ANGALIA LIVE NEWS

Wednesday, May 10, 2017

KAMATI YA MAAFA ZANZIBAR YAKUTANA KUJADILI MVUA ZA MASIKA ZINAZOENDELEA KUNYESHA

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi kulia akikiongoza Kikao cha Kamati ya Kitaifa ya Kukabiliana na Maafa Zanzibar akiwa Mwenyekiti Ofisini kwake Vuga Mjini Zanzibar. Wa kwanza kulia ni Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mheshimiwa Mohamed Aboud Mohamed.

Kamati ya Kitaifa ya Kukabiliana na Maafa Zanzibar chini ya Mwenyekiti wake Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi imekutana Ofisini kwake Vuga Mjini Zanzibar kutathmini Mvua za Masika na muelekeo wa kukabiliana na changamoto zilizoanza kuibuka.

Tathmini hiyo imekuja kufuatia mvua kubwa zinazoendelea kunyesha katika Maeneo mbali mbali ya Visiwa vya Unguja na Pemba na kuathiri Nyumba 325 Mkoa Kusinin Pemba, Nyumba 667 kuhamwa ndani ya Mkoa Mjini Magharibi pamoja na kubomoka kwa miundombinu ya Bara bara na baadhi ya Madaraja hasa Kisiwani Pemba.

Akitoa Taarifa za awali za athari ya mvua zilizojitokeza kwa mwaka wa 2017 tokea kuanza kwa msimu wa Mvua za Masika, Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Kukabiliana na Maafa Zanzibar Nd. Ali Juma Hamad alisema athari ya Mvua hizo zimesababisha maporomoko ya ardhi yaliyosababisha kufukia kwa baadhi ya Nyumba na Bara bara.

Nd. Ali alisema ziara za Viongozi wa Serikali zimegundua athari kubwa ya uharibifu wa miundombinu ya Bara bara na nyumba kutokana na mvua hizo hasa katika Mkoa wa Kusini Pemba na kusababisha kifo cha Mtoto Mmoja Ramadhan Mohamed baada ya kuangukiwa na ukuta wa Madrasa Chanjani Chake Chake Pemba.

Naye Mkurugenzi wa Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania Kanda ya Zanzibar Nd. Mohamed Khamis Ngwali alisema bado Visiwa vya Unguja na Pemba viko katika msimu wa mvua hali ambayo wananchi wanapaswa kufuatilia Taarifa zainazotolewa na Mamlaka ya Hali ya Hewa.

Nd.Ngwali alisema viwango vya mvua katika visiwa vya Zanzibar viongezeka kama vilivyotangazwa na Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania mnamo Tarehe 28 Mwezi uliopita na kuanza kunyesha mara moja siku iliyofuata.

Kwa upande wake Mkurugenzi Idara ya Kinga Wizara ya Afya Dr.Fadhil Abdulla alieleza kwamba Wizara ya Afya tayari imeshajiandaa na changamoto yoyote inayoweza kujitokeza endapo kutaibuka kwa maradhi ya mripuko katika kipindi hichi cha msimu wa mvua za masika.

Dr. Fadhil alisema udhibiti wa vyakula vinavyouzwa katika maeneo ya wazi bado mgumu na ndio uliochangia kuibuka kwa maradhi ya Kipindupindu mwaka jana kwa asilimia 16%.

Alisema katika kukabidhiana na udhibiti wa mfumko wa maradhi ya kuambukiza Wataalamu wa Afya tayari wameshapima wagonjwa 22 walioonyesha ishara ya kusumbuliwa na maradhi ya matumbo ya kuharisha.

Dr. Fadhil alitanabaisha wazi kwa jamii kwamba suala la matumizi bora ya maji safi na salama ndio jambo la msingi litakalosaidia kujikinga na maradhi ya kuambukiza ikiwemo kipindupindu.

Wakichangia mjadala huo baadhi ya Wajumbe wa Kamati ya Kitaifa ya Kukabiliana na Maafa Zanzibar walisema upo umuhimu wa wataalamu kuendelea kutumia vyombo vya habari katika kuwaelimisha wananchi juu ya kujikinga na maradhi mbali mbali.

Walisema suala la kutibu maji kwa kuyatia dawa ni jambo la msingi kwa vile chanzo cha magonjwa ya miripuko ukiwemo ule wa hatari wa kuharisha ni matumizi mabaya ya maji yasiyo salama.

Akiahirisha Kikao hicho Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar ambae ni Mwenyekiti wa Kamati ya Kitaifa ya Kukabiliana na Maafa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alisema ipo haja ya kuandaliwa mikakati ya muda mrefu ya kukabiliana na changamoto zinazojitokeza kila mwaka wakati wa msimu wa mvua za Masika.

Balozi Seif alisema mpango wa kutibu maji safi na salama kabla ya matumizi ya binaadamu linafaa kuzingatiwa ili kusaidia kujikinga na maradhi yanayosababishwa na maji.

Alieleza kwamba elimu ya Afya iendelee kutolewa na Wataalamu wa afya itakayokwenda sambamba na kujiepusha na viashiria vyote vinavyosababisha kupata maradhi ya mripuko ikiwemo ulaji wa vyakula ovyo.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alifahamisha kwamba Serikali Kuu inaangalia utaratibu wa namna inavyoweza kuwasaidia Wananchi ambao nyumba zao zimeharibika kabisa kutokana na mafuriko ya Mvua.

Othman Khamis Ame

Ofisi ya Makamu wa 9ili wa Rais wa Zanzibar9/5/2o17.

No comments: