ANGALIA LIVE NEWS

Friday, August 11, 2017

Uchaguzi Kenya: IEBC yajibu malalamiko ya kina Raila Odinga

Tume ya Huru ya Uchaguzi na Mipaka nchini Kenya (IEBC) imejibu malalamiko ya kasoro za uchaguzi yaliyotolewa na muungano wa Nasa, hasa kura za urais.
Barua ya IEBC iliyoandikwa na mwenyekiti wake, Wafula Chebukati pia inabainisha makosa ya kitakwimu kuwa hawakujumuisha kura za wafungwa na diaspora na wamewahisha madai ya kutaka ushindi wakati IEBC haijapokea matokeo yote ya kura za urais.
Chebukati katika barua yake kwa mwanasheria wa Nasa, James Orengo alibainisha kuwa wakati IEBC inapokea malalamiko ya Nasa Agosti 9, tume ilikuwa imepokea fomu 131 kati ya majimbo 290 za matokeo ya kura za urais namba 34B, ikimaanisha kwamba kazi ya utumaji wa fomu hizo kwa ajili ya kulinganisha usahihi wa matokeo ilikuwa haijakamilika.
Pia, Chebukati alibainisha kuwa nyaraka iliyowasilishwa kwao na Nasa ikidai idadi ya wapiga kura waliosajiliwa ni 19,601,502 si ya kweli kwani idadi sahihi ni 19,611,423.
Chebukati pamoja na kubainisha baadhi ya makosa ya kitakwimu kwenye barua ya Nasa ambayo ilitangazwa hadharani jana na Musalia Mudavadi, pia alisema madai yao yana kasoro nyingi za kisheria.
Pia, alibainisha kuwa nyaraka waliowasilisha Nasa kwamba ndiyo sahihi iliyopo kwenye kompyuta za IEBC siyo ya kweli, kwa kuwa imetolewa kwenye mfumo mwingine wa kompyuta tofauti na ule wa tume ambao alisema ni salama na hauwezi kuingiliwa na mtu.
Awali, Nasa waliwasilisha malalamiko kwa waangalizi wa uchaguzi wa kimataifa wakiwataka wachunguze kuingiliwa mfumo wa kompyuta za IEBC na kuvurugwa matokeo ya kura za urais.
Hata hivyo, waangalizi hao walishauri Nasa iwasilishe malalamiko yake katika mamlaka husika kwa mujibu wa sheria kama IEBC au mahakamani.
Nasa walitaka mgombea wao Raila Odinga atangazwe mshindi wakati kura zilikuwa bado zinajumlishwa vituo vya kukusanyia matokeo katika maeneo mbalimbali ya nchi.

No comments: