Hakuna bosi yeyote serikalini anayelipwa zaidi ya Sh17 milioni baada ya Serikali ya Awamu ya Tano kuanza kutekeleza sera zake za kubana matumizi, lakini yupo kiumbe hai mmoja tu ambaye matumizi yake yalifika Sh64 milioni kwa mwezi; na kuna sababu za kuhalalisha gharama hizo.
Kiumbe huyo ni mnyama mwitu aina ya faru aliyepewa jina la Fausta, ambaye sasa anatumia Sh20.4 milioni.
Fausta ndiye faru kikongwe kuliko wote nchini, akiwa na umri wa miaka 54, na anahitaji matunzo mazuri ili aendelee kuvuta watalii na wanasayansi kutoka kila pembe ya dunia.
Fausta anaishi Hifadhi ya Ngorongoro ambako analindwa kwa saa 24 kumuepusha kushambuliwa na wanyama wengine kama fisi na mbwa mwitu kutokana na uzee, lakini gharama za ulinzi zitapungua baada ya kupata makazi salama ndani ya mwitu jengo lake litakapomalizika.
Hiyo ni sehemu tu ya gharama zinazomfanya Fausta kutumia fedha nyingi zaidi ya mfanyakazi mwandamizi wa serikalini.
Kazi ipo kwenye malisho
Imeelezwa kuwa sababu zinazofanya matunzo ya Faru Fausta kutumia jumla ya Sh768 milioni kila mwaka ni pamoja na ulinzi, chakula chake kuagizwa kutoka nje na miwa anayotakiwa kula.
Sakata la Faru huyo kutumia kiasi hicho cha fedha liliibuliwa juzi na Mbunge wa Babati Mjini (Chadema), Pauline Gekul alipoelezea gharama hizo na Serikali kuthibitisha.
Meneja wa maendeleo ya tafiti na Ikolojia wa Hifadhi ya Ngorongoro, Asantaeli Merita alisema jana kuwa matunzo yake yalianza kugharimu fedha nyingi baada ya kuanza kutunzwa katika eneo maalumu.
Alisema katika eneo hilo ilibidi kujengwa banda lake la kuishi na uzio wa chuma ambao si rahisi faru huyo kuvunja na kutoka nje. Banda hilo limezungushiwa mbao maalumu.
Merita alisema kutokana na faru huyo kuwa katika eneo hilo, kuna askari 15 maalumu ambao wanamlinda kwa zamu kwa saa 24 na kuna gari ambalo ni la mahitaji mbalimbali, ikiwa ni pamoja na kubeba majani ya lishe kila siku.
Alisema ili kudhibiti maradhi ambayo faru huyo amekuwa akiugua, Hifadhi ya Ngorongoro imekuwa ikigharamia chakula cha virutubisho aina ya luseni ambacho kinapatikana nchini Kenya na amekuwa akipelekewa chakula hicho mara mbili kwa mwezi.
Alisema luseni anayotumia Fausta ni tofauti na luseni ya ng’ombe wa maziwa ambayo inapatikana hapa nchini.
Alisema faru huyo ‘kikongwe’ pia amekuwa akipewa miwa ambayo inapatikana eneo la Dareda mkoani Manyara. Miwa hiyo humsaidia kuboresha afya yake na imekuwa ikipelekwa mara mbili kwa mwezi.
Merita alisema kuna dawa zake ambazo anapaswa kuzitumia kila baada ya wiki mbili.
“Hiyo gharama ya milioni 64 ni ya mwanzo tu baada ya kuanza kuhifadhiwa, lakini baada ya kupatikana eneo la kumuhifadhi na kujengwa itapungua sana,” alisema.
Alisema baada ya kukamilika ujenzi wa banda maalumu la kumuhifadhi kwa sasa wastani wa gharama kwa mwezi zitakuwa Sh20.8 milioni.
Merita alisema kwa maendeleo ya hifadhi ni muhimu kwa Fausta kuendelea kupatiwa matunzo maalumu kwa kuwa licha ya kuingiza fedha nyingi za kigeni, pia amekuwa akitumika katika tafiti za wataalumu wa hifadhi za asili.
Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro imekuwa ikiingiza zaidi ya Sh70 bilioni kwa mwaka kutokana na watalii ambao wanafika kutembelea eneo hilo. Karibu nusu ya watalii wanaokuja nchini, hutembelea Hifadhi ya Ngorongoro.
Katika kipindi cha maswali na majibu bungeni, Gekuji alihoji mpango wa Serikali kwa faru huyo kutokana na gharama kubwa za kumtunza.
“Hifadhi ya Ngorongoro inatumia gharama kubwa, ikiwa ni pamoja na kumtunza na kumlisha Faru Fausta. Kiasi cha Sh64 milioni kinatumika kwa mwezi. Je, Serikali ina mpango gani na huyu Faru Fausta,” alihoji Gekul.
Akijibu swali hilo, Waziri wa Maliasili na Utalii, Profesa Jumanne Maghembe alisema ni kweli mnyama huyo anatunzwa kwa gharama kubwa kwa sababu ni mzee na ananyemelewa na magonjwa mbalimbali.
Waziri alisema wanafanya hivyo kutokana na ukweli kuwa wanyama wa aina hiyo ni wachache katika hifadhi, akasema utafiti unafanyika ili gharama za kumtunza ziwe ndogo kulingana na thamani inayopatikana. Kiwango hicho cha fedha kilisababisha Mbunge wa Tunduma (Chadema), Frank Mwakajoka kuomba mwongozo wa Spika.
”Majibu ya waziri anasema Faru Fausta yupo na anatunzwa kwa Sh64 milioni kwa mwezi. Tafsiri yake ni kwamba anatunzwa kwa Sh768 milioni kwa mwaka. Anatoa sifa eti kwa sababu ni mzee sana, naomba mwongozo wako kuhusu hili kwa sababu mnyama huyu hawezi kuingiza faida yoyote,” alisema Mwakajoka.
Akitoa mwongozo wake Spika Job Ndugai alisema suala hilo anaiachia wizara.
Chanzo: Mwananchi
No comments:
Post a Comment