JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA
WIZARA YA MAMBO YA NJE NA USHIRIKIANO WA AFRIKA MASHARIKI
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
KUHUSU MISHENI YA MAWAZIRI WA MAMBO YA NJE WA SADC TROIKA NCHINI JAMHURI YA KIDEMOKRASIA YA KONGO (DRC)
Mheshimiwa Dkt. Augustine P. Mahiga (Mb), Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki na Mwenyekiti wa SADC wa Kamati ya Mawaziri ya Asasi ya Ushirikiano wa Siasa, Ulinzi na Usalama (SADC Ministerial Committee of the Organ on Politics, Defense and Security Cooperation – MCO) amewasili Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) kwa ajili ya kuongoza Ujumbe wa Mawaziri wa Mambo ya Nje wa SADC Troika (Tanzania, Angola na Msumbiji) kwa dhumuni la kufanya Misheni ya Pili ya kutathmini hali ya siasa, ulinzi na usalama nchini humo.
Misheni hii inafanyika kufuatia Azimio la Mkutano wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa SADC Troika Mbili uliofanyika Falme ya Swaziland tarehe 17 Machi, 2017. Mkutano huo uliagiza kufanyika kwa Misheni ya Pili ili kuendelea kufuatilia kwa ukaribu maendeleo ya hali ya siasa nchini DRC wakati ikifanya maandalizi ya Uchaguzi Mkuu unaotarajiwa kufanyika mwezi Desemba, 2017.
Sambamba na hayo, Viongozi Wakuu katika Mkutano huo walipokea na kujadili taarifa ya hatua zilizochukuliwa na SADC katika kutatua changamoto za kisiasa, kiulinzi na kiusalama katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo ikiwemo Taarifa ya Misheni ya Kwanza ya Mawaziri iliyofanyika mwezi Oktoba, 2016 na Taarifa ya Misheni ya Timu ya Wataalam wa SADC nchini DRC iliyofanyika mwezi Februari, 2017.
Katika Misheni hii ya Pili, ujumbe wa Angola utaongozwa na Mhe. Manuel Augusto, Naibu Waziri wa Mambo ya Nje; na ujumbe wa Msumbiji utaongozwa na Mhe. Nyeleti Mondlane, Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa.
Ratiba inaonyesha kuwa ujumbe wa Misheni ya Mawaziri wa SADC utakutana na kufanya mazungumzo na wadau wafuatao: Serikali ya DRC akiwemo Waziri wa Mambo ya Nje wa nchi hiyo; Wawakilishi wa Jeshi la Walinda Amani wa Umoja wa Mataifa (MONUSCO); Wawakilishi wa Baraza la Maaskofu Katoliki nchini DRC (CENCO); Wawakilishi wa Vyama vya Siasa na Asasi za Kiraia; na Ofisi ya Rais – DRC. Aidha, Mawaziri watapata pia fursa ya kufanya mazungumzo na Mabalozi wa nchi wanachama wa SADC wenye makazi mjini Kinshasa.
Misheni inatarajiwa kukamilika tarehe 21 Aprili, 2017.
-Mwisho-
Imetolewa na:
Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali,
Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki,
Dar es Salaam
19 Aprili, 2017
No comments:
Post a Comment