda kujiendeleza.
HABARI LEO
No comments:
Post a Comment