Advertisements

Tuesday, May 9, 2017

‘Tumebaki nusu bwenini’

Wanafunzi wa shule mbalimbali za jijini Arusha wakibubujikwa na machozi walipohudhuria ibada maalumu ya kuaga miili ya wanafunzi 32, walimu wawili na dereva mmoja wa Shule ya Lucky Vicent kwenye Uwanja wa Sheikh Amri Abeid jana. Picha na Filbert Rweyemamu

By Mussa Juma, Mwananchi mjuma@mwananchi.co.tz

Arusha. Baada ya Shule ya Msingi ya Lucky Vicent kupoteza wanafunzi 32, walimu wawili na dereva katika ajali ya gari iliyotokea wilayani Karatu, wanafunzi wengine wamesema wamebaki nusu ya wanafunzi bwenini.

Kila mwanafunzi ameonekana mwenye hisia katika hafla maalumu ya kuaga miili ya wenzao kwenye Uwanja wa Sheikh Amri Abeid mjini hapa na msiba huu unaonekana utaendelea kuwa katika vichwa vya wanafunzi waliobaki kwa muda mrefu.

Ndiyo maana imemlazimu Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Dk Eva Maria Semakafu kutoa ushauri wa uongozi wa elimu jijini Arusha, kuwatafutia mwalimu wa saikolojia ili awawezeshe kukabiliana na hali hiyo.

Noreen Josia, mwanafunzi wa shule hiyo anayesoma darasa la sita, anasema hatasahau msiba huo.

Anasema alishtushwa na taarifa kuwa gari lao la shule limepata ajali kutokana na simu ambazo zilikuwa zinapigwa na pia taarifa kusambaa kwenye mitandao ya kijamii.

“Nilirudi shuleni kuuliza kama ni kweli, nikaambiwa ni kweli. Tangu wakati huo hadi sasa, sijisikii vizuri, nahisi kuumwa kwa kuwa bwenini kwetu karibu nusu ya wanafunzi sijawaona. Nadhani wamefariki,” amesema huku akitokwa na machozi.

Noreen, ambaye muda mwingi, alikuwa ameshikiliwa na watoa huduma wa Msalaba Mwekundu, alisema: “Siwezi kusahau kwa kuwa tulikuwa nao bwenini wakati wakijiandaa kwenda kwenye mitihani ya majaribio Karatu na tuliagana. Sasa kuambiwa hawapo tena ni jambo ambalo siwezi kusahau,” anasema.

Noreen anawakilisha idadi kubwa ya wanafunzi wa shule hiyo ambao wameathiriwa na msiba huo mkubwa wa aina yake na ambao wamepewa siku saba za mapumziko kwa majili ya kutuliza akili.

Mwalimu mkuu wa shule hiyo, Ephraim Jackson anasema, wanafunzi 96 wa darasa la saba ndio walisafiri kati ya wanafunzi 106 wa darasa hilo.

No comments: