ANGALIA LIVE NEWS

Wednesday, June 7, 2017

RC MGHWIRA: SIACHII UENYEKITI ACT

Na ELIZABETH HOMBO-DAR ES SALAAM

MKUU wa Mkoa wa Kilimanjaro, Anna Mghwira amesema hana mpango wa kuachia nafasi yake ya uenyekiti wa Chama cha ACT-Wazalendo.

Mghwira alitoa msimamo huo baada ya kuapishwa kushika wadhifa huo na Rais Dk. John Magufuli Ikulu, Dar es Salaam jana.

Alisema kwa sasa anachokiangalia ni kusimamia shughuli za maendeleo kwa faida ya Watanzania.

Juni 3, mwaka huu, Rais Dk. Magufuli alimteua Mghwira kuwa Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, uteuzi ambao ulizua maswali na mshtuko mkubwa katika tasnia ya siasa.

Mjadala mkubwa uliibuka kutokana na cheo alichopewa, kuwa ni tofauti na kile cha ubunge, huku wengine wakienda mbali zaidi huenda kuna usaliti.

Mghwira ambaye katika uchaguzi mkuu wa mwaka juzi, aligombea urais kupitia ACT- Wazalendo, sasa atalazimika kusimamia utekelezaji wa ilani ya CCM.


Mbali na hilo, pia atabeba jukumu la kuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa.

MGHWIRA

Akizungumza na MTANZANIA jana, Mghwira alieleza kushangazwa na namna watu wanavyohoji endapo ataachia uenyekiti wa ACT-Wazalendo, wakati kuna mambo ya msingi.

“Sasa unataka niseme nini wakati leo (jana) ndio nimeapishwa? Hakuna vitu vya msingi vya kuhoji? Mimi sitazami hizo nafasi.

“Mimi ni mwenyekiti wa chama na kama unakumbuka wakati Magufuli aliposhinda urais, nilimkabidhi ilani ya chama chetu na hata leo (jana) wakati ananikabidhi ya CCM nilimkumbusha kuwa hata mimi nilimpatia ya ACT akasema kweli anayo.

“Lakini kwani tatizo liko wapi? Mbona Mbowe (Freeman) ni Mbunge wa Hai halafu ni Mwenyekiti wa Chadema sasa tatizo liko wapi kwangu?” alihoji.

Alipoelezwa na mwandishi kuwa upo utofauti wake na Mbowe kwa kuwa yeye anakwenda kutekeleza ilani ya CCM, alisema. “Bungeni wanatekeleza ilani ya chama gani? Waziri Mkuu na wengine wote wanatekeleza ilani ya chama gani?

“Nikwambie tu, wengine ni maneno tu hawasomi hata hii ilani ya CCM na kwamba ilani yao si mbaya kinachotakiwa ni utekelezaji tu,”alisema.

Alisema chama chochote kinapoingia madarakani hakuna mbadala zaidi ya kutekeleza ilani yake.

“Mara nyingi tumekuwa tukilalamika ooh tunaonewa, tukipewa huo uhuru tena tukatae? Tujikite kwenye masuala ya msingi,”alisema Mghwira.

Kuhusu kipaumbele chake katika Mkoa wa Kilimanjaro, alisema ataanzia pale alipoishia Said Meck Sadick na kwamba ataripoti eneo lake la kazi ndani ya wiki hii.

Alipoulizwa endapo kabla ya kuapishwa amekutana na viongozi wa chama chake, alisema. “Jana tumeongea sana na viongozi wangu na leo (jana) tutaonana,” alisema.

JPM

Akizungumza baada ya kumwapisha Mghwira, Rais Dk. Magufuli alisema hateui watu ovyo ovyo hususani wale wanaopiga piga kelele, bali anateua wanaopenda kuwatumikia Watanzania kwa moyo.

“Nampongeza mama Anna, ni mstaarabu very focused, najua katika nafasi niliyomteua atafanya kazi vizuri kwa sababu ni mpenda maendeleo.

“Mimi nikikuteua, nikakupeleka mahali najua utafanya kazi kwa niaba ya Watanzania na hicho ndicho tunachokihitaji. Maendeleo hayana chama, kabila, dini kila mtu anahitaji maendeleo.

“Wapo wanaosema mbona nilishazungumza sitateua wapinzani, ni lazima watu waelewe kuwa nilizungumza hilo mahali gani. Nilizungumza nikiwa Zanzibar,” alisema Rais Magufuli.

Kuhusu uteuzi wa nafasi kumi za wabunge, alisema msimamo wake uko pale pale na kwamba hatateua wapinzani.

“Msimamo uko pale pale wa kutoteua upinzani katika nafasi kumi ya ubunge, sasa hivi nimeshateua tisa, bado moja na hiyo haitakuwa ya upinzani kwa sababu huwezi kumpeleka mtu bungeni halafu anakusema na huna mamlaka ya kumtoa.

“Mimi nawateua katika nafasi hizi kwa sababu nina mamlaka ya kuwatoa wakati wowote. Wapo watu wao kila kitu ni kupinga tu,

“Wanapopinga tuna information zao nyingi, saa nyingine tunawahifadhi tu. Wengine wanahangaika kutafuta data especially kwenye madini, anahangaika wee anatuma sms kwa wale anaowatafutia ‘data’ eti nitashtakiwa!

“Wewe ukishakuwa mwanasheria unaogopa kushtakiwa. Ngoja nitasema siku nitakapopokea ile ripoti.

“Najua utasemwa, wengine wanakuonea wivu wapo watakaokuonea wivu kutoka kwenye chama chako, waliokuwa CCM wakitaka niteue tu CCM.

“Wapo watakaokuonea wivu hata wa Chadema kwa sababu sikuwateua pamoja na kwamba wapo wengi wananiombaomba mpaka wabunge lakini nimesema hapana nataka upinzani uwepo.

“Una uwezo wa kuwaweka watu ndani saa 48. Kwa ‘power’ hii niliyokupa leo na bahati mbaya mtu akija kukusema katika mkoa wako shughulika naye. Yeyote atakayekubeza kasimama naye, kwa sababu sasa una ‘power’.

“Wengine wanasema mbona Kamati ya CCM inasema mjumbe ni Mkuu wa Mkoa kwani kuna ubaya? Kwani wewe huhitaji barabara? Kwani utashi wako nani anazuia ukiamua kwenda CCM?

“Kasimamie utashi wako, nina raha sana nilipokuteua sikukuuliza, ulikuwa na uwezo wa kukataa na bahati mbaya hata namba yako ya simu siijui. Nafahamu wengine wamenuna kweli waache wanune wewe ukawatumikie Watanzania,”alisema Rais Magufuli.
MTANZANIA

No comments: