ANGALIA LIVE NEWS

Tuesday, September 26, 2017

NAPE: WANANCHI WA MTAMA WANAHOJI HIZO NDEGE ZA BOMBARDIER ZINA FAIDA GANI KWAO KIJIJINI

Wananchi wa jimbo la Mtama mkoani Lindi wamemhoji mbunge wao, Nape Nnauye kuhusu ndege aina ya Bombardier, wakitaka kujua inawasaidiaje.

Ndege mbili aina ya Bombardier Dash 8 Q400 zilinunuliwa na Serikali kwa ajili ya kulifufua shirika la usafiri wa anga la Air Tanzania (ATCL), ambalo lilikuwa limezorota na kutishia uhai wake.

Ndege hizo zilizinduliwa na Rais John Magufuli Septemba 28, 2016 jijini Dar es Salaam.

Lakini wananchi wa Mtama bado hawajaona umuhimu wake na walimuhoji Nape, ambaye alikuwa Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo.

Jana Nape aliandika katika akaunti yake ya Twitter kuhusu utashi huo wa wananchi wake kuhusu Bombardier.

“Watu hawa wanapambana na hali zao! Waliniuliza bombardier ndiyo nini” na sie wa vijijini tutafaidikaje au ni kwenu mjini tu!?” ameandika Nape katika akaunti hiyo.

Alipoulizwa , Nape aliyewahi kuwa katibu wa itikadi na uenezi wa CCM, alithibitisha kutuma ujumbe huo, akisema ni swali aliloulizwa na wanakijiji.

“Mimi sijui kwa nini mnauliza sana hicho kitu.Mimi nilikuwa jimboni kwangu nazungumza na wananchi kuhusu korosho, mwanakijiji mmoja akauliza kwamba hiyo Bombardier ina faida gani? Na mimi nimeripoti maneno yake. Si maneno yangu.

“Suala si mimi kuwa na cheo, mimi ni mbunge wa wananchi. Hilo swali hata wewe ukiliuliza hapo mtaani utapata majibu matano tofauti.
“Nilikuwa nazungumza na wanavijiji kuhusu fedha zinazotolewa na Serikali kuhusu korosho, mbaazi na mazao mengine, ndipo nikaulizwa na mimi nimeripoti kwa rafiki zangu nilivyoulizwa.”

Lindi na Mtwara ni kati ya mikoa iliyokuwa inafikika kwa shida kabla ya Serikali kujenga barabara zilizorahisisha usafiri. Pamoja na usafiri wa barabara, Air Tanzania imeanzisha usafiri wa anga kwa ajili ya kuhudumia wasafiri wengine kwenda na kutoka mikoa hiyo ambayo hivi sasa inachangamshwa na uwekezaji katika gesi na viwanda vya saruji.

No comments: