Advertisements

Sunday, May 14, 2017

BALOZI SEIF AONGOZA DUA MAALUM YA KULIOMBEA AMANI TAIFA

Waumini wa Dini ya Kiislamu wakisoma Dua maalum ya kuliombea Taifa Amani na Utulivu pamoja na kujiandaa kuukaribishwa Mwezi Mtukufu wa Ramadhani iliyofanyika katika Msiki wa Ijumaa Malindi Mjini Zanzibar.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar akijumuika pamoja na Waumini mbali mbali wa dini ya Kiislamu Nchini katika Dua maalum ya kuliombea Taifa Amani na Utulivu pamoja na kujiandaa kuukaribishwa Mwezi Mtukufu wa Ramadhani. Kulia ya Balozi Seif ni Mufti Mkuu wa Zanzibar Sheikh Saleh Omar Ka’abi pamoja na Sheikh wa Mkoa wa Dar es salaam Sheikha Alhad Mussa Salum.
Mufti Mkuu wa Tanzania Bara Sheikh Abubakar Zubeir Ali wa kwanza kutoka Kushoto, Kadhi Mkuu wa Zanzibar Sheikh Khamis Haji pamoja na Mkuu wa Mkoa Mjini Magharibi Mh. Ayoub Mohamed Mahmoud walikuwa miongoni wa Viongozi walioshiriki Dua

Baadhi ya Waumini wa Dini ya Kiislamu wa Madhehebu ya Shia Kutoka Nchni Iran waliojumuipa pamoja na Waumini wa Zanzibar katika Dua ya kuliombea Taifa Aman.
Maulamaa na wahadhiri kutoka Nchini Misri nao walikuwa miongoni mwa washiriki wa Dua hiyo iliyofanyika katika Msikiti wa Ijumaa Malindi.
Baadhi ya Maimamu wa Misikiti mbali mbali ya Mkoa wa Mjini Magharibi wakisoma Dua hiyo maalum ya kuliombea Taifa Amani na Utulivu pamoja na kujiandaa kuukaribishwa Mwezi Mtukufu wa Ramadhani.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akitoa nasaha ya kuwataka waumini na Wananchi kuendelea kudumisha Amani kwenye Dua ya Kuliombea Taifa amani. Picha na – OMPR – ZNZ.


Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alisema Mkusanyiko wa Waumini wa Dini ya Kiislamu katika mfumo wa kushikamana bila ya kufarakana daima huzaa baraka zinazootesha neema na kheir miongoni mwa Umma huo mtukufu mbele ya Muumba wao Mwenyezi Mungu.


Alisema Vitabu vya Dini na Miongozo yote iliyotolewa katika Vitabu hivyo imekuwa ikielekeza na kusisitiza umuhimu wa Binaadamu hasa Wale walioamini Vitabu hivyo kushikamana pamoja ili lile lengo lao la kumuabudu Mwenyezi Muungu likamilike bila ya kutetereka kwa kitu chochote kile.

Balozi Seif Ali Iddi alisema hayo wakati wa Dua Maalum ya kuliombea Taifa Amani na Utulivu pamoja na kujiandaa kuukaribishwa Mwezi Mtukufu wa Ramadhani unaokaribia kuingia wiki chache zijazo dua iliyofanyika katika Msikiti wa Ijumaa Malindi Mjini Zanzibar na kuhudhuriwa na Mamia ya Waumini wa Dini ya Kiislamu, Wananchi pamoja na baadhi ya Viongozi wa Serikali na Kisiasa.

Alisema Waumini na Wananchi wote wanapaswa kuzingatia umuhimu wa suala la Amani iliyopo Nchini kwani kwa kufanya hivyo kutatoa fursa kwa Waumini hao kutekeleza kwa utulivu Ibada zao sambamba na Wananchi kuendelea na harakati zao za Kimaisha za kila siku.

Aliwahimiza Waumini wa Dini zote hapa Nchini kuendeleza Dua mbali mbali ambazo ndio ufunguo wa Ibada yoyote ile inayomuelekeza Mja kudumu katika ucha Mungu unaotakiwa kudumishwa katika mazingira yanayomzunguuka ya kila siku.

Balozi Seif aliwashukuru Wananchi wa Kisiwa cha Pemba kwa mshikamano wao waliouonyesha ndani ya kiindi hichi cha Mvua za Masika zilizoleta maafa na kusababisha Mamia ya Wakaazi wake kukosa sehemu za Kuishi baada ya nyumba zao kujaa maji na nyengine kuanguka kabisa.

Alisema kitendo hicho cha mshikamano kimerejesha mafungamano ya Wananchi hao kilichokosekana kwa kipindi kirefu kutokana na itikadi zao tofauti za Kisiasa zilizosababisha kutengana na kuleta athari kubwa hata kwenye maeneo ya Ibada katika kumcha Mwenyezi Mungu.

Akizungumzia ujio la Mwezi Mtukufu wa Ramadhani unaotarajiwa kuingia wiki chache zijazo Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif alitoa wito kwa Wafanyabiashara wote hapa Nchini kuacha tabia ya kupandisha bei za bidhaa muhimu zinazotumiwa kwa wingi na waumini wa Dini ya Kiislamu katika kipindi hicho cha saumu.

Alisema tabia hiyo mbaya ni dhambi kubwa na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar haitakuwa na huruma katika kuwachukulia hatua za kisheria wafanyabiashara wowote watakaopandisha bei bidhaa zao bila ya sababu za msingi zitakazokubalika.

Balozi Seif alisema ni vyema kwa Wafanyabiashara kuwaonea huruma Waumini watakaofunga Mwezi Mtukufu wa Ramadhan ambao wengi kati yao wanaeleweka upatikanaji wa kiato chao unakuwa na mazingira ya mashaka.

Mapema Mufti Mkuu wa Tanzania Bara Sheikh Abubakar Zubeir Ali alisema Dua ni fursa kubwa inayompa fursa Mwanaadamu kumuomba Mungu amuelekeze katika njia ya Amani.Sheikh Zubeir alisema Mwenyezi Muungu muda wote hutarajia kuombwa na waumini wake vyenginevyo anaondosha baraka zake na kutowajaalia kheir na hatma njema waombaji hao anayoisisitiza kila siku kufanywa na waja wake.

Hata hivyo Mufti Mkuu huyo wa Tanzania alitahadharisha wazi kwamba zipo ishara zinazoanza kujichomoza za mmong’onyoko wa Maadili unaotishia kutetereka kwa Amani jambo ambalo kila Muumini na Mwananchi anapaswa kuliondoa au kulikemea lisije kuleta athari hapo baadae.

Akimkaribisha Mgeni rasmi katika Dua hiyo Mkuu wa Mkoa Mjini Magharibi Mheshimiwa Ayoub Mohamed Mahmoud aliipongeza Kamati ya Amani ya Kitaifa Zanzibar kwa juhudi inazochukuwa za kuhakikisha kwamba Taifa la Tanzania linaendelea kuwa na utulivu.

Mh. Ayoub alisema Dua hiyo ni tukio muhimu kwa Mustakabala wa Taifa hili na aliwaomba Waumini na Wananchi wote popote pale walipo kuendelea kuwaombea dua Viongozi wao waliojitolea kusimamia mapambano dhidi ya Dawa za kulevya na Mmong’onyoko wa Maadili unaooneka kuliathiri Taifa hasa kundi kubwa la Vijana.

Katika shughuli hiyo ya dua Maalum ya kuliombea Taifa Amani na Utulivu pamoja na kujiandaa kuukaribishwa Mwezi Mtukufu wa Ramadhani Masheikh na Maulamaa wa Mkoa Mjini Magharibi wametoa zawadi Maalum kwa Rais wa Zanzibar Al – Hajj Dr. Ali Mohamed Shein, Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi pamoja na Mkuu wa Mkoa Mjini Magharibi Mheshimiwa Ayoub Mohamed Mahmoud.

Zawadi hizo wamezitoa kutokana na mchango mkubwa wa Viongozi hao katika kusimamia suala la Amani, mapambano dhidi ya Dawa za Kulevya Nchini pamoja na kuzuia mmong’onyoko wa Madili ulioonekana kupotea siku za nyuma.

Dua hiyo ya Ighaathatul – Mustaghiith ambayo pia husomwa kila jumatano baada ya sala ya Ishaa katika Msikiti huo wa Ijumaa wa Malindi iliongozwa na na Mwenyekiti wa Kamati ya Amani ya Kitaifa Zanzibar Sheikh Salim Mohamed Hassan.

Othman Khamks Ame

Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar

14/5/2017.

No comments: