Mkuu wa Mkoa wa Singida Dkt. Rehema Nchimbi akikagua ujenzi wa uwanja wa Namfua uliopo Manispaa ya Singida, kulia kwake ni Mkuu wa Usalama wa Taifa Mkoa wa Singida
Uwanja wa Namfua uliopo manispaa ya Singida ambao ukarabati wake umefikia hatua ya kuridhisha umeanza kutoa matumaini kwa wananchi wa Singida ambao wamekuwa wakifuatilia kwa karibu ukarabati wake.
Mkuu wa Mkoa wa Singida Dkt. Rehema Nchimbi akiwa pamoja na Mkuu wa Usalama wa Taifa Mkoa wa Singida wamefanya ziara ya kushtukiza kujionea hatua iliyofikiwa katika ujenzi wa uwanja huo ambao utatumika kama uwanja wa nyumbani wa timu ya Mpira wa Miguu iliyobeba jina la mkoa ‘Singida United’.
Dkt. Nchimbi amesema anaridhishwa na kasi ya utengenezaji wa uwanja wa Namfua unaomilikiwa cha chama cha Mapinduzi Mkoa wa Singida huku akiupongeza uongozi wa CCM mkoa wa hatua ilipofikia uwanja huo kwa kuwa ni tegemeo la fursa nyingi hasa za wajasiriamali wadogo.
“Chama cha Mapinduzi kimetengeneza fursa na ajira nyingi kwa wajasirimali mkoani Singida kwa kuukarabati Uwanja huu ili uweze kutumika na timu ya Singida United ambayo inatupa heshima kubwa wana Singida”, ameongeza Dkt. Nchimbi.
Ameongeza kuwa wananchi wa Singida wana hamu kubwa ya kuziona timu kubwa zinazocheza ligi kuu Tanzania bara zikicheza katika uwanja wa Namfua na hivyo kuitumia fursa hiyo kufanya biashara mbalimbali.
Aidha Dkt. Nchimbi amesema kuwa uwanja huo utakuwa ni chanzo cha mapato kwa mmiliki wa uwanja huo ambaye ni CCM Mkoa wa Singida, huku timu zitakazocheza, TFF na Manispaa ya Singida watapata mgao wao kulingana na taratibu zilizopo.
Kwa upande wao vijana waliokuwa wakishuhudia ukarabati wa uwanja huo wamesema wamejiandaa kuuza bidhaa kama jezi na vipeperushi vya timu kubwa huku wakisema watatoa kipaumbele katika kuuza na kuvaa jezi za timu yao ya Singida United.
Wameongeza kuwa uwanja huo ni faraja kwa kila mjasirimali mkoani Singida wakitoa mfano kwa wamiliki wa hoteli, nyumba za kulala wageni, wauzaji wa vinywaji na bidhaa ambazo zinapatikana mkoani Singida kwa ubora mkubwa ambazo ni asali, mafuta ya alizeti, kuku wa kienyeji, vitunguu bora na Viazi vitamu watapata wateja wa kutosha.
Uwanja wa Namfua uliopo Manispaa ya Singida ukiendelea kukarabatiwa.
Mkuu wa Mkoa wa Singida Dkt. Rehema Nchimbi akikagua ujenzi wa uwanja wa Namfua uliopo Manispaa ya Singida, kulia kwake ni Mkuu wa Usalama wa Taifa Mkoa wa Singida.
Uwanja wa Namfua uliopo Manispaa ya Singida ukiendelea kukarabatiwa.
No comments:
Post a Comment