Advertisements

Thursday, June 8, 2017

MAASKOFU WALAANI KUBWA KWA UBONGO WA MTAKATIFU BOSCO

Askofu wa Jimbo Katoliki la Rulenge Ngara, Severine Niwemugizi alisema anachoamini ni kuwa, aliyeiba mabaki hayo atakuwa na kasoro kichwani.

By Kalunde Jamal, Mwananchi kjamal@mwananchi.co.tz


Dar es Salaam. Maaskofu wa Kanisa Katoliki Tanzania, wamelaani kuibwa mabaki ya ubongo wa Mtakatifu John Bosco wa Italia.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti na gazeti hili, walishangazwa iweje mtu mwenye akili timamu na nia thabiti ya kuhiji na kuomba baraka kutoka kwa watakatifu aibe mabaki hayo.

Kauli hiyo imetolewa baada ya mtu aliyejifanya hujaji kuiba kisanduku kilichokuwa na mabaki ya ubongo wa Mtakatifu John Bosco uliokuwa umehifadhiwa katika Kanisa la Casstelnuovo jijini Turin.

Kutokana na wizi huo, polisi wa Italia wameweka vizuizi katika mipaka kaskazini mwa nchi hiyo ili kumsaka mhusika.

Mtakatifu John Bosco aliyezaliwa Agosti 16, 1815 na kufariki dunia Januari 31, 1888 alikuwa padri wa Kanisa Katoliki na mwanzilishi wa Shirika la Mtakatifu Fransisko wa Sales (Salesian Congregation).

Gazeti la USA Today liliandika kuwa mwizi huyo aliingia katika Kanisa la Castelnuovo lililopo jirani na mji wa Turin Ijumaa iliyopita na kuiba mabaki ya ubongo huo.

Kwa kawaida waumini hufika kanisani hapo kusali mbele ya mabaki hayo ambayo huwekwa nyuma ya altare.

“Namuomba yeyote aliyeuchukua aurudishe haraka, bila masharti ili tuufunge ukurasa huu na tuendelee kuadhimisha kumbukumbu ya Don Bosco vizuri,” alisema Askofu Mkuu wa kanisa hilo, Cesare Nosiglia.

Askofu wa Jimbo Katoliki la Rulenge Ngara, Severine Niwemugizi alisema anachoamini ni kuwa, aliyeiba mabaki hayo atakuwa na kasoro kichwani.

Naye Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu Katoliki la Mwanza, Jude Thadeus Ruwa’ichi alisema waliofanya kitendo hicho inawezekana imani yao ni tofauti na waliokwenda kuhiji.

No comments: