NA ELVAN STAMBULI | GAZETI LA UWAZI | NIONAVYO MIMI
NILIKUWA sikupanga kuandika makala haya lakini nimeamua kuandika baada ya tukio lililotikisa nchi nzima.
Ni tukio la wafanyakazi wa serikali zaidi ya 9,932 kukutwa na vyeti feki vya kitaaluma. Inanifanya niamini kwamba wapo wanafiki ambao wanapokuwa majukwaani wanamlilia na kumkumbuka Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere lakini matendo yao ni tofauti kabisa na wanavyomkumbuka.
Waliogundulika kuwa na vyeti bandia ni wengi sana ndiyo maana taifa linakwenda ndivyo sivyo kwani inawezekana kuna wenye madaraka walikuwa na ziro nyingi, hivyo kukosa weledi wa utendaji.
Mtu anakuwa na madaraka makubwa kwa kuamini kwamba ana taaluma nzuri, kumbe ni ‘kihiyo’ (alikuwa amejipatia ubunge wakati hakuwa na vyeti halali).
Ndiyo maana watu wa aina hiyo wapo tayari kuwagawa Watanzania katika makundi ya vyama, makabila na dini ili wawe katika madaraka na waendelee kushibisha matumbo yao na kulitelekeza taifa.
Watu wenye tabia ya kufoji vyeti ni wabaya kama alivyosema Rais Dk. John Magufuli, ni sawa na majambazi.
Kwa nini namkumbuka Mwalimu Nyerere? Ni kwa sababu alikuwa mjamaa, mtetezi wa haki za binadamu, aliyependekeza na kutamani kuona Afrika ikiungana. Alikuwa msomi na mchambuzi, mwandishi mwenye hekima na busara, upendo wa dhati kwa wananchi wake na huruma. Alikuwa na upendo na huruma, zaidi ya yote alikuwa na maono.
Kiongozi huyo alikwenda kwa hoja, ukimshinda kwa hoja anakuunga mkono.Wengi wanaojifanya kumkumbuka ni wanafiki, mifano ni mingi ya wanafiki hawa.
Mifano ya uadilifu wa Nyerere ipo mingi, angalia watoto wake ambao sijawahi kuwaona wakijitutumua kuonesha ufahari wowote kwamba wao ni watoto wa baba wa taifa.
Sikushangaa, ila kusema kweli si jambo la kawaida na hasa kwenye nchi za Afrika; mtoto wa aliyekuwa rais wa nchi, tena rais wa kwanza kuwa mtu wa kawaida kama wengine na kudiriki kupanda daladala.
Wengi huwa na magari yao ya kifahari na dereva wa kuwaendesha, lakini mtoto wa Mwalimu Nyerere alishawahi kuingia kwenye daladala kama msafiri yeyote yule, naikumbuka siku hiyo na watu wakashangaa.
Huwa nakaa na kutafakari juu ya Mwalimu Nyerere na upekee wake, uongozi, uzalendo na mapenzi yake kwa Watanzania. Hata hivyo, zaidi nilitafakari juu ya malezi ya watoto wake. Mwalimu aliwapatia malezi ambayo watoto wengi Watanzania huwa wanayapata isipokuwa wachache wa vigogo.
Watoto wake walisoma kwenye shule zile walizosomea watoto wengine wa walalahoi wa Tanzania. Mwalimu aliamua kutoa elimu ya bure si kwa watoto wake, bali kwa watoto wote wa Tanzania. Kama si mpango wa Mwalimu Nyerere wa kutoa elimu ya bure watu wengi leo hii wasingekuwa na elimu waliyonayo hata mimi ninayeandika makala haya.
Hata watendaji wake, yaani mawaziri watoto wao walikuwa wakisoma shule za kawaida. Nakumbuka nilipokuwa nasoma Shule ya Sekondari ya Umbwe, Kibosho Moshi nilikuwa nasoma na mtoto wa Waziri Mkuu (enzi hizo), Cleopa Msuya, anaitwa David, alikuwa anaishi kawaida kabisa na hakuwa na majivuno, badala yake alikuwa mpole na mtulivu sana.
Naambiwa hata mtoto wa Mwalimu Nyerere, Makongoro alipokuwa anasoma Tabora Boys, alikuwa anakwenda kutembea Kipalapala na kula mapera kama watoto wengine. Alikuwa akitembea kutoka Tabora Boys hadi Kipalapala kwa miguu kama watoto wengine. Bila kuambiwa kwamba ni mtoto wa rais, ilikuwa vigumu kutambua. Alikuwa hana majivuno kwa sababu ya kulelewa katika mazingira ya kujitambua kwamba yeye hana tofauti na watoto wengine.
Mwalimu hakumpatia mtoto wake yeyote yule cheo cha upendeleo ndani ya serikali yake na wala hakuwashawishi watoto wake kuingia kwenye siasa kama tunavyoona kwa baadhi ya viongozi leo. Sote tulishuhudia Makongoro alivyojiingiza kwenye siasa badala ya kuiingia kwenye chama cha baba yake, akajiunga na upinzani NCCR tena baada ya kumbembeleza.
Mwanaye mwingine, Rose Nyerere aliingia bungeni baada ya kifo cha baba yake. Historia haituonyeshi mtoto wa Mwalimu aliyependelewa kwa aina yoyote ile. Kila mmoja mahali alipo, amepambana kama watoto wengine wote wanavyopambana na maisha na kufanikiwa.
Mwalimu hakuwapendelea watoto wake au kumuamuru mrithi wake Ali Hassan Mwinyi kuwafanyia upendeleo wa vyeo. Aliwapenda watoto wote wa Tanzania. Alijenga shule, vyuo vya watoto wote wa Tanzania. Lengo lake kubwa lilikuwa kuiandaa nchi yenye neema kwa vizazi vijavyo.
Mwalimu Nyerere hakuwapeleka watoto wake kusoma nje ya nchi. Kama kuna mtoto wake aliyefanikiwa kusoma huko, atakuwa alisaidiwa na wamisionari. Ninakumbuka Mwalimu mwenyewe akiwa hai, alisema kwamba mmoja wa watoto wake alipata msaada kusoma Canada na kwamba msaada huo ulitolewa na wamisionari.
Nina imani kama Mwalimu angekuwa hai bado, wajukuu zake wangesoma kwenye sekondari za kata kwani hakupenda kuwatenga watoto wake na jamii.
Watoto wake walijiunga na Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) kama watoto wengine. Huko waliishi na kufanya kila kitu kama watoto wengine wote walivyokuwa wakifanya.
Leo hii wale wote wanaojifanya wanamlilia Mwalimu, ni nani anafuata mifano yake? Ni mtoto gani wa kiongozi anapanda daladala? Ni mtoto gani wa kiongozi anasoma kwenye sekondari za kata? Ni mtoto gani wa kiongozi asiyesoma nje ya nchi?
Tumesikia habari za baadhi ya watoto wa viongozi kuwashikia watu bastola, lakini hawafikishwi mbele ya sheria. Tumeshuhudia watoto wa viongozi wakiingizwa kwenye siasa na kupata nafasi za juu. Tumeshuhudia watoto wa viongozi wakifanya biashara na kupata upendeleo na leo tunasikia watu wakifoji vyeti ili wapate kazi nzuri.
Wapo baadhi ya watu wanaomlaumu Mwalimu Nyerere kwa siasa yake ya Ujamaa na Kujitegemea. Wengine wanamlaumu kwa kile wanachokiita ‘kuitelekeza’ familia yake, kwamba hakuwatafutia watoto wake nafasi nzuri katika mfumo wa serikali au kuiba mali za umma ili waneemeke.
Wanasema Mwalimu Nyerere alikosea, alidumaza uchumi wetu. Ukweli ni kwamba Mwalimu Nyerere, aliona mbali. Siasa ya Ujamaa na Kujitegemea ilikuwa silaha kubwa ya kupambana na ukoloni mambo leo na ubeberu mamboleo.
Mwalimu, alijua wazi kabisa kwamba ungefika wakati tutazidiwa nguvu na Ukoloni Mambo leo, alijua wazi kwamba tutafikia mahali tungevamiwa na wawekezaji kwa mgongo wa utandawazi.
Sasa utajiri wetu unaporwa na wageni. Badala ya kujenga uchumi wa taifa letu, tunajenga na kukuza uchumi wa mataifa mengine. Badala ya kuulinda uhuru wetu, tunakubali kuwa ‘watumwa’.
Kwa mtazamo wangu ni kwamba Mwalimu Nyerere alifanya makosa mawili katika maisha yake; kosa la kwanza ambalo limemgharimu ni kuwaamini watu ambao ndiyo wale wale walioangusha na kuyazika maono yake. Wale aliowaamini ndiyo waliolizika Azimio la Arusha kule Zanzibar. Ni watu wachache wa aina ya Rashid Kawawa walibaki waaminifu kwa Mwalimu. Wengine walikuwa wanafiki, walitaka vyeo na utajiri wa haraka.
Walionyesha unyenyekevu kwa Mwalimu Nyerere, walizungumza kama yeye na kuvaa nguo kama zake. Baada ya Mwalimu Nyerere kutoka madarakani, watu hawa walibadilika haraka, walianza kuongea lugha nyingine na kuvaa ngozi za Kizungu.
Kosa la pili la Mwalimu Nyerere ni kwenda haraka. Mfano, hakujipatia nafasi kufanya maandalizi ya kutosha kabla ya kufanya uamuzi wa Azimio la Arusha.
Hakuwaandaa watu kupokea siasa ya ujamaa na kujitegemea. Alifanya haraka ya kutaifisha, viwanda, shule na hospitali. Uharaka huu, ambao haushangazi kwa mwanamapinduzi kama alivyokuwa Mwalimu Nyerere ndiyo sababu kubwa ya kuanguka kwa siasa ya ujamaa na kujitegemea.
Hata hivyo, mimi ni miongoni mwa watu wanaotetea uharaka wa Mwalimu Nyerere. Ni kweli kwamba aliona mbali. Alifikiri kwamba bila kujenga ujamaa kwa haraka tungemezwa bila maandalizi.
Baada ya Uhuru, Mwalimu Nyerere alitangaza maadui wa taifa letu kwamba ni maradhi, ujinga na umaskini. Na kwamba silaha pekee ya kupambana na maadui hawa ni ardhi, siasa safi, uongozi bora na watu.
Hatukusikia malalamiko ya madini kusombwa na kupelekwa nje tena na mchanga wake, hatukusikia wizi wa magogo, hatukusikia vitalu vya wawindaji kuvamiwa na kuibwa wanyama hai wala hatukusikia watu wakifoji vyeti au kupitisha makontena ya wizi bandarini, nabaki kujiuliza, tunakwenda wapi? Ndiyo maana namkumbuka Nyerere!
No comments:
Post a Comment