Advertisements

Thursday, June 15, 2017

MADIWANI WA CHADEMA ARUSHA WAHOFIA KASI YA JPM

Meya wa Jiji la Arusha, Calist Lazaro

MADIWANI wa Halmashauri ya Jiji la Arusha, wamemsifu Rais Dk John Magufuli kwa maamuzi yake ya kuwachukulia hatua wale wote waliohusika katika kuiangamiza nchi na kuingia katika mikataba tata, iliyoingizia nchi hasara kubwa katika sekta ya madini.

Baraza la Madiwani la Jiji la Arusha linaloongozwa na Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) na madiwani hao, walisema kuwa iwapo Rais Dk Magufuli atakwenda kwa kasi hiyo ya kufanya vema katika uongozi wake kwa kuwachukulia hatua viongozi wanzake, walioiharibu nchi na kuingia mikataba mibovu, uwezekano wa upinzani kuwepo na kufanya vema mwaka 2020, utakuwa mgumu na wapinzani watakosa hoja.

Diwani wa Kata ya Kimandolu, Rayson Ngowi alisema kuwa Rais Magufuli amethubutu na amechukua maamuzi, ambayo yamewagusa wananchi na kuona ni jinsi gani nchi ilivyokuwa ikiliwa na wajanja wachache.

Ngowi alisema hatua aliyochukua ni sawa na kiongozi wa upinzania, kwani hilo na mengine mengi ambayo anachukua hatua kwa sasa ndio wapinzani walikuwa wakipiga kelele kila kukicha, lakini viongozi wakuu wa nchi waliopita, walikuwa hawachukui hatua hivyo anapaswa kupongezwa na kuungwa mkono kwa asilimia mia.

Alisema Rais Magufuli anachukua maamuzi bila ya kuangalia wenzake, waliomteua ndani ya chama chake cha CCM na pia haangalii rafiki wala ndugu, kwani ametanguliza maslahi ya nchi. Ngowi alisema kuwa Watanzania kwa muda mrefu, walikosa kiongozi shupavu na jemedari wa namna hiyo ambaye hamung’unyi maneno.

Alisema kasi yake inahatarisha uhai wa upinzani hapa nchini, kwani yote yanayotekelezwa kwa sasa ni vilio vya wapinzani miaka ya nyuma na sasa Rais Magufuli anayafanya tena kwa kasi ya hali ya juu.

“Nataka niseme kuwa kama kasi hii ikiendelea na kutekeleza yote bila ya kumwonea huruma mtu wala aibu, wapinzani katika uchaguzi ujao hatutakuwa na hoja za msingi za kuwaambia wananchi.

“Sasa mimi nitakwenda kwenye kata yangu nitasema nini, maana kwangu kila kitu kimewekwa sawa na serikali ya Rais Magufuli na vyote nilivyokuwa nikisema na kulalamika juu ya maendeleo katika kata yangu katika uchaguzi uliopita vyote vimetekelezwa kwa kishindo” alisema Diwani Ngowi.

Diwani Ngowi alisema yeye ni mpinzani mkongwe katika siasa za nchi hii, lakini hawezi kupinga kila kitu bila ya kusifu na kukosoa, kwani ndio sifa ya demokrasia hapa nchini na nchi zilizoendelea. Aliiwaasa wapinzani kote nchi, kubadilika na kwenda na wakati kwani kusifu sio dhambi.

Alisema kiongozi aliyepo madarakani akifanya vizuri, hatuna budi kumsifu na akifanya vibaya pia tunapaswa kumkosoa na kumwelekeza la kufanya na sio kumwacha tu ili aweze kutumbukia shimoni.

Ukiachilia mbali siasa, Diwani Ngowi ambaye ni mchungaji wa madhehebu ya kilokole, ametoa ombi kwa Rais kufumua mikataba yote ya madini na gesi, kwani baadhi ya viongozi waliopita, walifanya hivyo kwa maslahi yao na sio ya Watanzania.

Diwani Ngowi pia alidai kinga kwa marais iondolewe ili watawala wawe na nidhamu na rasilimali za nchi, vinginevyo itakuwa kazi bure kwani watafanya uzembe kwa kujua hawatashitakiwa.

Diwani Amani Riwad wa Kata ya Engutoto jijini Arusha, alimsifu Rais kwa hatua anazochukua na kumtaka kuchukua hatua zadi kwa wale wengine, walioingizia nchi hasara kwa kuingia mikataba mibovu ambayo imetoa mwanya kwa wawekezaji kuiba rasilimali za nchi.

Riwad alisema kazi anayofanya Rais, inapaswa kupongezwa kwa nguvu zote na kila Mtanzania mpenda maendeleo na kilio hicho kilikuwa ni kilio cha wapinzani siku zote, lakini sasa kimepata kiongozi ambaye ni Rais Magufuli ambaye hana woga na huruma, kwa yule mwenye kucheza na mali za nchi.

Alisema na kumshauri Rais kutaifisha fedha na mali zote walizochuma, wale wote walioingizia nchi hasara ili iwe fundisho kwa wengine kuwa ili wawe waoga na mali za umma. Diwani wa Chadema Kata ya Ngarenaro, Isaya Doita alisema alichofanya Rais kwa kutekeleza ripoti mbili za madini ni jambo jema na ni mawazo mazuri, yanapaswa kupongezwa bila ya kificho.

Doita alisema iwapo suala hilo, litakuwa na umaliziaji mzuri, nchi hii itakuwa na kiongozi na jabari na shupavu, aliyekosekana miaka mingi na anastahili kupongezwa kwa namna yoyote ile. “Nina hofu kubwa katika umaliziaji wa suala hili kwani tumezoea kuona na kusikia matamshi mengi, lakini umaliziaji wake unakuwa mgumu au mbaya na wa kusuasua, sasa hilo sitaki nilione kwa Rais Dk Magufuli,” alisema Doita.

Akizungumzia upinzani katika uchaguzi ujao, Doita alisema kuwa upinzani utakuwepo na utaimarika na utaendelea kuleta changamoto kwa serikali ya chama kilichopo madarakani, kwani hoja zingine nyingi za ufisadi zitaibuliwa. Doita alisema kuwa kwa sasa Rais Magufuli ameimarisha upinzani kwa asilimia kubwa, kwani yote yanayotekelezwa kwa sasa ni hoja za wapinzani na upinzani hautakufa.

HABARI LEO


No comments: