Advertisements

Monday, March 20, 2017

Wanashera wajadili kuinusuru TLS

WANACHAMA wa Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS) jana walikuwa katika mjadala mkali wakati baadhi yao wakitaka kuwepo kwa azimio la kumfuta uanachama, Waziri wa Katiba na Sheria, Dk Harrison Mwakyembe, kufuatia tishio la kukifutia usajili chama hicho na wangine wakipinga uamuzi huo.

Katika mchango wake, Waziri wa zamani wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Lawrence Masha, alipendekeza Mkutano huo ufikie azimio la kumfuta uanachama Dk Mwakyembe.

“Tumfukuze Mwakyembe TLS, haiwezekeni atoe pendekezo la kukifutia usajili wakati mwenyewe ni mwanachama, hii inamaanisha nini,” alisisitiza.

Profesa Josephat Kanywanyi, alisema Dk Mwakyembe ambaye ni mwanachama wa wahadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Waziri na mwanachama wa TLS, amejikuta katika wakati mgumu kutoa tishio kama hilo kwa kuwa anatoa maamuzi ya Serikali na si yake binafsi, hivyo hawapaswi kumhukumu.

Alisema inawezekana tishio hilo likawa limetoka upande wa Serikali na yeye Mwakyembe ndiye Waziri alipaswa kulitamka.

Aliwataka wanachama kujenga hoja za kutetea Chama hicho kisiondolewe usajili wake, badala ya kumshambulia mtu. “Ni jukumu la chama kuhakikisha majukumu yake yanatekelezwa na kuyatetea,” alisema.

Naye Dk Eve Hawa Sinare, aliwataka wanachama wenzake kuelewa suala la Dk Mwakyembe si la msingi kwa sasa isipokuwa, kupigania chama hicho kisifutiwe usajili ndio jambo la msingi. “Hebu tupiganie chama kisifutiwe usajili, tishio hili linaweza kuwa ni uamuzi wa Baraza la Mawaziri, hakuna anayejua hilo,” alisema.

Dk. Rugeremeleza Nshalla, alisihi kuepuka kufanya mapambano na badala yake, waunde kamati itakayofanya mchakato wa kuifanyia marekebisho makubwa TLS.

Jaji Thomas Mihayo, alisema ingawa kuna tishio la kukifutia usajili TLS, lakini hoja ya kumfuta uanachama Dk Mwakyembe si sahihi.

Alisema uamuzi wowote utakaochukuliwa kwa mihemko utakuwa na athari kubwa kwao na kwa wanachama wa baadaye. Dk Erick Ngimaryo, aliunga mkono mawazo ya Dk Sinare ya kukifanyia marekebisho makubwa chama hicho.

Alisema hatua wanayopaswa kuchukua ni kufanya mazungumzo na Serikali na si kupambana nayo.

HABARI LEO

No comments: