Advertisements

Wednesday, August 16, 2017

MKEO SIKUMWITA, ALIKOSEA MLANGO

MKEO SIKUMWITA
VYOMBO vimetupwa nje na baba mwenye nyumba. Si kwamba eti sijalipakodi, la hasha! Ni sababu ndogo ya kipuuzi imepelekea yote haya.

Saa nane usiku nikiwa nimelala katika kitanda changu cha kunesa, mke wa baba mwenye nyumba alitoka ndani na kuelekea msalani ili kushughulika na haja ndogo. Wakati anarudi chumbani kwake, kwa sababu ya usingizi mzito aliokuwa nao, akakosea mlango, badala ya kuingia katika chumba chake, akaingia chumbani kwangu. Kumbe nilisahau kufunga mlango! Ukawa mwanzo wa matatizo.

Alipoingia nini kilitokea?

Hakikutokea chochote. Nilikuwa naelea katika bahari ya usingizi kwa sababu ya uchovu wa shughuli za kutwa nzima. Hata ujio wake sikuutambua.


Yeye alipongia, kwa sababu ya kuzidiwa na usingizi kama nilivyosema awali, hakugundua tofauti ya chumba changu na cha mumewe. Akajilaza kama mzigo. Tukalala bila kutambuana.
Chumbani kwa mumewe

Mumewe ambaye ndiye baba mwenye nyumba, alishtuka saa tisa usiku. Akapapasa kitanda kizima asimuone mkewe.

Mzee huyu hana mchezo kwa mkewe. Akaendesha msako mkali baada ya kumsubiri mama watoto wake kwa dakika 15. Alianzia chooni. Hakumkuta. Akazunguka kila kona aliyohisi angempata. Lakini kona zote hizo hakumwona.

Ikawaje?
Alianza kuamsha wapangaji wote ‘mabachela’. Kila aliyemfungulia mlango alimwomba atazame ndani kwake kujihakikishia kama mkewe hakuwamo. Alikagua vyumba vitatu bila mafanikio, kikabaki kimoja. Chumba changu!

Alipofika katika mlango wangu, hakubisha hodi. Aligundua mlango ule uliegeshwa. Hamu ya kutaka kujua kilichoendelea ndani ikamvaa.
Alifungua taratibu bila kelele. Kwa sababu sikuzima taa, palikuwa peupe,akajionea kila kitu.

Alipotazama kitandani akatoa sauti ya uchungu: “Fumaniziiii”

Mimi na mke wake tukashtuka toka usingizini. Tukatazamana, nikamuuliza, “Umefikaje kitandani kwangu?” akanikodolea macho akiniuliza, “Nimefikaje hapa!”

Baba mwenye nyumba akafoka: “Msinifanyie maigizo, leo mtanitambua!”

Kabla hajafanya kitu kibaya, majirani wakaingia. Wakajitahidi kutuliza hali ya hewa, pakawa shwari kidogo.

Mke wa baba mwenye nyumba alijaribu kueleza hali i livyokuwa, naminikaeleza ukweli wangu. Hakuna aliyeamini. Nilijitetea mpaka asubuhi, nikaishia kupuuzwa.
Namaliza kama nilivyoanza, vyombo vimetupwa nje na baba mwenye nyumba. Lakini mzee amini usiamini, mkeo sikumwita, alikosea mlango.

GPL

1 comment:

Anonymous said...

Wewe ulikuwa unaweka mtego kuacha mlango wazi halafu taa zinawaka huyo mama mwenye nyumba asione kweli wewe sio mumewe na chumba kiko tofauti?