ANGALIA LIVE NEWS

Tuesday, June 6, 2017

Upinzani nchini wawekwa njiapanda

By Peter Elias, Mwananchi pelias@mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Mgogoro wa uongozi ndani ya CUF, wabunge wa upinzani kudhibitiwa bungeni, kuzuiwa kwa mikutano ya vyama vya siasa na hata uteuzi wa viongozi wa vyama vya upinzani serikalini ni baadhi ya mambo ambayo yameuweka upinzani njiapanda.

Licha ya vyama vya upinzani kulalamika mara kwa mara kuwa havitendewi haki na kushirikishwa, suala la uteuzi wa viongozi wa upinzani kushika nyadhifa serikalini unawaweka njiapanda zaidi.

Huku nje ya bunge hali ikiwa hivyo, wapinzani wamekuwa wakilalamikia kuwa hata ndani ya bunge wanadhibitiwa.

Spika wa Bunge, Job Ndugai mara kadhaa amewatoa nje wabunge wa upinzani ama kwa pamoja au mmoja mmoja na wakati mwingine huagiza kamati ya maadili kuwahoji wahusika na kuwachukulia hatua.

Tukio la hivi karibuni ni la mwishoni mwa wiki wakati Ndugai alipoagiza askari kumtoa nje kwa nguvu mbunge wa Kibamba (Chadema), John Mnyika kwa madai ya kukidharau kiti cha spika. Spika amemsimamisha Mnyika kutohudhuria vikao vya bunge kwa siku saba.

Hiyo haikuwa mara ya kwanza. Mara kadhaa kiti cha spika kimeagiza wapinzani kutolewa nje au kusimamishwa vikao au mikutano kadhaa, na jana wabunge wawili wa Chadema, Ester Bulaya na Halima Mdee walisimamishwa mpaka Bunge la bajeti mwakani.

Hata hivyo Chadema, CUF na ACT Wazalendo vimekuwa vikitikiswa kwa staili tofauti.

ACT Wazalendo imepoteza viongozi wake muhimu ndani ya mwaka mmoja kutokana na sababu mbalimbali ikiwamo baadhi yao kuteuliwa kuitumikia Serikali.

Wiki iliyopita, Rais Magufuli alimteua mwenyekiti wa ACT Wazalendo, Anna Mghwira kuwa mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro.

Kabla ya uteuzi huo, Aprili 4, Rais alimteua aliyekuwa mshauri wa chama hicho, Profesa Kitila Mkumbo kuwa katibu mkuu wa Wizara ya Maji na Umwagiliaji. Baada ya uteuzi huo Profesa Mkumbo alitangaza kujiuzulu nafasi zake zote ndani ya ACT Wazalendo.

Chama hicho pia kilimpoteza mwanasheria na mshauri wake, Albert Msando ambaye alijiuzulu mwenyewe kwa sababu ya kusambaa kwa video yake iliyokuwa inakwenda kinyume na maadili.

Kadhalika, Aprili 21, 2016 aliyekuwa katibu mkuu wa kwanza wa chama hicho, Samson Mwigamba alitangaza kujiuzulu nafasi hiyo kwa sababu aliyosema kuwa ni kupata muda wa masomo yake ya shahada ya uzamili nchini Kenya.

Kuthibitisha hilo, kiongozi wa ACT Wazalendo, Zitto Kabwe juzi aliliambia Mwananchi kuwa sasa anahitaji utulivu mkubwa.

“Kwa sasa nahitaji utulivu kuliko wakati wowote. Nipeni muda,” alisema Zitto alipoulizwa msimamo wake kuhusu uteuzi wa Mama Mghwira.

Wakati chama hicho kikiondokewa na viongozi wake muhimu, CUF ipo kwenye mgogoro wa ndani baada ya Profesa Ibrahim Lipumba ambaye alijiuzulu uenyekiti Agosti 6, 2015 kutangaza kurudi katika nafasi hiyo.

Lipumba alibatilisha barua ya kujiuzulu baada ya kukaa nje ya chama hicho kwa mwaka mmoja, lakini mkutano mkuu wa CUF ukabariki kujiuzulu kwake Agosti 21 mwaka huu.

Mgogoro huo umeongezeka zaidi baada ya msajili wa vyama vya siasa nchini, Jaji Francis Mutungi kutangaza kumtambua Profesa Lipumba kama mwenyekiti wa chama hicho licha ya kuwapo kwa sintofahamu ya kujiuzulu kwake.

Mpasuko ndani ya chama hicho una pande mbili ambazo ni ule unaomuunga mkono katibu mkuu, Maalim Seif Sharif Hamad na ule wa Profesa Lipumba. Pande hizo zimefikishana mahakamani na kesi bado inaendelea.

Mgogoro wa CUF umefika mbali zaidi baada ya viongozi wake kuamua kugawana majengo ya ofisi. Wakati ofisi za CUF upande wa Tanzania Bara zikidhibitiwa na wafuasi wa Profesa Lipumba, ofisi za Zanzibar zinadhibitiwa na upande wa Maalim Seif.

Viongozi hao wakuu wanafanya uamuzi tofauti bila kushirikishana na Maalim Seif alitangaza kuwafukuza baadhi ya viongozi wa chama hicho, lakini Profesa Lipumba alitangaza kuwarudisha.

Lakini si vyama hivyo tu vinapitia kwenye changamoto hizo.

Kwa upande wa Chadema, shughuli zake nyingi zimepata changamoto zinazotofautiana.

Septemba Mosi mwaka jana, chama hicho kilikuwa na mpango wa kuendesha operesheni yake iliyoitwa kupinga udikteta nchini (Ukuta) , lakini ilizuiwa na polisi.

Kabla ya uchaguzi mkuu wa 2015, chama hicho kiliendesha operesheni zake kadhaa nchi nzima na kufanya mikutano ya hadhara sehemu mbalimbali bila kuzuiwa.

Miongoni mwa operesheni ambazo chama hicho kimewahi kufanya ni Operesheni Sangara na Movement For Change (M4C).

Kama ilivyo kwa vyama vingine, Chadema imeshindwa kufanya mikutano ya hadhara kwani serikali ilipiga marufuku mikutano yote ya kisiasa ya hadhara mpaka mwaka 2020 isipokuwa kwa wabunge walioshinda uchaguzi ambao wameruhusiwa kufanya mikutano kwenye majimbo yao tu.

Ugumu huo unapunguza nguvu ya ushindani kwa vyama vya upinzani kukikabili chama tawala.

Changamoto hizo hazijaishia kwa vyama vya upinzani tu, kwani hata viongozi wao wameguswa.

Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe kuhusishwa katika sakata la dawa za kulevya linatajwa kama ni mkakati wa kisiasa.

Pia kukamatwa kwa wabunge wakiwamo wa chama hicho kama Tundu Lissu, Godbless Lema na Peter Lijualikali ni jambo ambalo lilizua mjadala mkubwa nchini.

Wanavyosema wadau wa siasa

Akizungumzia hali ya kisiasa nchini na madai ya kudhibitiwa kwa upinzani bungeni, mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Dk Benson Bana alisema baada ya kuanzishwa kwa vyama vya siasa nchini, sheria na kanuni zilitungwa kwa ajili ya kusimamia uendeshaji wake.

Alisema wabunge wanatakiwa kuheshimu kanuni walizojiwekea wenyewe na spika naye aongoze kiti chake kwa kufuata kanuni za Bunge ili kuondoa sintofahamu inayotafsiriwa kama kuwadhibiti wapinzani.

“Kiti cha Spika kiheshimiwe na wabunge wote, lakini naye afuate kanuni na taratibu za Bunge katika kufanya maamuzi. Kila mbunge akijali maslahi ya wananchi wake, yanayotokea bungeni hatuwezi kuyaona tena,” alisema Dk Bana.

Kuhusu uteuzi wa Mghwira kuwa mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Dk Bana alisema Rais amepewa mamlaka ya kumteua mtu yeyote anayeona anafaa kufanya kazi katika sehemu husika, hivyo haoni tatizo na kwamba hauwezi kuua upinzani.

“Tatizo la wapinzani hapa Tanzania hawana ajenda, wanatakiwa kuanza kujiandaa kwa ajili ya uchaguzi wa mwaka 2020. Chama cha siasa hakiwezi kufifishwa kwa mtu fulani kuteuliwa kuwa mkuu wa mkoa. Haiwezekani,” alisema.

Akiwa na mtazamo tofauti na huo, mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dodoma (Udom), Innocent Tarimo alisema imezoeleka kwamba kila wanachofanya wapinzani ni lazima kitakuwa kibaya hata kama wanasimamia mambo ya msingi kwa nchi yao.

Alisema kiti cha spika kimekosa subira ya kuwasikiliza wapinzani kabla ya kuchukua hatua kali ambazo haziwaumizi wabunge wa upinzani pekee, bali pia zinawakosesha wananchi uwakilishi katika Bunge hilo.

“Kanuni za Bunge zipo, lakini hazifuatwi na viongozi wa Bunge, hicho ndicho kikwazo kikubwa. Wakati mwingine wapinzani wanakosea, lakini pia wakati mwingine kiti cha spika nacho kinafanya makosa kwa kutofuata kanuni za Bunge,” alisema Tarimo.

Mhadhiri wa Chuo Kikuu Huria cha Tanzania (OUT), Hamad Salim alisema upinzani una kazi kubwa ya kuwashawishi Watanzania kwa kujipambanua kuwa tofauti na chama tawala (CCM).

Alisema bahati mbaya vyama vyote vya upinzani vinafanana huku vikishindwa kufanya siasa za mabadiliko, badala yake vinatumia nguvu nyingi kufanya maandamano na kukosoa hata mambo ambayo awali walikuwa wakitaka yafanyike.

Juzi, Profesa wa Chuo Kikuu cha Katoliki Iringa (Rucu), Gaudence Mpangala alisema si vyama vyote vya upinzani ni wapinzani kweli.

Alisema vyama vingine vilianzishwa kimkakati kwa ajili ya kudhoofisha upinzani nchini.

No comments: