Waziri wa Mambo ya Ndani Tanzania Mwigulu Nchemba, amewaonya waumini wa dini mbalimbali nchini kutotumia mwamvuli wa dini kufanya vitendo vya uhalifu ikiwemo kudhuru maisha ya wengine, huku akitangaza kulegeza masharti ya usajili wa nyumba za ibada
Waziri Mwigulu ametoa onyo hilo jana alipokuwa mgeni rasmi katika tamasha la Pasaka lililofanyika katika uwanja wa Taifa Jijini Dar es Salaam, ambapo alisema serikali haitawavumilia watu wa aina hiyo.
Katika hotuba yake fupi Waziri Mwigulu alisema serikali inatambua uhuru wa kuabudu iliyoutoa kwa wananchi wake na inaunga mkono kazi nzuri inayofanyika kupitia ibada, lakini uhuru huo usikwaze wengine, na wala usivunje sheria.
Alisema "Ucha Mungu Siyo Udini", hivyo ni sahihi kwa waumini kumcha Mungu kwa kiwango wanachopenda lakini si kuwashikia silaha watu wengine ili wajiunge na dini zao.
“Wale ambao watatumia misimamo iliyopitiliza kudhuru maisha ya watu wengine, serikali itasimama na kuwahesabia kuwa ni waovu na tutashughulika nao kama wahalifu wengine” Alisema Mwigulu
Katika hatua nyingine, Waziri Nchemba ameagiza taasisi zilizo chini ya wizara yake kulegeza masharti ya usajili wa nyumba za ibada, badala ya kuwapa njia ngumu kwani nyumba hizo ni muhimu kwa ajili ya kumuombea Rais Magufuli na taifa kwa ujumla
"Nimeelekeza watu wangu kuwa waelekezeni watu wanaotaka kusajili nyumba za ibada watimize masharti na muwasajili, hatuwezi kuweka masharti magumu ya kusajili nyumba za ibada halafu tukaweka masharti rahisi ya kusajili bar na kumbi za disco" Alisisitiza Mwigulu
Aliwataka waumini wa dini mbalimbali kuendelea kuliombea taifa, huku akiwapongeza kwa kazi nzuri ya maombi waliyoifanya wakati wa Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015.
"Endeleeni kuliombea taifa letu, wana maombi mkishaomba, mambo yakawa mema, watu huwa hawakumbuki kama mlisugua magoti… hata wakati wa uchaguzi mliomba ndiyo maana tukapita salama wakati kuna watu walitaka kuona Tanzania inayojidai kuwa na amani, itakuwaje.....
"..Wakati ule walikuwa wameandaa magari ya washawasha na mabomu ya machozi lakini nilipofika wizarani nilikuta yale magari yapo hayakutumika pamoja na mabomu, kazi mlishamaliza wana maombi"
Waziri Mwigulu pia alitumia nafasi hiyo kuwahakikishia wasanii wa nyimbo za injili kuwa serikali itafanya kila iwezalo kulinda maslahi ya kazi zao, huku akipongeza kazi nzuri inayofanywa na Rais Magufuli ya kuwaletea maendeleo wananchi licha ya kupingwa na baadhi ya watu na kutolea mifano ujenzi wa reli ya kisasa, ununuzi wa ndege, elimu bure na mengine.
No comments:
Post a Comment