ANGALIA LIVE NEWS

Friday, September 22, 2017

PROFESA MBARAWA ATOA MIEZI SITA KWA TBA KUKAMILISHA MRADI WA NYUMBA MAGOMENI

 Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Prof. Makame Mbarawa akizungumza na watendaji wa Wakala wa Ujenzi nchini wakati alipotembelea kukagua mradi wa ujenzi wa nyumba eneo la Magomeni mapema hii leo jijini Dar es Salaam.
 Mkurugenzi wa Huduma za Ushauri toka Wakala wa Ujenzi nchini Daud Kondoro akifafanua jambo kwa Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Prof. Makame Mbarawa wakati Waziri huyo  alipotembelea kukagua mradi wa ujenzi wa nyumba eneo la Magomeni mapema hii leo jijini Dar es Salaam.
 Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Prof. Makame Mbarawa aliyenyoosha mkono akikagua mradi wa ujenzi wa nyumba eneo la Magomeni mapema hii leo jijini Dar es Salaam.
 Mafundi wakiendelea na ujenzi wa nyumba za makazi eneo la Magomeni mapema hii leo wakati Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Prof. Makame Mbarawa alipotembelea kukagua mradi wa ujenzi wa nyumba eneo la Magomeni mapema hii leo jijini Dar es Salaam.
Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Prof. Makame Mbarawa akizungumza na watendaji wa Wakala wa Ujenzi nchini wakati alipotembelea kukagua mradi wa ujenzi wa nyumba eneo la Magomeni mapema hii leo jijini Dar es Salaam.
Picha na Eliphace Marwa - Maelezo

Na Ismail Ngayonga - MAELEZO
WAZIRI wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasilinp Profesa Makame Mbarawa ametoa muda wa miezi sita hadi kufikia Mwezi Machi mwaka 2018 kwa Wakala wa Majengo Tanzania (TBA) kukamilisha mradi wa ujenzi wa Nyumba za kisasa katika eneo la Magomeni Kota Jijini Dar es Salaam.
Waziri Mbarawa aliyasema hayo leo (Septemba 22, 2017) Jijini Dar es Salaam wakati alipokuwa akikagua maendeleo ya ujenzi wa mradi huo wa nyumba za makazi unaotarajia kunufaisha jumla ya 656 mara baada ya kukamilika kwake.

Waziri Mbarawa alisema malengo ya Serikali ni kuhakikisha kuwa mradi huo unakamilika kwa wakati, ambapo pamoja na kiwango cha ujenzi wa mradi huo kufikia asilimia 30 hadi sasa tangu kuanza kwa mradi huo mwaka jana aliitaka TBA kuhakikisha kuwa inaongeza kasi zaidi katika muda uliotolewa.

“Tarehe 30 Septemba mwaka huu tulipanga mradi huu uwe umekamilika, lakini bahati mbaya tumeshindwa hata hivyo tunajipanga upya kuhakikisha kuwa hadi mwezi Machi 2018 mradi huu unakamilika na kaya 656 zinapatiwa makazi” alisema Profesa Mbarawa

Aidha Profesa Mbarawa alisema Serikali imetenga kiasi cha Tsh. Bilioni 2O kwa ajili ya utekelezaji wa mradi huo, ambapo hadi sasa kiasi cha Tsh. Bilioni 10 tayari zimekwishatolewa, hivyo aliitaka TBA kuhakikisha kuwa mradi huo unakuwa wa mfano katika viwango vya juu vya ubora wa makazi.

Profesa Mbarawa aliihakikishia TBA kuwa Serikali ipo karibu yao ili kuhakikisha kuwa changamoto mbalimbali zinazojitokeza katika ukamilishaji wa mradi huo zinaweza kupatiwa ufumbuzi wa haraka ili kuhakikisha kuwa mradi huo unakamilika katika kipindi na muda uliowekwa.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Huduma za Ushauri wa TBA, Daud Kondoro alisema TBA ilipanga kukamilisha mradi huo mwaka huu, ambapo hata hivyo ilikabiliana na changamoto gharama ya bei katika vifaa ikiwemo nondo, ambazo zilifikia kuuzwa kiasi cha Tsh. Bilioni 2 kwa tani.

Aliongeza kuwa, hata hivyo kwa sasa changamoto hiyo imeweza kupatiwa ufumbuzi ambao umefanya mazungumzo na wasambazaji wengine wa nondo na vifaa hivyo pamoja na magari matatu na mtambo maalum wa kuchakata zege umeweza kununuliwa na kuanza kazi katika eneo la mradi.

Tulipokuwa tunajenga Hosteli za Wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, tuliweza kupata vifaa vyote hivi kwa bei ya chini sana, lakini kuanzia mwezi Oktoba mwaka jana wakati wa kuanza mradi huu, bei ya vifaa ikiwemo nondo ilipanda maradufu” alisema Kondoro.

Aidha aliongeza kuwa kufuatia kupatikana kwa vifaa hivyo, kila baada ya siku 12 kutoka sasa, katika utaratibu waliojiwekea Wakandarasi wa ujenzi huweza kutoa mirunda maalum katika ardhi na kuanza kujenga ghorofa mpya.

No comments: