ANGALIA LIVE NEWS

Tuesday, July 4, 2017

TRL Yavikataa vichwa vya treni Vilivyo Bandarini

Vichwa viwili kati ya 13 vya treni vilivyonunuliwa na TRL ambavyo vilipokelewa katika Bandari ya Dar es Salaam Machi 21, 2015. Vichwa hivyo vimetengenezwa nchini Afrika Kusini. Picha na Maktaba 

Wakati Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano ikitaka taarifa kutoka Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari (TPA) na Mamlaka ya Mapato (TRA) kuhusu vichwa vya treni vilivyoingizwa nchini, ununuzi wa vichwa hivyo umegubikwa na utata.
Utata huo unatokana na ukweli kwamba Shirika la Reli Tanzania (TRL), lilinunua vichwa hivyo kupitia mkataba kati yake na kampuni ya EMD ya Marekani na utengenezaji wake ukafanywa na kampuni ya DCD ya Afrika Kusini.
Juzi, wakati akizindua mradi wa uboreshaji wa Bandari ya Dar es Salaam, Rais John Magufuli amesema kuna vichwa vya treni vilishushwa katika bandari hiyo lakini mmiliki wake hajulikani, akisisitiza kwamba kuna mchezo mchafu umefanyika.
Hata hivyo, Mkurugenzi Mkuu wa TPA, Mhandisi Deusdedit Kakoko aliweka bayana kwamba vichwa hivyo vina nembo ya TRL na kwamba ulitokea mgogoro kati ya shirika hilo na kampuni iliyotengeneza vichwa hivyo baada ya kubainika kuwa mchakato wake wa ununuzi haukuwa sahihi.
Taarifa hiyo ilifafanua kwamba ununuzi huo umegharimu Sh70.5 bilioni ambazo zote zilishalipwa. “Mradi huu wa ununuzi wa vichwa 13 vipya vya treni ni sehemu tu ya mpango kabambe wa Serikali wa kuifufua na kuiimarisha TRL chini ya mpango wa Matokeo Makubwa Sasa (BRN),” inasomeka sehemu ya taarifa hiyo iliyotolewa kwa vyombo vya habari.
Alipoulizwa kuhusu vichwa hivyo, Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Mhandisi Edwin Ngonyani amesema wizara haikuwa na taarifa juu ya ujio wake na kwamba taarifa ya Rais ni sahihi.
Ngonyani amesema wizara imeziagiza TRA na TPA kuandaa taarifa kuhusu vichwa hivyo vilivyoshushwa bandarini bila wamiliki wake kutambulika na pia wameviagiza vyombo vya ulinzi na usalama kufanya uchunguzi juu ya suala hilo.

Chanzo: Mwananchi

No comments: