ANGALIA LIVE NEWS

Friday, April 14, 2017

MILLIONI 278 ZA WANACHAMA WA USHIRIKA WA MATAMBA WILAYANI MAKETE HAZIJULIKANI ZILIPO

Zaidi ya shilingi milioni 278 mali ya wananchi ambao ni wanachama wa chama cha kuweka na kukopa cha Neema SACCOS kilichopo kata ya Matamba wilayani Makete hazijulikani zilipo hali ambayo imewafanya wananchi hao kuiomba serikali kuingilia kati kwa kuwa wanaamini zimeliwa na wajanja wachache.
Katika siku za hivi karibuni hali ya mzunguko wa fedha katika chama cha kuweka na kukopa cha Neema SACCOS kilichopo kata ya matamba wilayani makete imekuwa mbaya kwa wanachama ambao wamewekeza hisa, amana na akiba ya kwenye chama hicho,hali ambayo ikawalazimu kuusimamisha uongozi wa SACCOS hiyo na kuunda kamati ya uchunguzi ambayo baada ya kukamilisha kazi yake imebaini upotevu wa zaidi ya shilingi milioni 278.

Baada ya kupewa taarifa hiyo ambayo imewasilishwa kwa wanachama wa Neema SACCOS chini ya usimamizi wa afisa ushirika wa wilaya ya Makete,alloyce Rajab Mwakityega, wanachama wakaiomba serikali kuwasaidia kuchukua hatua kwa kuwakamata na kuwafikisha polisi viongozi wote waliokuwa madarakani chini ya mwenyekiti wao ambaye pia ni makamu wa askofu wa kanisa la Kiinjili la Kirutheri Tanzania dayosisi ya kusini magharibi, mchungaji ambonwile ngavo.


Akizungumza kwa niaba ya watuhumiwa wenzake, mwenyekiti wa bodi ya neema SACCOS ambaye pia ni makamu wa askofu wa kanisa la KKKT Dayosisi ya Kusini Magharibi, Mchungaji Ambonwile Ngavo amekiri kupotea kwa fedha za wanachama lakini akasema kuna umuhimu wa kuunda kamati kwa ajili ya kuchunguza kila kiongozi kwa lengo la kubaini ukweli kuhusu upotevu wa fedha hizo.

Hata hivyo afisa ushirika wa wilaya ya Makete Alloyce Rajab Mwakityega ameshidwa kuchukua hatua kulingana na matakwa ya wanachama wa SACCOS hiyo ya kuwakamata watuhumiwa na badala yake akadai kuwa atalifikisha suala hilo kwa bosi wake ambaye ndiye mwenye mamlaka ya kuamuru kukamatwa kwa watuhumiwa wanaodaiwa kutafuna fedha hizo.

Chanzo: ITV Tanzania

No comments: