ANGALIA LIVE NEWS

Thursday, August 10, 2017

Waangalizi wa uchaguzi Kenya wazungumza na timu ya Raila Odinga

Waangalizi wa kimataifa wa Umoja wa Afrika na Jumuiya ya Madola wametoa ripoti yao ya awali kuhusu uchaguzi Kenya na mazungumzo yao na kambi ya upinzani ya National Super Alliance (Nasa) waliowasilisha madai kwamba kompyuta za IEBC zimeingiliwa na upande Jubilee kuvuruga matokeo halisi ya kura.
Kiongozi wa ujumbe wa Waangalizi wa Umoja wa Afrika, Thabo Mbeki alisema ni kweli mgombea wa Nasa, Raila Odinga na ujumbe walikutana nao wakiwa na nyaraka za madai kuhusiana na Jubilee walivyovamia kompyuta hizo.
Mbeki alisema waliwasikiliza na kuwaeleza kuwa watalifikisha suala hilo IEBC. Hata hivyo alisema Nasa walitaka waangalizi hao wafanyanyie kazi nyaraka hizo kwa kuchunguza.
"Kwa mtu kama sina utaalamu wa teknolojia kuniambia nichunguze ni sawa na kuniambia nifanye kazi ambayo sina ujuzi," alisema Mbeki.
Alisema kazi ya waangalizi ni kuangalia ni si kuchunguza, kwa kuwa wao jukumu lao ni kuangalia namna mchakato mzima ulivyofanyika kama ulifuata sheria za nchi husika na taratibu za kuheshimu demokrasia walizojiwekea katika Umoja wa Afrika.
Alisema tuhuma zote zilizotolewa na Nasa wameziwasilisha kwa mamlaka husika ndani ya Kenya.
Kwa upande wake mkuu wa ujumbe wa waangalizi wa Jumuiya ya Madola, Rais wa zamani wa Ghana, John Dramani Mahama alisema walikutana na Odinga na ujumbe wake na walitoa madai ya kompyuta za IEBC kuvamia huku wakiwa na nyaraka kama ushahidi wa madai yao, hata hivyo Mahama alisema nao waliwaeleza kwanza hawana utaalamu wa teknolojia hiyo, lakini jukumu lao ni kuangalia kama utaratibu mzima wa uchaguzi umefuata sheria na katiba ya nchi na madai mengine ya ukiukwaji wa taratibu yana utaratibu wake uliowekwa kwa mujibu wa sheria.

Chanzo: Mwananchi

No comments: