Dar es Salaam. Serikali ya Nigeria imepata chanzo kingine cha kuendesha bajeti; fedha zilizotaifishwa kutoka kwa viongozi mafisadi, Shirika la Habari la Nigeria limeeleza.
Kwa mpango huo, asilimia 20 ya bajeti yake ya mwaka huu itatokana na fedha zilizotaifishwa kutoka kwa viongozi wala rushwa.
Nigeria inakadiria kukusanya na kutumia dola23 bilioni za Kimarekani kwa mwaka huu (sawa na takribani Sh50 trilioni za Kitanzania) na bajeti hiyo inatarajiwa kupitishwa wakati wowote.
Okoi Obono-Obla, ofisa maalumu mwandamizi msaidizi wa Rais Muhammadu Buhari anayehusika na masuala ya mashtaka, aliliambia Shirika la Habari la Nigeria (NAN) kuwa bajeti hiyo itagharimiwa na fedha ambazo serikali imetaifisha kutoka kwa viongozi wala rushwa.
Ingawa hakusema serikali imetaifisha kiasi gani, lakini asilimia 20 ya Sh50 trilioni ni takriban Sh10 trilioni.
Obono-Obla aliiambia NAN kuwa fedha hizo zitaanza kutumika mara baada ya kupitishwa na Bunge.
“Karibu asilimia 20 ya bajeti ya mwaka huu zitatokana na fedha zilizorejeshwa kutokana na harakati za hivi karibuni,” alisema Obono-Obla juzi.
Kaimu rais wa Nigeria, Profesa Yemi Osinbajo alipitisha bajeti ya dola 23 bilioni za Kimarekani (sawa na zaidi ya Sh50 trilioni za Kitanzania) Jumatatu baada ya kuchelewa kwa miezi kadhaa kutokana na hali ngumu ya kiuchumi.
Bajeti ya mwaka jana iliyopitishwa Mei, ilichelewa kusainiwa kwa miezi kadhaa kutokana na kutowepo makubaliano kati ya wabunge na Rais.
Hali hiyo iliyumbisha zaidi uchumi ambao ulishuka kwa mwaka wa pili mfululizo kutokana na kushuka kwa bei ya mafuta ambako kumesababisha kupungua kwa mapato ya Serikali, kudhooisha sarafu ya naira na kusababisha dola kuadimika.
Rais Muhammadu Buhari alianzisha mpango wa taifa wa kufufua uchumi, NERP, mwezi Aprili kuiwezesha Nigeria kukabiliana na kuporomoka kwa uchumi.
Pia, Desemba mwaka jana alianzisha sera ya kutaka wananchi kutaja mafisadi kuwezesha Serikali kurudisha fedha zilizoliwa na viongozi.
Hadi sasa, sera hiyo ya kupambana na rushwa imewezesha kupata tetesi 337 kutoka kwa watu 2,000 kutoka kitengo cha kupokea taarifa ambacho kimesambaa katika vikosi vyote vya usalama, kwa mujibu wa viongozi walioongea na NAN.
No comments:
Post a Comment