ANGALIA LIVE NEWS

Friday, June 16, 2017

Vijiji vitano vyaidai Acacia bilioni 53/-

Sehemu ya Mgodi wa North Mara
MABARAZA matano ya vijiji wilaya ya Tarime mkoani Mara, yamefungua kesi ya kibiashara katika Mahakama ya Kuu Kanda ya Mwanza, dhidi ya Mgodi wa Dhahabu wa North Mara, unaoendeshwa na Kampuni ya Acacia wakidai Sh bilioni 53 za mrahaba kutokana na mauzo ya madini.

Katika shauri hilo, Mabaraza ya yaliyofungua kesi hiyo ni ya vijiji vya Nyamwaga, Kerende, Kewanja, Nyangoto na Genkuru vilivyoko wilayani Tarime mkoani humo. Wameungana na kudai kampuni ya North Mara Gold Mine Limited (East Africa Gold Mines Limited) kuwalipa Dola za Marekani 26,786,250.30 kuanzia Julai 2002 hadi Desemba 2011, pamoja na riba ya asilimia 21 kwa viwango vya benki za baishara kuanzia Januari 2012 hadi tarehe ya hukumu.

Shauri hilo limepangwa kusikilizwa Juni 27 mwaka huu mbele ya Jaji Sirilius Matupa. Inadaiwa kuwa kati ya Agosti 24 na Septemba 8, mwaka 1995, vijiji hivyo na kampuni ya East Africa Gold Mines Limited, waliingia katika makubaliano ambapo wadai hao walitoa leseni za kutafuta madini kwa kampuni hiyo.

Kinyume cha matarajio, kwa mujibu wa wakili wa wadai hao, Joseph Rutabingwa, miongoni mwa mambo ya kuzingatia waliyokubaliana wafanyike, mdaiwa alishindwa kurejesha kwa jamii kiwango sawa na thamani ya asilimia moja ya dhahabu zote zilizozalishwa kwa hesabu walizokubaliana.

Kwa mujibu wa makubaliano, malipo hayo yalikuwa yalipwe taslimu kwa kila robo ya mwaka (miezi mitatu) tangu siku ya makubaliano. Uzalishaji wa madini kuanzia mwaka 2002 hadi Desemba mwaka 2011 ulipaswa kuwa wakia (ounces) 2,114,701.

Ilidaiwa kuwa uzalishaji huo unahusishwa kufanywa na wakala aliyeteuliwa kwa kazi hiyo aliyetajwa kuwa ni M/S KPMG na anatambulika. “Ilivyochanganuliwa kwa mujibu wa thamani ya Dola 1,290 (kipindi hicho) kwa wakia, thamani halisi kwa mdai kwa ile asilimia moja ilikuwa Dola za Kimarekani 27,279,655.80 ,” ilieleza sehemu ya mdai hayo.

Aidha katika kipindi hicho, mdaiwa alilipa kwa mdai jumla ya Dola za Marekani 493,405.50 na kuacha deni la Dola za Marekani 26,786,250.30, ambazo wadai wanazidai kwa kampuni hiyo. Juni 2, 2014, kwa mujibu wa ripoti ya awali ya mkaguzi wa hesabu M/S KPMG, mdaiwa alikuwa na hati ya madai ya malalamiko na tishio la kushtakiwa, lakini hakuna mwitikio wowote uliochukuliwa.

Imeelezwa katika utetezi kuwa kuwa kampuni hiyo imefanya kazi zake katika maeneo makuu matatu ambayo ni Gokona, Nyabirama na Nyabigena na ilikubalika kuwa, hesabu zitafanyika kwa kuzingatia uzalishaji wa dhahabu na uuzaji kutoka Nyabigena pekee na si maeneo yote matatu kama ilivyoelezwa na wadai (vijiji).

Kwa mujibu wa mdaiwa, takwimu zilizopo zinaonesha kuwa uzalishaji katika Nyabigena ulifanyika mwaka 2005 na kuisha mwaka 2010. Aidha, taarifa ya uzalishaji inaonesha kuwa, jumla ya dhahabu iliyozalishwa ni wakia 685,382 na iliyouzwa ni ni wakia 318,027.

Aidha ilielezwa pia kuwa, pamoja na kuacha uzalishaji huo wa eneo moja la Nyabigena kutokana na maombi ya viongozi wa kijiji, kampuni ililipa kwa vijiji hivyo Dola za Marekani 493,405.25.

HABARI LEO

No comments: