Msichana mmoja (jina linahifadhiwa) mwenye umri wa mika 16 na mwanafunzi wa kidato cha 3 huko Zanzibar, juzi alijitosa baharini katika eneo la Chumbe kutoka katika boti ya Azam Marine Kilimanjaro V.
Msichana huyo aliyekuwa akisafiri na mjomba wake kutoka Dar es salaam kwenda Unguja alijirusha baharini majira ya saa 5 na kuokolewa na mabaharia wa boti hiyo ndani ya muda mchache.
Wanafamilia wa binti huyo waishio eneo la Kikwajuni Unguja walieleza kuwa kabla ya kutoroka kwa binti huyo, walimkuta na simu ambayo hawakufahamu alikoipata. Kutokana na utaratibu wa familia hiyo ya kutoruhusu simu kwa watoto, walimnyang’anya simu hiyo na kumtaka aeleze alikoitoa vinginevyo watampeleka Polisi. Binti huyo alikasirishwa na kitendo hicho ndipo alipofanya uamuzi wa kutoroka.
Mama mdogo wa binti huyo alieleza kuwa walimtafuta binti huyo bila mafanikio ndipo walipoamua kuipekua simu aliyokuwa akiitumia na kukuta namba ya kijana mmoja iliyokuwa imetumiwa mara nyingi. Walipowasiliana na kijana huyo kumuuliza anafahamiana vipi na yule binti, alijibu kuwa walijuana kupitia mtandao wa ‘facebook’ lakini hawajawahi kukutana kwa kuwa binti anaishi Zanzibar na kijana anaishi Dar es Salaam.
Alisema walimpa taarifa kijana huuyo kuwa binti yao ametoroka na hajulikani alikokwenda, hivyo kumwomba kusaidiana kuhakikisha wanampata akiwa salama.
“Kwa kweli kijana huyo alikubali kutoa ushirikiano na akawa anawasiliana na binti yetu na kumuleza kuwa yuko Dar es Salaam na amehifadhiwa na dereva teksi baada ya kukosa msaada wa eneo analotaka kwenda ambako ni kwa bibi yake anayeishi Mburahati, Dar es Salaam” alisema
Alisema aliwasiliana na dereva huyo aliyemuhifadhi binti yao na kuambiwa kwamba amesharipoti katika serikali ya mtaa anoishi kuwa amemuokota binti huyo bandarini , Dar es salaam baada ya kukaa kwa muda mrefu bila ya kupata msaada.
Mama mdogo ambaye ndiye aliyemlea binti huyo tangu akiwa mdogo alieleza kwamba mama mzazi wa binti huyo anaishi Muscat, Oman, na alipatwa na mshtuko mkubwa baada ya kupata taarifa kuwa binti yake amejitupa baharini wakati akitokea Dar es Salaam baada ya kusakwa kwa siku kadhaa na hatimaye kupatikana.
Naye mjomba wa binti huyo ambaye ndiye aliyekwenda Dar es Salaam kumchukua, alieleza kuwa wakiwa ndani ya boti binti alilalamika kuwa anajisikia vibaya, hivyo anahitaji kwenda kukaa kwenye veranda ya boti ili apunge upepo. Wakatoka kwenda kwenye veranda nje ya boti hiyo.
Wakiwa wamekaa binti huyo alimtaka mjomba wake kumpatia kitambaa cha kufunika uso ‘nikabu’ na baibui avae ili kuepuka usumbufu wakati wa kushuka kwani muda wa kufika Zanzibar ulikuwa umekaribia.
Mjomba alipogeuka upande wa pili ili kuvichukua vitu hivyo katika begi, ndipo ghafla msichana huyo alijitosa ndani ya bahari.
“Nilipiga yowe baada ya kuangalia na kumwona. Tulishirikiana na mabaharia wa boti hiyo ili kumwokoa na ndani ya muda mchahe tulifanikiwa” alisema
Wanafamilia wa binti huyo walisema binti huyo alikuwa na tabia nzuri tokea alipokuwa mdogo, na mara nyingi alipendelea kukaa ndani. “Hatujui kwa nini amliamua kufanya uamuzi huo”
Aidha daktari Suleiman Abdul, Mratibu wa huduma za afya Hospitali ya Kidongo Chekundu alikotibiwa msichana huyo, alisema wanaendelea na uchunguzi wa afya ya akili ya msichana huyo na kuwataka wanafamilia yake kutokuzungumzia chochote kuhusu tukio hilo na waendelee kushirikiana nae vizuri ili kuona maendeleo ya afya yake.
No comments:
Post a Comment