ANGALIA LIVE NEWS

Friday, May 5, 2017

VYETI FEKI VYAWATESA WAKURUGENZI, MTALAAM WA KIINGEREZA AKUMBWA

Askari wa Hifadhi ya Taifa ya Serengeti wakijaza fomu za uhakiki wa vyeti vyao kama walivyokutwa kwenye kituo cha Kogatende kwenye hifadhi hiyo mkoani Mara jana. Picha na Anthony Mayunga.

By Waandishi Wetu, Mwananchi mwananchipapers@mwananchi.co.tz

Dar/Mikoani. Wakati athari za matokeo ya ripoti ya uhakiki wa vyeti vya elimu ya sekondari zikizidi kuwa bayana, hasa katika halmashauri, Kinondoni imempoteza mchapakazi aliyekuwa mwandishi tegemeo wa ripoti, hasa za lugha ya Kiingereza.

Hilo limebainika baada ya gazeti la Mwananchi kufanya uchunguzi wa athari hizo katika halmashauri kadhaa, ambako wakurugenzi na wafanyakazi wanalalamikia huduma kudorora kutokana na waliotajwa katika orodha ya watumishi wanaotuhumiwa kuwa na vyeti vya kughushi kuhofia kwenda kazini.

Akipokea ripoti iliyokuwa na orodha ya watumishi wenye vyeti vya kughushi, maarufu kama vyeti feki, Rais John Magufuli alitaka wafanyakazi wote 9,932 waliotajwa kuachishwa kazi mara moja na wale watakaokuwa hawajaacha kazi kwa hiari yao ifikapo Mei 15, wafikishwe mahakamani.

Alimtaka Waziri Mkuu na mawaziri wawili wa Ofisi ya Rais, Angella Kairuki (Utumishi) na George Simbachawene (Tamisemi) kusimam ia suala hilo.

Agizo hilo limesababisha kizaazaa katika halmashauri ambazo zimeathirika kiutendaji katika sekta ya afya na elimu.

Wilayani Kinondoni, mmoja wa watu waliotajwa kuwa ana vyeti vya kughushi ni mtaalamu huyo wa kuandika ripoti, ambaye amepotea ofisini na juhudi za kumpata ili angalau kumfariji, zimeshindikana kutokana na kuzima simu yake.

Mwananchi ilishuhudia shughuli zikiendelea katika ofisi ya Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni, lakini watumishi waliosalia wakilalamika kulemewa na kazi kutokana na wenzao kuondoka.

Akizungumza na gazeti hili, ofisa uhusiano wa Manispaa ya Kinondoni, Sebastian Mhowera alisema tangu orodha hiyo ilipotolewa, kumekuwa na pengo kubwa katika baadhi ya idara.

Tayari Serikali imezitaka idara au taasisi zilizoathirika na suala la vyeti feki, kuomba kibali cha dharura cha kuajiri wafanyakazi. Hata hivyo, mchakato wa kuajiri serikalini huchukua muda kukamilika.

“Unakuta idara ilikuwa na watumishi watano, wawili wameondoka kwa hiyo kazi zao wanazifanya watu watatu. Ni kweli kuna mtikisiko kidogo lakini tunaangalia ndani ya siku hizi chahe tuone hali itakuwaje,” alisema.

Alisema wote waliotajwa hawaruhusiwi kuwepo kazini na hata wakionekana wanakamatwa na kupelekwa polisi. Kwa hiyo hawafiki na kwamba wapo ambao kuondoka kwao kumeleta mtikisiko kwa baadhi ya idara.

“Tulikuwa na mtumishi idara ya utawala anayeitwa Fred Uiso, yeye alikuwa katibu muhtasi. Alikuwa mwandishi wa ripoti mbalimbli na alikuwa mtaalamu wa Kingereza. Ripoti zote za Kiingereza alikuwa anaziandaa yeye,” alisema Mhowera.

“Alikuwa anafanya kazi wakati mwingine hadi usiku. Siku za weekend (za mwisho wa juma) alikuwa anakuja ofisini.

“Tuseme tulimtegemea sana na hata orodha ilivyotoka, alikuwa hajaiona na alikuwa anakuja ofisini. Jana (juzi) ndio tukamwambia ukweli. Alionekana kuchanganyikiwa.”

Mhowera alisema baada ya kuona jina lake, Uiso aliondoka na tangu siku hiyo hajaonekana.

“Hata kwa simu yake ya mkononi hapatikani. Kwa kweli kuondoka kwake kumeleta shida maana yeye ndiye alikuwa tegemeo kwa kuandaa ripoti.”

Hali ni kama hiyo katika Halmashauri ya Wilaya ya Babati ambako mkurugenzi mtendaji wake, Hamis Malinga amesema sasa wana upungufu mkubwa wa watumishi.

Malinga alisema anajitahidi kurekebisha ili kwa wakati huu huduma zisizorote.

Alisema ameshaandika barua kwa katibu mkuu wa Utumishi ili kupata kibali cha kuajiri kwa lengo la kujaza nafasi za waliotoweka.

Wilayani Newala, magari yanashinda katika maegesho kutokana na kukosa madereva, wakati walimu wanakosekana shuleni.

Mkurugenzi mtendaji wa halmashauri hiyo, Mussa Chimae alisema pia baadhi ya ofisi za watendaji wa vijiji nazo zimekosa watendaji.

“Katika halmashauri yangu wapo 15, athari ni kwamba kuna baadhi ya nafasi zimekosa watumishi, kwa mfano kuna magari yamepaki kwa kukosa dereva. Pia kuna wanafunzi wamekosa vipindi kwa kukosa walimu na baadhi ya ofisi za watendaji wa vijiji zimekosa watendaji,” alisema Chimae.

Hali ni kama hiyo katika Manispaa ya Mtwara Mikindani ambako ofisa habari wake, Jamadi Omari alisema athari zipo kwa upande wa walimu kutokana na kutokuwa na uwiano baina ya mwalimu na wanafunzi.

“Walimu wa shule za msingi wamepungua wanne na kwa mujibu wa uwiano mwalimu mmoja anafundisha wanafunzi arobaini, hivyo wanne ni sawa na wanafundisha wanafunzi 160. Hivyo upungufu wa walimu wanne una athari kwa wananfunzi wetu,” alisema Omari.

Halmashauri ya Tandahimba ndiyo imeathirika zaidi baada ya wafanyakazi 52 kukumbwa na tatizo hilo.

Ofisa utumishi wa Tandahimba, Ahmada Suleiman alisema idara ya afya ndiyo imeathirika zaidi baada ya wafanyakazi 33 kuwa katika orodha ya wanaotuhumiwa kuwa na vyeti vya kughushi.

Idara nyingine ni elimu ya msingi iliyopoteza wafanyakazi 12, kilimo (2), utawala (4) na fedha (1).

“Kwanza maeneo waliyokuwa wakifanya kazi yalikuwa na upungufu. Mfano hospitali kulikuwa na shift (zamu) na tuna miaka miwili Serikali haijaajiri. Kama unavyojua sisi ni binadamu, watu wanafariki hivyo ni lazima kujaza hizo nafasi. Na zoezi lilivyokuja, limeathiri zaidi,” alisema Suleiman.

Wakati hali ikiwa mbaya, mwalimu mmoja mkazi wa Ilala jana alifika ofisi za halmashauri ya manispaa hiyo akitaka vyeti vyake vihakikiwe upya.

Mwalimu huyo alisema ameshangazwa na kitendo cha Serikali kutaja jina lake, wakati ana vyeti halisi.

“Nimeshangaa sana kuona jina langu kwenye ile orodha, lakini pamoja na hayo nimejaribu kusoma majina nimebaini kasoro nyingi kwa kuwa kuna sehemu jina moja limeandikwa mara mbili,” alisema.

“Nimefanya kazi kwa miaka 29 na ualimu ni sehemu ya maisha yangu na naitunza familia kwa kutegemea kazi hii,” aliiambia Mwananchi.

“Watumishi wengi sasa wanalalamikia huu utaratibu. Umefanya kazi kwa miaka 29 leo ufukuzwe kazi? Hii haiathiri mtumishi peke yake, bali hata maisha kwa ujumla,” alisema.

Hali katika ofisi za halmashauri hiyo ilionekana kuwa na pilikapilika, baadhi wakionekana kushika bahasha ndefu mithili ya watu waliobeba vyeti.

Wilayani Temeke kulikuwa na matangazo mawili yanayohusu watumishi waliotajwa katika orodha ya walioghushi vyeti, moja la Mei 2 likiwataka waliotajwa kikao kilichofanyika kwenye ukumbi wa Idd Nyundo na jingine la Mei 3 limeambatanishwa na majina ya watumishi 43 likiwataka kufika Baraza la Mitihani kabla ya Mei 15 wakiwa na vyeti vyao halisi vya elimu ya sekondari na taaluma ili kuondoa utata uliojitokeza wa majina yao kutumiwa na mtu zaidi ya mmoja.

Baadhi ya watumishi wa halmashauri hiyo waliokuwa eneo hilo walionekana kuwa na hofu.

“Kwa hali hii kweli hata kazi zenyewe zitafanyika kwa amani? Maana kila siku mambo mapya yanakuja unaweza ukashangaa kesho na wewe jina lako lipo, na uzee huu sijui unaishije,” alisema mtumishi mmoja akimwambia mwenzake.

Bungeni mjini Dodoma, mbunge wa viti maalumu (CCM), Taska Mbogo aliomba msaada kwa Serikali kupeleka watumishi mapema ili kukabiliana na upungufu wa watumishi 60.

Kuzorota kwa huduma kumeikumba pia Halmashauri ya Wilaya ya Chunya ambako wafanyakazi 19 wameonekana kuwa na tatizo na kati yao sita wanatoka idara ya afya.

Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Chunya, Sophia Kumbuli amesema utoaji huduma umeathirika kutokana na waliopo kuzidiwa kazi.

“Athari ni kubwa watumishi waliopo hawamudu utoaji huduma kutokana na uchache eneo husika, ila naendelea kufuatilia kwa ukaribu kuweza kukabiliana nao,” alisema.

Kauli hiyo inalingana na ya mkurugenzi wa Halmashauri ya Mbarali, Kivuma Msangi ambaye alisema baada ya watumishi 26 kutajwa, ameamua kukutana na waliosalia kupeana mikakati ya kuhakikisha wanakabiliana na tatizo hilo.

“Athari lazima ziwepo tu na hii ni nchi nzima kuna mtikisiko. Ninachokifanya kwa sasa nakaa na watumishi waliopo na kuwapa motisha ili kufanya kazi kulingana na mazingira yaliyopo kwa vile tumejijua kwamba tupo wachache,” alisema.

Madereva sita wahukumiwa

Wakati halmashauri zikikabiliana na tatizo la upungufu wa wafanyakazi, madereva sita wa Halmashauri ya Wilaya ya Kilwa mkoani Lindi wamehukumiwa kifungo cha nje cha mwaka mmoja baada ya kupatikana na hatia ya makosa matatu ya kughushi vyeti vya kidato cha nne na kujipatia ajira.

Hukumu hiyo imetolewa jana na Hakimu wa Mahakama ya Wilaya ya Kilwa, Gabriel Ngaeje baada ya kuridhishwa na ushahidi.

Madereva waliohukumiwa ni Juma Sungura, Issa Abdurahman, Abdul Chubi, Dactuce Joseph, Ahmad Selemani na Abdallah Kilolopera.

Baada ya Hakimu Ngaeje kuwauliza kama wana sababu zinazoweza kumshawishi asiwape adhabu kali, wote walisema wana familia zinazowategemea, hivyo iwapo watapewa adhabu kali kuna hatari kwamba watakosa matunzo.

Mwanasheria kutoka Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), Emmanuel Camilius aliiomba mahakama kutoa adhabu kali ili iwe fundisho kwao na kwa watu wengine wenye tabia za aina hiyo.

Hata hivyo, hakimu aliwahukumu kifungo cha nje cha miezi 12.

Imeandikwa na Jackline Masinde, Asna Kaniki, Haika Kimaro, Aurea Simtowe, Mwanja Ibadi na Godfrey Kahango

No comments: