Warsha kuunganisha Mipango ya APRM na Mipango ya Serikali kufanyika Zanzibar
Warsha hiyo inalenga kujenga uwezo wa Watendaji wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ), katika kuoanisha (kuunganisha) Mpango Kazi wa APRM na mipango ya Maendeleo ya Zanzibar, hasa Mpango wa Kupunguza Umaskini na Kuleta Maendeleo Na. III.
Na itajadili masuala yafuatayo: Namna ya kuunganisha Mipango ya Maendeleo ya nchi, Agenda 2063 ya Umoja wa Afrika, Malengo Endelevu ya Milenia pamoja na Mpango Kazi wa APRM; Uzoefu wa nchi nyingine za Kiafrika katika kuunganisha Mipango yao ya Maendeleo na Mpango Kazi wa APRM na Mkakati wa Tathmini na Ufuatiliaji.
Warsha hiyo inagharamiwa kwa pamoja baina ya Shirika la Umoja wa Mataifa la Maendeleo ya Uchumi Barani Afrika pamoja na Serikali ya Jamhuri ya Muungano Tanzania.
Mwishoni inatarajiwa kuwa washiriki wataweza kuunganisha Mpango Kazi wa APRM na kuonda changamoto za Utawala Bora pamoja na Mipango ya Maendeleo ya Zanzibar kwa lengo la kutumia vizuri rasilimali zilizopo ili kujenga uhusiano kati ya Mipango hiyo pamoja na kukuza uwezo wa kitaasisi.
Hatua hiyo ni muhimu sana kwani itasaidia kwa kiasi kikubwa kukamilisha Taarifa ya kuondoa changamoto za Utawala Bora zilizobainishwa kwenye Ripoti ya Nchi. Na hatimaye nchi yetu itaweza kuwasilisha Ripoti ya Utekelezaji wa Mpango Kazi wa kuondoa changamoto hizo kwenye kikao cha Wakuu wa nchi wanaoshiriki mchakato wa APRM.
Inatarajiwa kuwa, kwa kutatua changamoto za utawala bora nchi itaweza kuendelea kuwa na amani na utulivu, kukuza uchumi, kuwa na maendeleo endelevu pamoja na kuharakisha Muungano wa Kikanda, na hatimaye kuwaondolea wananchi umaskini.
Tanzania ni mojawapo kati ya nchi 36 za Afrika zinazoshiriki mchakato wa APRM, nayo imeshawasilisha Ripoti yake ya kwanza kwa Wakuu Wenza wanaoshiriki mchakato huu mwaka 2013. Hivi sasa ipo katika hatua ya utekelezaji wa Mpango Kazi wa kuondoa changamoto zilizobainishwa kwenye Ripoti ya Utawala Bora.
Imetolewa na APRM Tanzania
22 Agosti 2017
No comments:
Post a Comment