ANGALIA LIVE NEWS

Saturday, April 8, 2017

Mdahalo Maalum: Watanzania Wa Nyumbani Na Diaspora Kukutanishwa..


Ni Jumanne na Jumatano, Aprili 11 na 12. Ni mdahalo kuhusu nafasi ya Diaspora kuungana na wenzao walio nyumbani kwenye kuchangia kusukuma mbele jitihada za kuifanya Tanzania kuwa nchi ya uchumi wa viwanda kutokana na maendeleo ya viwanda. Hivyo, umuhimu wa kujadili fursa na changamoto.

Tukio hilo ambalo ni sehemu ya maadhimisho ya Miaka Kumi ya kuanzishwa kwa mtandao wa ' Mjengwablog' litafanyika Aprili 11 na 12 ( Jumanne na Jumatano) kwenye Ukumbi wa Nyumba ya Makumbusho, Dar Es Salaam. Ukumbi upo Mtaa wa Shabaan Robert na utazamana na IFM.

Mdahalo utaambatana na maonyesho ya bidhaa zinazozalishwa Tanzania na wajasiriamali wa Kitanzania. Washiriki wa mdahalo huo wanaotarajiwa kuwa zaidi ya mia mbili wanatazamiwa kuwa katika makundi matatu makuu; Baadhi ya Watanzania waishio ughaibuni, waliokuwa wakiishi ughaibuni na sasa wamerejea nyumbani na Watanzania wa nyumbani. Wote hao wanaunganishwa jambo kuu lenye kuhusu maendeleo ya uchumi wa nchi na kwa ngazi ya mtu binafsi. Hivyo, inahusu kujadili fursa za kufanya biashara na uwekezaji. Mdahalo hauna kiingilio.

Na Alhamisi April 13, kutakuwa na ' Usiku wa Nyumbani Na Diaspora' kwenye ukumbi wa Mzalendo Pub, Kijitonyama. Kutakuwa na chakula cha Kiafrika na maonyesho ya mavazi ya Kiafrika. Baada ya hapo ni mwendo wa kujirusha kwa muziki mchangayiko wa DJ BonyLuv!

No comments: