Advertisements

Thursday, June 1, 2017

Majaliwa alivyopangua maswali ya papo kwa papo bungeni



Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa
By Julius Mnganga, Mwananchi jmathias@mwananchi.co.tz

Dodoma. Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amejibu maswali mbalimbali ya papo kwa papo bungeni leo Alhamisi ikiwemo suala la madini ambapo amewataka wawekezaji wa madini nchini kuondoa hofu ya kukosa haki zao kwani kamati ya pili iliyoagizwa kufanya uchunguzi kuhusu mchanga wa madini (makinikia) bado haijakamilisha kazi yake.

Waziri Mkuu amesema hayo wakati akijibu swali la Mbunge wa Tabora Mjini(CCM), Emmanuel Mwakasaka lililohoji kuhusu taswira ya Tanzania kimataifa hasa katika uwekezaji wa madini.

Majaliwa amewataka wawekezaji wa madini kuondoa hofu kwa kuwa kamati ya pili iliyoundwa kuangalia athari za kisheria, kisiasa na kimataifa kuhusu sakata la mchanga wa madini bado haijatoa ripoti yake.

“Watanzania wengi walikuwa na hofu, hata wabunge wengi katika serikali hii ya awamu ya tano mmekuwa mkizungumzia sakata la mchanga wa madini, lakini niwatoe hofu, Rais John Magufuli alifanya hayo kwa nia njema ya kulinda rasilimali za Taifa,” amesema

Majaliwa pia amesema Serikali ikishindwa kujenga mitambo ya kuchenjua makinikia basi itakaribisha wawekezaji wa kufanikisha mchakato huo.

"Lengo la zuio hili ni Serikali kujiridhisha juu ya wasiwasi wa wananchi mkiwamo wabunge ambao mmekuwa amkiuliza maswali mengi. Baada ya uhakiki huu na ushauri wa wataalamu tutaona kama Serikali inaweza kujenga mitambo hiyo kwenye maeneo yanayotoa mchanga huo kwa wingi. Ikishindwa, tutakaribisha wawekezaji," amesema Majaliwa na kuwataka wananchi kuiunga mkono Serikali katika mchakato huo.

"Wawekezaji wote wa madini wawe watulivu kwani haki zao zitalindwa," amesema Waziri Mkuu.

Katika maswali hayo Majaliwea vilevile amewaambia watumishi wa Serikali watakaobainika kushiriki kwenye udanganyifu uliofanywa na mawakala wa pembejeo watachukuliwa hatua za kinidhamu na kisheria.

Majaliwa amesema hayo alipokuwa akijibu swali la Mbunge wa Viti Maalum(Chadema), Devotha Minja kuhusu malipo ya mawakala waliotoa pembejeo hizo ili kuimarisha kilimo nchini.

"Tumegundua uwapo wa udanganyifu kwenye taarifa za mawakala. Kwa kushirikiana na wenyeviti wa vijiji, waliorodhesha majina ya wakulima walionufaika ambao hawapo. Nilitoa muda wa uchunguzi ambao umekamilika jana. Kuanzia leo nitakuwa napokea ripoti kutoka mikoani watakaobainika kushiriki tutawachukulia hatua," amesema Majaliwa.

Mawakala hao ambao walitoa huduma hiyo tangu mwaka 2014 wataanza kulipwa muda wowote baada ya Waziri Mkuu kupokea ripoti ya utekelezaji.

No comments: