Advertisements

Friday, September 15, 2017

POLISI DAR YAPIGA MARUFUKU MIKUSANYIKO YA MAOMBI

Jeshi la Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam limesema halitaruhusu mkusanyiko wa aina yoyote utakaopangwa kwa kigezo cha kufanya maombi.
Jeshi hilo limesema halikatazi watu kufanya maombi, lakini utaratibu wa kufanya jambo hilo upo wazi na unatekelezwa katika sehemu maalumu.
Kamanda wa Polisi wa kanda hiyo, Lazaro Mambosasa, amewaambia waandishi wa habari leo Ijumaa Septeba 15 kwamba suala la maombi halijaanza leo wala jana hivyo lazima watu wafuate utaratibu wa kufanya maombi.
“Hivi mtu anatoka Kimara, mwingine Mwenge halafu mnakutana sehemu kisha mnakwenda kufanya maombi Msimbazi, haya hayatakuwa maombi bali ni maandamano na hatutayaruhusu na wakithubutu kufanya hivi hawatazidi hatua tano, wataangukia mikononi mwa polisi,” amesema Mambosasa na kuongeza:
“Ukiwa kanisani wewe fanya maombi hata usiku kuchwa hatutashukulika na wewe.”
Kamanda Mambosasa amesema maombi yanafanyika katika sehemu maalumu lakini kitendo cha watu kujikusanya sehemu moja kisha kuanza safari ya kwenda kufanya maombi mahali fulani huko siyo sahihi bali ni kutotii sheria zilizopo.
Kuhusu watu waliokamatwa Temeke, ambao wanadaiwa kuwa ni wafuasi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Kamanda Mambosasa amesema; “Wale ni wahalifu na wenyewe wanajua walichokitenda. Hatukataza watu kujitolea damu na mara zote wananchi wanahimizwa kuchangia damu.”
Katika hatua nyingine, Kamanda Mambosasa amesema askari polisi wameapiga risasi na kuwaua watu watatu wanaodhaniwa kuwa ni majambazi. Amesema watu hao waliuawa katika majibizano ya risasi na polisi.
Amesema tukio hilo lilitokea Mbiku Chamazi wakati watu hao wakiwa katika harakati kufanya uporaji kwenye maduka ya kutuma na kupokea fedha kwa njia ya mitandao ya simu.
“Walikuwa watu watano na walipofika eneo lile walianza kufyatua risasi baada ya kubaini uwepo wa polisi eneo hilo. Polisi walipojibu mashambuzli hayo walifanikiwa kuwajeruhi majambazi watatu kati yao huku wawili wakikimbia,”anasema Kamanda Mambosasa.
Kamanda Mambosasa amesema watu hao walifariki dunia baada ya kufikishwa katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH), kwa ajili ya matibabu.

Chanzo: Mwananchi

1 comment:

Anonymous said...

KWANI KUNA SHIDA GANI MMOJA AKITOKA KIMARA MWINGINE MWENGE WAKIKUTANA KUSALI KURASINI???? HUKU SASA NI KUKIUKWA KWA HAKI ZA BINADAMU NCHI YETU INAKUWA KAMA RWANDA SASA, UDIKTTETA UCHWARA UMETAMALAKI, MAUAJI YA WASIO NA HATIA YANAENDELEA, USHAMBULIAJI WA WANASIASA NA UCHOMAJI MOTO WA NYUMBA ZA WANASIASA SASA UMEKUWA NI JAMBO LA KAWAIDA.