Advertisements

Monday, September 25, 2017

Wanafunzi 214 Ukerewe, Rorya wapata mimba

Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, John Mongela
Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, John Mongela

WANAFUNZI 214 wa shule za msingi na sekondari katika Halmashauri ya Wilaya ya Ukerewe mkoani Mwanza na Rorya Mkoa wa Mara wamebainika kuwa na ujauzito katika kipindi cha Januari mwaka huu hadi sasa na hivyo kulazimika kukatisha masomo na kushindwa kutimiza ndoto zao.

Kati ya hao, Wilaya ya Ukerewe mkoani Mwanza waliopata mimba ni 126 wakati Wilaya ya Rorya Mkoa wa Mara ni wanafunzi 88 waliokuwa wakisoma katika shule mbalimbali za msingi na sekondari.

Mkurugenzi Mtendaji wa Wilaya ya Ukerewe, Frank Bahati aliyasema hayo jana wilayani humo katika ziara iliyolenga kuangalia mazingira ya ujifunzaji na ufundishaji wa Kusoma, Kuandika na Kuhesabu, KKK pamoja na kuangalia hali ya uboreshaji wa miundombinu ya shule kupitia Mradi wa Lipa Kulingana na Matokeo (P4R).

Bahati alisema wanafunzi waliopata ujauzito, 118 ni wa shule za sekondari na nane ni wa shule za msingi na tayari kesi zimefunguliwa mahakamani dhidi ya wahusika. Alisema kutokana na tatizo hilo wamekuwa wakibuni njia mbalimbali za kukabiliana na tatizo hilo ikiwemo kufanya operesheni na kuwakamata wahusika na kuwafikisha katika vyombo vya kisheria, lengo likiwa ni kuboresha elimu katika wilaya hiyo.

“Hizi mimba ni kiwango kikubwa ambacho kinatishia kwa mustakabali wa taaluma ya Wilaya yetu, hivyo tunatoa elimu ya afya kwa shule za msingi na sekondari...pia tuna utaratibu wa kuwapima ujauzito mara kwa mara,” alieleza.

Pia alisema wanafanya vikao vya mara kwa mara na kamati za shule, wazazi, walezi, waalimu na jamii inayozunguka shule na kuwaelimisha kuhusu malezi bora pamoja na kuwahamisha kutoa ushirikiano kwa kuwataja wanaowapa wanafunzi ujauzito.

“Kumekuwa na ukimya wa kutotaka kuwataja wanaowapa mimba wanafunzi na kupotosha ukweli kati ya muhusika, mzazi na mwanafunzi...hivyo bado tatizo ni kubwa na tumekuwa tukichukua hatua za ziada kushughulikia tatizo hili.

Sisi kama Halmashauri tumekusudia kuwalinda wanafunzi wetu,” alisema. Pia alisema zaidi ya Sh milioni 500 zilizotolewa na serikali kupitia Mradi wa P4R zimesaidia kuboresha miundombinu na kujenga mabweni katika shule za Sekondari Pius Msekwa na Bujingo zilizopo wilayani humo na hivyo husaidia kupunguza changamoto ya wanafunzi kutembea umbali mrefu.

Aidha, alisema kupitia mpango wa Kusoma, Kuandika na Kuhesabu (KKK) umesaidia kupunguza tatizo la wanafunzi wanaomaliza elimu ya msingi bila kujua KKK. Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya hiyo, Estomih Chang’ah alisema tatizo la mimba katika wilaya hiyo linasikitisha na kuhuzunisha na linachangiwa na malezi ya kifamilia kuwa dhaifu kutokana na shughuli za uvuvi.

“Maeneo yetu mengi ni visiwa, hivyo wananchi wanatoka umbali mrefu... kama tungekuwa na hosteli na mabweni ya kutosha tungepunguza tatizo hili. Pia tumefungua kesi zaidi ya 10 mahakamani dhidi ya wanaowapa mimba wanafunzi na zipo katika hatua mbalimbali,” alisema mkuu wa wilaya.

Akizungumza katika kikao cha madiwani wilayani Rorya, Diwani wa Viti Maalumu, Edna Charles alisoma taarifa ya idadi ya wanafunzi waliopata ujauzito katika kipindi cha mwaka mmoja, na kueleza kuwa katika robo ya kwanza wanafunzi 25 walipata mimba, ya pili wanafunzi 17, ya tatu wanafunzi 23 na katika robo ya nne wanafunzi 23 walipata mimba na kufanya idadi ya wanafunzi 88

HABARI LEO

No comments: