JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA
WIZARA YA MAMBO YA NJE NA USHIRIKIANO WA AFRIKA MASHARIKI
TTT
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Watanzania waliokuwa wanashikiliwa nchini Malawi waachiwa huru
Mahakama Kuu ya Mzuzu nchini Malawi jana tarehe 12 Aprili 2017 iliwaachia huru Watanzania wanane waliokuwa wanashikiliwa nchini humo kwa kosa la kuingia kinyume cha sheria kwenye mgodi wa urani wa Kayerekera.
Hakimu Mkazi Mkuu wa Mahakama ya Mzuzu, Bw. Texious Masoamphambe alitoa hukumu ya kifungo cha mwezi mmoja kwa kosa la kuingia kinyume cha sheria kwenye mgodi wa urani wa Kayerekera (trespass) na kifungo cha miezi mitatu kwa kosa la kufanya ujasusi (reconnaissance).
Makosa hayo mawili, kifungo chake kinakwenda pamoja na kwa mujibu wa Hakimu huyo watuhumiwa tayari wameshatumikia kifungo hicho na kuamuru waachiliwe huru. Aidha, Hakimu aliamuru Wizara ya Mambo ya Ndani na Usalama wa Ndani kuhakikisha kuwa Watanzania hao wanasafirishwa na kurejeshwa makwao haraka iwezekanavyo.
Kwa mujibu wa taarifa kutoka Ubalozi wa Tanzania nchini Malawi, Watanzania hao wamesafirishwa leo tarehe 13 Aprili 2017, kutoka Mzuzu hadi Mpaka wa Songwe/Kasumulu kati ya Tanzania na Malawi.
Watanzania hao ambao ni Walasa Mwasangu, 30, Binto Materinus, 32, Ashura Yasiri, 63, Christian Msoli, 38, Layinali Kumba, 47, Maliyu Mkobe, Gilbert Mahumdi, 32, na Martin Jodomusole, 25 walikuwa wamekamatwa na kushikiliwa na vyombo vya usalama vya Malawi tokea tarehe 20 Desemba 2016.
Imetolewa na:
Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali,
Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki
Dar es Salaam, 13 Aprili 2017.
No comments:
Post a Comment