Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Mhe. Ummy Mwalimu (katikati) akizindua vyumba viwili vya upasuaji wa watoto wadogo leo katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH). Kushoto ni Mkurugenzi Mtendaji wa Muhimbili, Profesa Lawrence Museru, Mwenyekiti wa Bodi ya Mfuko wa Wood na Archie, Sir. Ian Wood na maofisa wengine wakiwa kwenye uzinduzi huo leo.
Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Mhe. Ummy Mwalimu akiangalia baadhi ya vifaa vilivyotolewa na Mfuko wa Wood na Archie katika vyumba vya upasuaji wa watoto wadogo kwenye hospitali hiyo.
Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Mhe. Ummy Mwalimu akizungumza kabla ya kuzindua vyumba vya upasuaji wa watoto. Kushoto ni Mkurugenzi Mtendaji wa hospitali hiyo, Profesa Lawrence Museru, Mkurugenzi wa Huduma za Upasuaji wa Muhimbili, Dk. Julieth Magandi na kulia ni Mwenyekiti wa Bodi ya Wood na Archie, Ian Wood akiwa kwenye mkutano huo leo.
Baadhi ya watoto wanaotibiwa katika hospitali hiyo wakiwamo madaktari, wauguzi na baadhi ya watumishi wakimsikiliza Waziri Ummy Mwalimu leo.
Mkurugenzi Mtendaji wa Muhimbili, Profesa Lawrence Museru akizungumza leo kwenye mkutano huo kabla ya kuzinduliwa kwa vyumba vya upasuaji wa watoto.
Baadhi ya watumishi wa Muhimbili wakifuatilia mkutano huo leo
Profesa George Youngson akizungumza kwenye mkutano huo leo kabla ya kukabidhi vyumba vya upasuaji na wodi ya watoto yenye vitanda 25. Pembeni ni timu ya wataalamu wa Wood na Archie Foundation.
Mwenyekiti wa Bodi ya Mfuko wa Wood na Archie, Sir. Ian Wood akizungumza katika mkutano huo leo.
Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano na Huduma kwa Wateja, Aminiel Aligaesha akiwa na mmoja wa watoto ambaye amemweleza Waziri Ummy Mwalimu kwamba ndoto yake ni kuwa daktari. Waziri ameahidi kumsomesha mtoto ili kufikia ndoto yake.
Na John Stephen, Muhimbili
Serikali imesema itaendelea kuiwezesha Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) katika mikakati yake ya kutoa huduma bora za afya zikiwamo za ubingwa wa hali ya juu pamoja na upasuaji katika maeneo mbalimbali.
Kauli hiyo imetolewa leo na Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Mhe. Ummy Mwalimu katika hospitali hiyo wakati akizindua vyumba viwili vya upasuaji wa watoto wadogo (Pediatrick operating theatres) vyenye thamani ya Dola za Marekani 675,000 sawa na Tsh. 1.5 bilioni pamoja na uzinduzi wa wodi ya watoto yenye vitanda 25.
Katika uzinduzi huo Waziri Mwalimu ameitaka Muhimbili kutokutoa rufaa kwa mgonjwa yoyote ambaye anaweza kupatiwa mabatibabu katika hospitali hiyo.
“Narudia tena, hata kama ni mimi au kiongozi yoyote asipewe rufaa kama ugonjwa wake unaweza kutibiwa hapa, mimi naweza kuja hapa nikawashinikiza mnipeleke nje, msikubali, simamieni taaluma yenu. Kama madaktari wamezibitisha mgonjwa anaweza kutibiwa hapa, hakuna haja ya kupelekwa nje,” Mhe. Ummy.
Vyumba hivyo vya upasuaji vimewekewa vifaa vya upasuaji kwa msaada wa mfuko wa ARCHIE WOOD FOUNDATION ya Scotland. “Napenda kuwashukuru kwa namna ya pekee wahisani wetu Sir.Ian Wood na mtoto wako Garret Wood ambao mlipoletewa wazo la kuisaidia Hospitali ya Taifa Muhimbili kupitia taasisi yenu ya Archie Wood Foundation mlilipokea kwa mikono miwili na kulitekeleza. Nichukue nafasi hii kwa niaba ya Serikali chini ya Uongozi wa wa Rais Dkt. John Pombe Magufuli kuwashukuru sana kwa msaada huu,” amesema Waziri Ummy Mwalimu.
Waziri ameutaka uongozi wa Muhimbili kuweka mpango mzuri wa matengenezo kinga ili kuhakikisha kila kifaa kinatunzwa na kutumika kwa lengo lililokusudiwa.
Naye Mkurugenzi wa Muhimbili, Profesa Lawrence Museru amefafanua kuwa msaada uliotolewa na mfuko huo kuwa ni taa za kufanyia upasuaji (operating lights), mashine za usingizi (anesthetic machines with monitors), mashine za kuzuia damu isiendelee kupotea wakati wa upasuaji (diathermy machines), mashine ya kutasisha vifaa vya upasuaji na vifaa vyake, vitanda vya kufanyia upasuaji (operating tables) na vifaa mbalimbali vya upasuaji (surgical kits).
Profesa Museru amesema kuwa leo wamepatiwa vifaa vya kisasa kwa kutumia vyumba hivyo viwili na kwamba upasuaji utakuwa ikifanyika mara 10 kwa wiki badala ya mara tatu kwa wiki kama ilivyokuwa awali.
“Hii itaondoa kero ya msongamano kwa watoto wanaohitaji kufanyiwa upasuaji wakati mwingine ilibidi wasubiri kwa muda wa miaka miwili ili kufanyiwa upasuaji,”amesema Profesa Museru.
No comments:
Post a Comment