Advertisements

Friday, June 30, 2017

Safari za treni Dar zasitishwa baada ya mabehewa kuacha njia

Treni inayofanya safari zake kati ya Ubungo na Stesheni maarufu ‘Mwakyembe’ imepata ajali eneo la Mabibo Magengeni baada ya mabehewa matano kuacha njia na kusababisha taharuki kwa abiria waliokuwemo ndani.
Akizungumza na Mwananchi leo (Ijumaa Juni 30) Ofisa Mawasiliano wa Kampuni ya Reli Tanzania (TRL), Midlady Maize amesema ajali hiyo ilitokea saa 12.30 asubuhi wakati ikitokea Ubungo Maziwa kuelekea Stesheni, Posta.
Amesema mabehewa ya nyuma yaliacha njia na kusababisha taharuki kwa abiria.
Hata hivyo amesema hakuna aliyejeruhiwa na abiria hao walihamishiwa kwenye mabehewa ya mbele na waliendelea na safari zao.
Amesema mafundi wanaendelea na taratibu za kuondoa mataruma yaliyopata hitilafu ili baadaye treni iendelee na safari zake.
“Sasa hivi ukarabati unaendelea eneo la tukio hivyo tunatarajia baadaye safari zitaendelea kama kawaida na imeundwa kamati ambayo itatoa ripoti baada ya wiki mbili kuhusu nini kimesababisha kutokea ajali hiyo,” amesema Maize.
Mhandisi wa Mitambo wa TRL, Shija Isanga amesema tatizo reli hiyo imechakaa na hivyo wataalamu wa ujenzi wanaendelea na ukarabati ili kuhakikisha safari zinarejea kama awali.
“Tunajitahidi kurekebisha sehemu yenye hitilafu ili safari za treni ziendelee kama kawaida,”alisema Isanga.

No comments: