ANGALIA LIVE NEWS

Saturday, September 30, 2017

SEKTA BINAFSI ZAONGEZA NGUVU KATIKA KUBORESHA HUDUMA ZA AFYA SINGIDA.



Mratibu wa Ukimwi Mkoa wa Singida Dkt Mohamed Mbalazi akitoa mada katika mkutano ulijadili uboreshaji wa ushirikiano baina ya serikali na wadau wa sekta binafsi zinazotoa huduma ya Afya Mkoani Singida.

Afisa Lishe Mkoa wa Singia Teda Sinde akifafanua jambo katika mkutano ulijadili uboreshaji wa ushirikiano baina ya serikali na wadau wa sekta binafsi zinazotoa huduma ya Afya Mkoani Singida.
Mratibu wa Kifua Kikuu na Ukoma Mkoa wa Singida Dkt Evans Mlay (wa kwanza kushoto) akipitia dondoo, kabla ya kuwasilisha mada iliyoonyesha mchango mkubwa wa wadau Sekta ya Afya katika mapambano dhidi ya Kifua Kikuu Singida, Kulia kwake ni Afisa Mradi wa AMREF Mkoa wa Singida Donathapeace Kayoza.
Mwakilishi wa Kaimu Katibu Tawala Mkoa, Cosmas Sikali akizungumza na wadau wa sekta binafsi zinazotoa huduma katika Mkoa wa Singida.
Mganga Mkuu wa Mkoa wa Singida Dkt Salum Manyatta akisikiliza kwa makini maoni na michango mbalimbali ya wadau ambao ni taasisi na mashirika binafsi yanayotoa huduma za Afya Mkoani Singida.
Meneja Mradi wa EGPAF Kanda ya Kati Dkt Joseph Obedi akiandika baadhi ya mapendekezo ya kuboresha ushirikiano kati ya sekta binafsi na serikali katika uboreshaji wa huduma za Afya Mkoa wa Singida.

Wadau mbalimbali wa sekta binafsi wameweza kuongeza nguvu katika kuboresha sekta ya Afya Mkoani Singida kutokana na ushirikiano mzuri ulipo baina yao na serikali.

Hayo yamebainishwa katika mkutano maalumu wa siku mbili uliohitimishwa jana Mjini Singida, ambapo viongozi wa serikali, taasisi na mashirika 15 yanayotoa huduma za Afya na Ustawi wa jamii Mkoani hapa wamejadiliana namna ya kuboresha ushirikiano baina yao.

Mratibu wa Ukimwi Mkoa wa Singida Dkt Mohamed Mbalazi amesema katika mapambano dhidi ya Ukimwi na Virusi vya Ukimwi (VVU) Mkoani hapa, Sekta binafsi zimekuwa na mchango mkubwa.

Dkt Mbalazi amesema wadau hao wameweza kutoa dawa za kupunguza makali ya VVU, tiba lishe, mafunzo kwa watoa huduma wa afya, ufuatiliaji wa watumia wa dawa za VVU pamoja na kuandaa takwimu jambo ambalo limeboresha mapambano dhidi ya VVU na Ukimwi.

“Sisi kama watendaji wa serikali tunathamini na kutambua mchango wa wadau wa sekta afya kwakuwa ni nguzo muhimu sana, mfano wadau wetu shirika la EGPAF, wametenga bilioni 1.6 kwa ajili ya mapambano dhidi ya Ukimwi na maambukizi ya VVU” Mkoani Singida”, amesema na kuongeza kuwa,

“Fedha hizo zitaongea nguvu pale ambapo kuna changamoto au bajeti inakuwa haitoshelezi, lakini pia tunaendelea kutoa wito kwa wadua wengine waendelee kuongea nguvu na wigo wa ushirikiano kwakuwa lengo letu ni moja yaani kumsaidia mwananchi apate huduma bora za afya”, amesisitiza Dkt Mbalazi.

Naye Afisa Lishe Mkoa wa Singida Teda Sinde amesema wadau wamekuwa watekelezaji wazuri wa masuala ya Lishe Mkoani hapa hasa kwa ngazi ya jamii hivyo ushirikiano kati yao umekuwa wa manufaa makubwa.

Teda amesema mkutano huo wa wadau umewawezesha watendaji na viongozi wa serikali kuelewa kwa upana zaidi kazi wanazofanya wadau pamoja na changamoto wanazopitia ili waweze kusaidiana katika kuboresha hali ya Lishe Mkoani hapa.

“Mkutano huu umeongeza na kuboresha ushirikiano baina yetu na wadau wetu ambao wengi wao wanatoa chakula lishe na elimu ya lishe kwa akina mama wajawazito, watoto wenye umri wa miezi sita mpaka 59 na akina mama wanaonyonyesha watoto chini ya miezi sita”, ameeleza Teda.

Ameongeza kuwa mkutano huo umeweza kusaidia katika kupanga mikakati ya utoaji huduma ili kuepusha wadau wanaotoa huduma ya aina moja kutoelekeza nguvu katika maeneo yanayofanana au ambayo hayana uhitaji mkubwa kuliko mengine.

Akifungua Mkutano huo Mwakilishi wa Kaimu Katibu Tawala Mkoa, Cosmas Sikali aliwataka wadau kujadili sera, sheria, kanuni, maeneo ya kipaumbele katika miradi mbalimbali, mafanikio na changamoto katika utekelezaji wa mipango mikakati inayosisitiza ushirikiano kati ya Sekta ya Umma na binafsi.

Sikali amesema endapo nguvu hizi kwa pamoja zitaunganishwa na kuratibiwa vizuri kwa kiasi kikubwa changamoto zilizopo katika sekta ya afya na ustawi wa jamii pamoja na maradhi kwa wananchi yataweza kupungua.

Ameongeza kuwa serikali peke yake haitaweza kufikia malengo ya kupunguza vifo vya watoto, akina mama wajawazito na kuweza kudhibiti magonjwa ya kuambukiza na yasiyoambukiza, pamoja na kuboresha afya ya mazingira na kupata maji safi na salama bila kushirikiana na Sekta binafsi.

Kwa upande wake Mganga Mkuu wa Mkoa wa Singida Dkt Salum Manyatta amesema mkutano huo umeshirikisha wadau wote muhimu wanatoa huduma za afya na ustawi wa jamii mkoa wa Singida.

Dkt Manyatta amesema mkutano huo umeweka malengo na maazimio ya pamoja na wadau wa sekta binafsi ili kuimarisha sekta ya afya na ustawi wa jamii Mkoani Singida.

No comments: