Mkuu wa Mkoa wa Singida Dkt. Rehema Nchimbi akimkabidhi afisa wa usalama kutoka shirika la TANESCO Mkoa wa Singida Juma Mauba zawadi ya cheti na TV flat screen baada ya kuchaguliwa kuwa mfanyakazi bora mwaka 2017.
Mkuu wa Mkoa wa Singida Dkt. Rehema Nchimbi akiwa ameshikama na Mwenyekiti wa Shirikisho la vyama vya wafanyakazi TUCTA Mkoa wa Singida Aaran Jumbe (kulia kwake) na Mkuu wa Wilaya ya Singida Elias Tarimo (kushoto kwake) wakiimba wimbo maalumu wa wafanyakazi wa Mshikamano daima pamoja na wimbo wa taifa.
Watumishi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Singida wakimsikiliza Mkuu wa Mkoa wa Singida Dkt. Rehema Nchimbi wakati akihutubia kwenye maadhimisho ya siku ya wafanyakazi kwa Mkoa wa Singida.
Watumishi wa Kutoka Halmashauri ya Ikungi wakipita mbele ya Mkuu wa Mkoa wa Singida Dkt. Rehema Nchimbi na kuonyeshwa mazao ambayo huzalishwa kwa wingi wilayani humo ambayo ni viazi vitamu na alizeti katika maadhimisho ya siku ya wafanyakazi kwa Mkoa kwa Mkoa wa Singida.
Mkuu wa Mkoa wa Singida Dkt. Rehema Nchimbi akitoa zawadi ya mpira kwa viongozi wa wafanyakazi wanawake kwa halmashauri zote saba za Mkoa wa Singida ili waweze kuunda timu za wanawake katika halmashauri zao.
Waajiri wote Mkoani Singida hususani wakurugenzi wa halmashauri ambao ndio wenye watumishi wengi wameelekezwa kujenga mahusiano mazuri baina yao ili kuboresha utumishi wao.
Mkuu wa Mkoa wa Singida Dkt. Rehema Nchimbi ametoa maelekezo hayo wakati wa maadhimisho ya siku ya wafanyakazi mkoani hapa yaliyofanyika katika uwanja wa Peolpe’s mjini Singida.
Dkt. Nchimbi amesema mwajiri na mtumishi sio maadui bali wanapaswa kujenga mahusiani mazuri hasa kwa mwajiri kujenga mazoea ya kufahamu sifa za watumishi wake, shida na matatizo yao.
Ameongeza kuwa waajiri wamekuwa wakisubiria watumishi wakosee ndio wawape adhabu lakini haipaswi kuwa hivyo kwani mwajiri anatakiwa ahakikishe anaweka mazingira mazuri na kumuelimisha mtumishi asifanye makosa.
“Ukiona mtumishi anafanya mambo yanayokinzana na sheria, kanuni na utaratibu, usimkaripie wala kumtega, mtafutie afisa ustawi wa jamii. Kwa vyo vyote afisa ustawi wa jamii atamrejesha kwenye mstari stahiki na mambo yatakwenda vizuri”.
Aidha Dkt Nchimbi amewataka wakurugenzi kutofanya ziara nyingi nje ya halmashauri zao bali wajikite katika kusikiliza na kutatua kero za wananchi na watumishi wao ambazo watazibaini endapo watafanya ziara za kutosha katika halmashauri zao.
Amesema ili kuboresha maslahi ya watumishi, waajiri wanapaswa kuandaa mafunzo kwa watumishi juu ya matumizi bora ya fedha ili waweze kutunza fedha zao, kila halmashauri kutenga maeneo kwa ajili ya watumishi kupewa viwanja vya makazi pamoja na kila halmashauri kuwa na afisa ustawi wa jamii atayehusika na watumishi kwa ajila ya masuala ya ushauri.
Pia Dkt. Nchimbi amekemea tabia mbaya ya baadhi ya wakuu wa idara/vitengo ya kuwa na mahusiano ya kimapenzi na wafanyakazi wa kike walio chini yao.
“Wakuu hawa wa idara/vitengo wanakiuka sheria kanuni na taratibu kwa kuanzisha mahusiano ya kimapenzi humo humo kazini. Wakati mwingine wanafanya mapenzi na wake za watu. Tabia hii haikubaliki na haivumiliki hata kidogo. Viongozi au wakuu wa idara/vitengo wenye tabia ya aina hii, waiache mara moja”, amesema Dk.Nchimbi.
Kwa upande wao wananchi na watumishi Mkoani Singida wamempongeza rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli kwa hatua zake utumishi wa umma ambapo kwa sasa amerejesha nidhamu na uadilifu kwa kiwango cha kuridhisha.
Wananchi hao wamesema chini ya serikali ya awamu ya tano watumishi wa umma wamebadilika sana na sasa wanatoa huduma kwa ukarimu mkubwa, wepesi na uharaka zaidi tofauti na ilivyokuwa awali.
“Huko nyuma watumishi wa umma wengi walikuwa wana urasimu wa hali ya juu. Walikuwa wakitoa huduma huku macho na akili zao zikiwa kwenye ‘whatsapp’. Mbaya zaidi mwananchi ukipeleka kero zako, wanakuona ni msumbufu. Hivi sasa mambo ni tofauti kero za wananchi zinatafutiwa majibu na majawabu kwa wakati,” ameongeza Dkt. Nchimbi akiunga mkono maoni ya wananchi.
Mmoja wa wananchi waliohudhuria maadhimisho hayo Sombi Hangida amekiri kwamba ni kweli watumishi wa umma wamebadilika mno na sasa wanatoa huduma bila kuomba rushwa na wamekuwa na lugha rafiki kwa wananchi.
Awali mwenyekiti wa Shirikisho la Vyama vya wafanyakazi TUCTA Mkoani Singida Aaran Jumbe amehimiza kuhusu mabaraza ya wafanyakazi kufanyika katika maeneo ya kazi kwa mujibu wa sheria, kanuni na taratibu na hasa kuwashirikisha vyama vya wafanyakazi.
Jumbe ameongeza kuwa halmashauri zimekuwa zikitoa ushirikiano kwa vyama vya wafanyakazi na kuomba ushirikiano huo uendelee huku akisisitiza zawadi za mfanyakazi hodari zinazo ahidiwa na taasisi na halmashauri zitolewe kwa wakati.
No comments:
Post a Comment