Katika hali isiyotarajiwa, baadhi ya wagonjwa waliolazwa katika Hospitali ya Wilaya ya Bukombe mkoani Geita juzi walikataa kupokea msaada wa vyakula na sabuni kama zawadi ya sikukuu ya Pasaka, badala yake wakaomba wapelekewe dawa na vifaa tiba.
Tukio hilo lililoacha gumzo lilitokea wakati kikundi cha Huruma kinachoundwa na wanawake wajasiriamali Wilaya ya Bukombe kilipotembelea hospitali hiyo kugawa zawadi kwa wagonjwa.
Mmoja wa wagonjwa waliogoma kupokea zawadi hiyo, Lucia Mbalala alisema muda umefika kwa wanaoguswa kusaidia wagonjwa kwa kutumia fedha kidogo walizonazo kununulia vitu muhimu vitakavyosaidia matibabu ikiwamo dawa na vifaa tiba badala ya chakula.
“Inamfaa nini kumpa zawadi ya chakula na sabuni mgonjwa aliyelazwa hospitalini siku tatu bila kupata hata ya panadol? Lazima Watanzania tubadilike kimtazamo kwa kukataa zawadi zisizo na tija katika maisha na jamii yetu,” alisema Mbalala.
Mgonjwa mwingine, Annastazia Deus alivitaka vikundi na watu binafsi wanaofikiria kuwasaidia wagonjwa kufikiria hata kuwanunulia nguo watoto wachanga ambao baadhi hawana nguo kutokana na hali duni ya wazazi wao, badala ya kila mmoja kukariri kuwa zawadi kwa wagonjwa ni chakula na sabuni pekee.
Akizungumza wakati wa hafla fupi ya kupokea zawadi hizo, Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Wilaya Bukombe, Dk Nyamhanga Range alisema hospitali hiyo yenye uwezo wa kupokea na kuhudmia wagonjwa 116 inakabiliwa na upungufu wa vifaa tiba.
Aliomba vikundi na watu binafsi wenye mapenzi mema kujitokeza kusaidia upatikanaji wa vifaa tiba kwa ajili ya makundi maalumu wakiwamo wazee, wajawazito na watoto.
“Tunahitaji mashine maalumu ya joto kwa ajili ya watoto wanaozaliwa kabla ya wakati, nepi na nguo kwa ajili ya watoto wachanga,” alisema Dk Range.
Mwenyekiti wa kikundi cha Huruma, Rebeka Juma alisema wanachama wa kikundi hicho walijitolea kujichangisha Sh316, 000 kwa ajili ya kununulia chakula na vifaa vya usafi kama sabuni kwa ajili ya wagonjwa kama mkono wa sikukuu ya Pasaka.
Alisema watafanyia kazi maombi ya wagonjwa na uongozi wa hospitali kuhusu vifaa tiba akiahidi kuwasiliana makundi na watu wengine kuangalia namna ya kusadiana kutafutia ufumbuzi suala hilo.
Chanzo: Mwananchi
No comments:
Post a Comment